ANGALIA LIVE NEWS
Monday, August 22, 2011
Mwinyi ataka wacha Mungu waongoze taifa
Ibrahim Yamola
RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi amesema nchi inatakiwa kuongozwa na viongozi wanaofuata maadili ya dini.Kauli ya Mwinyi maarufu kama Mzee Ruksa inakuja kipindi ambacho nchi inatikiswa na matukio makubwa ya ufisadi na ukiukaji maadili ya uongozi wa umma.Akizungumza kwenye hafla ya mashindano ya kuhifadhi Qur’an Tukufu yaliyoshirikisha nchi 10 za Afrika yaliyofanyika Dar es Salaam jana, Mzee Mwinyi alisema kiongozi mwenye maadili ya dini ataongoza kwa kumuogopa Mungu.
“Ili kuwapata viongozi waliokuwa wema na wenye kuongoza kwa usawa na haki, ni lazima watoke katika maadili ya kidini,” alisema Mwinyi.Alisema sababu za kuwapata viongozi wenye maadili ya kidini ni kwamba wataongoza kwa kumwogopa Mungu na hawatafanya kama wajuavyo.
Alisisitiza: “Viongozi watakuwa wanaongoza kwa kumwogopa Mungu, hivyo kuwa na usawa na kuleta maendeleo katika taifa letu.” Katika hafla hiyo, Mwinyi aliwataka wananchi kushirikiana katika shughuli za maendeleo kwani huo ni wajibu wa kila mwananchi.“Kila mtu anao wajibu wa kuchangia maendeleo ya Tanzania na siyo ombi. Ni lazima kwa kila mtu kuonyesha juhudi binafsi ili kuliweka taifa letu sehemu nzuri ya maendeleo,” alisema Mwinyi.
Rais huyo wa zamani alisema hata mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya na makatibu wakuu wacha Mungu watafanya kazi yao kwa kumwogopa Mungu na njia mojawapo ya kuwapata ni kuhifadhi Qur’an tukufu.
Mara baada ya kuwataja makatibu wakuu katika orodha ya viongozi wanaotakiwa kuwa na maadili ya ki-Mungu, watu waliohudhuria hafla hiyo waliangua kicheko na kumlazimu kukatisha hotuba yake hiyo na kusema: “Kwa kuwa nia yangu ilikuwa kumkaribisha mgeni rasmi tu hivyo ngoja nimwachie nafasi aje kutoa nasaha zake.”
Mgeni rasmi, Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal aliwataka Waislamu kutumia kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani kusoma na kuielewa Qur’an tukufu.
Dk Bilal aliwataka wanazuoni wa Kiislamu nchini kutafsiri na kufikisha mafunzo ya Qur'an tukufu kwa jamii yote.
Ujumbe katika kitabu hicho kitukufu, alisema unaweza kuleta tofauti kubwa katika jamii kama utaeleweka vema na kufuatwa, akawaonya Waislamu kuacha kupoteza muda kwa kupiga domo badala yake waketi chini na kuisoma na kuielewa Qur'an.
“Ni lazima tutenge muda kuisoma na kuishi kwa misingi ya Qur'an. Tunakosa baraka nyingi za Mwenyezimungu kwa kuacha kufanya hivyo ... kitabu kinaamrisha upendo na haki kwa wote,” alisema Dk Bilal.
Awali, Mratibu wa Mashindano hayo, Othman Kaporo alisema mashindano hayo yalianza kufanyika tangu mwaka 1995 yakishirikisha wakazi wa Dar es Salaam pekee.
“Tulianza kwa kuwahusisha washiriki kutoka Mkoa wa Dar es Salaam pekee, lakini mwaka jana nchi zote za Ukanda wa Afrika Mashariki zilihusika na kwa mwaka huu tumeshirikisha nchi 10 za Afrika,” alisema.
Kaporo alizitaja nchi zilizoshiriki mashindano hayo ni Ethiopia, Sudan, Kenya, Msumbiji, Uganda, Nigeria, Burundi, Somalia, Misri na wenyeji Tanzania.
Katika mashindano hayo yaliyoshirikisha washiriki wavulana wenye umri kati ya miaka 15-18. Mshiriki kutoka Sudan Juhuddin Adam alishika nafasi ya kwanza na kupata zawadi ya Sh5 milioni.Mshiriki kutoka Zanzibar, Kombo Bahi Makame alishika nafasi ya pili na kupata zawadi ya Sh3 milioni na mshiriki kutoka Misri Mohammad Sad Tawfiq alishika nafasi ya tatu na kupata zawadi ya Sh2 milioni.
Alisema ni wakati sasa umefika kwa wazazi kuweka kipaumbele katika elimu ya dini ili kuwapata viongozi watakaokuwa na maadili na kuwa na jamii inayomwogopa Mungu
“Kama tutawalea vizuri watoto wetu kwa kuwapa elimu ya kidini, tutakuwa na jamii yenye maadili bora kwani hivi sasa tunaona wenyewe jamii yetu inakoelekea” alisema Kaporo.
Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment