ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 22, 2011

Malecela aionya CCM




Waziri Mkuu Mstaafu John Malecela
ASEMA KAMA INATAKA KUENDELEA KUSHIKA DOLA IWAFUKUZE WATUMUMIWA WA UFISADI
Boniface Meena
WAZIRI Mkuu mstaafu, John Malecela amekitaka Chama chake cha Mapinduzi (CCM) kuwachukulia hatua za haraka wala rushwa walioko ndani yake kuanzia ngazi ya juu hadi chini kama kinataka kuendelea kushika dola.Kauli ya Malecela ambaye ni Mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu (CC) ya CCM, inakuja kipindi ambacho mpango mkakati wa chama hicho wa kujivua gamba unaonekana kupigwa kalenda.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi nyumbani kwake Sea View, Upanga Dar es Salaam jana, Malecela alisema ni muhimu wala rushwa wakaondolewa haraka bila kucheleweshwa ili chama kiendelee kuwapo.

Malecela alinukuu maandiko ya Mungu katika Ukristo akisema: "Mimi ni Mkristo, maneno ya Mungu yanasema ukiwa na jicho bovu na ukiona linakuzuia kuingia mbinguni litoe ili uweze kuingia."

"Kama kuna corrupt people in the party (wala rushwa ndani ya chama), ni kuwaondoa ili CCM iendelee kuwapo."

Hata hivyo, alisema suala la kujivua gamba haliwezi kuwa kwa watu wanne au watano, bali chama kisafishe wala rushwa wote waliopo ndani yake kuanzia ngazi ya juu hadi chini.

Kujivua gamba
Mpango wa kujivua gamba kwa CCM ulianza kutangazwa na Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete wakati wa maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa chama hicho yaliyofanyika mkoani Dodoma hivi karibuni akisema yalikuwa na lengo la kukihuisha.

Rais Kikwete alisema chama hicho kiliwahi kufanya mabadiliko mbalimbali kuanzia TANU kwa lengo la kujisafisha na kujipanga upya, baada ya kujifanyia tathmini kuhusu mwelekeo wake kwa wakati husika.

Mpango huo baadaye ulijadiliwa katika CC iliyokutana Mjini Dodoma mnamo Aprili ambayo pamoja na mambo mengine utekelezaji huo ulianza kwa Kamati hiyo Kuu kujiuzulu yote na kusukwa upya huku baadhi ya watuhumiwa akiwamo Andrew Chenge kutupwa nje.

Katika kikao hicho, ilitangazwa watuhumiwa wa ufisadi ukiwamo wa Richmond, Rada na Kagoda iliyochota Sh40 bilioni katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wangepaswa kujipima na kuachia nafasi zao ndani ya siku 90 lakini hadi kikao cha CC cha mwezi uliopita, watuhumiwa hao walikuwa hawajajiuzulu.

Badala yake, CC ilitoa muda zaidi kusubiri uamuzi wa kikao cha Halmashauri Kuu (Nec) ya chama hicho inayotarajiwa kukutana mwezi ujao.Hata hivyo, hakuna dalili zozote za watuhumiwa wakubwa wanaotajwa katika kashfa hizo za rada na Richmond kujiuzulu huku chama kikionekana kuwa katika wakati mgumu kuwafukuza, huku hatua ya kutowafukuza ikitajwa kama kitanzi kinachoweza kukimaliza kisiasa.

Tuhuma za kumiliki shamba hekta 100
Akizungumzia madai yaliyotolewa Bungeni hivi karibuni na Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee kwamba anamiliki hekta 100 za shamba huko Mvomero, Morogoro, Malecela alisema hana habari juu ya umiliki huo akisema: "Sina hati yake na wala sijawahi kufika kuliona, hata sijui liko sehemu gani ya Mvomero."

Alisema wakati Serikali ilipoipa Mvomero hadhi ya wilaya, iliwapa baadhi ya viongozi mashamba ili waendeleze maeneo hayo au wavute wawekezaji katika wilaya hiyo."Mimi niliambiwa nimepewa hekta 100 lakini sijawahi kufika kwenye eneo hilo, hata hati ya shamba hilo sina hivyo ni kusema sina shamba Mvomero."

"Ambaye analitaka shamba hilo akalichukue au kama kuna mtu anayefikiri kuwa ana hati ya shamba hilo aende wizarani athibitishe."

"Ni miaka 10 imepita tangu niambiwe suala hilo, wakati huo Mkuu wa Wilaya ya Mvomero akiwa ni (Samwel) Kamote, lakini sheria za kutoendeleza mashamba si zinajulikana kama lipo tu kwa nini lisichukuliwe?"

Malecela alisema asingeweza kupeleka trekta kutoka Dodoma kwenda kulima Mvomero hekta 100 kwa kuwa uwekezaji unahitaji zaidi ya hekta 300.

Alichokisema Mdee bungeni
Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe (Chadema), akisoma bajeti mbadala ya upinzani kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka 2011/12 aliwataja baadhi ya viongozi wa CCM wakiwamo Marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa akiwatuhumu kuhodhi maeneo makubwa ya ardhi mkoani Morogoro huku wakishindwa kuyaendeleza. Hata hivyo, Mkapa anaelezwa kuendeleza shamba lake.

Katika orodha hiyo pia ametajwa Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Katibu Mkuu wa CCM mstaafu, Philip Mangula, aliyekuwa Naibu wake (Tanzania Bara), Hassan Ngwilizi na Mwenyekiti wa CCM mkoani Mbeya, Nawab Mulla.

Mdee alisema umiliki wa maeneo makubwa ya ardhi unawanyima fursa wananchi wa kawaida kupata maeneo kwa ajili ya shughuli za maendeleo na kuongeza kwamba, vigogo hao kwa kutumia nafasi zao waliwanyang’anya wananchi ardhi hiyo na kujimilikisha wenyewe lakini kwa sehemu kubwa wameshindwa kuyaendeleza.

“Mheshimiwa Spika, matatizo ya ardhi kwa wakubwa kunyang’anya wanyonge imekumba pia Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ambako mgogoro huu unakumba shamba namba 299 iliyokuwa Narco Ranches lenye ukubwa wa hekta 49,981," alisema na kuongeza:

“Taarifa za kiuchunguzi zinaonyesha kuwa maeneo yaliyokuwa yamepangwa kugawiwa kwa wanavijiji wa Kijiji cha Wami, yamegawiwa wanavijiji wafuatao,’’ alisema na kuanza kuwataja vigogo hao kwa majina mmoja baada ya mwingine.

Akitoa orodha hiyo, Mdee alisema  Mangula anamiliki hekta 2,000, Mwinyi hekta 2,000 na Mkapa hekta 1,000 ambaye hata hivyo, ndiye pekee aliweza kuliendeleza shamba lake.

Katika orodha ya Mdee alimtaja pia  Sumaye kwamba anamiliki hekta 500, Malecela hekta 100 na Ngwilizi ambaye anamiliki hekta 100 huku akisisitiza orodha hiyo ni ndefu.Mdee alitaka Serikali itoe maelezo kwamba ni vigezo vipi vilitumika kuwagawia ardhi viongozi hao huku wakiwanyima ardhi wananchi wa maeneo husika.

Mwananchi

No comments: