
Pamela Chilongola
KAIMU Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadiki, jana aliahirisha kwa muda mkutano kati yake na waandishi wa habari kwa kile alichodai ni kukosekana kwa luninga.
Awali, mkutano huo ulipangwa kufanyika muda wa saa 5:00 asubuhi jambo ambalo waandishi karibu 10 wa magazeti na radio walifika bila kuchelewa.Hata hivyo wakati waandishi hao wakisubiri, mkuu wa mkoa alikuwa ndani akiendelea na shughuli za kiofisi.
Baadhi ya waandishi waliamua kumuuliza ofisa habari wa mkoa sababu za kuchelewa kuanza mkutano huo ambaye katika hali ya uwazi alisema mkuu huyo asingeweza kuanza kikao kwa vile watu wa TV hawakuwapo.
Ofisa wa habari huyo alisema kutokana na kuchelewa kwa vyombo vya TV, mkuu huyo asingeweza kufanya mkutano.
”Kwa hiyo atakwenda kwanza Lugalo kuuaga mwili wa marehemu Luteni Jenerali Silas Mayunga, lakini kama waandishi wa TV wangewahi angemaliza mkutano huu”, alisema. “Waliowaangusha ni watu wa TV, angefika hata mmoja mkutano ungefanyika, lakini kutokana na kuchelewa kwao itabidi msubiri hadi hapo atakaporudi," “alisema ofisa huyo ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja.
Alisisitiza, "waandishi mliopo ni magazeti, angewahi moja wa vyombo vya TV, tungeanza mara moja, muda umepita itabidi aende halafu baadaye ufanyike mkutano huu.”
Ghafla , mkuu wa mkoa alitoa ndani ya ofisi na kuwaaga waandishi akisema ‘naelekea kwenye msiba hivyo mkutano utafanyika saa 6:00 mchana’. Hata hivyo, Sadiki aliingia kwenye mkutano wa waandishi wa habari saa 6:40, ambapo kabla ya kuanza mkutano aliomba msamaha kwa yale yaliyojitokeza na kusema yaliingilia na msiba na kwamba hakutegemea kama angeanza muda huo.
Akizungumza katika mkutano huo aliosema vyandarua vya Sh3.2 milioni vinatarajia kugawiwa kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam, ili kupambana na ugonjwa wa malaria.Sadiki, alitangaza pia kuanza kwa zoezi la kuandikisha wananchi kwa ajili ya kugawiwa vyandarua hivyo vyenye dawa ya kudumu.
Alifafanua kwamba ugawaji huo ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Jakaya Kikwete ya kugawa vyandarua kwa kila mwananchi nchini, ikiwa ni njia mojawapo ya kupambana na ugonjwa wa malaria.“Tayari zoezi la ugawaji vyandarua limeshafanyika kwenye mikoa 15 nchini, jumla ya vyandarua 3.2 milioni vinatarajiwa kugawiwa kwa wananchi wa Dar es Salaam," alisema.
Pia, alisema zoezi la uandikishaji kwa ajili ya vyandarua hivyo litazinduliwa Agosti 12 hadi Septemba 2, mwaka huu ambalo ni marudio linawalenga wananchi wote ambao hawakupata fursa ya kuandikishwa kwenye zoezi la awali, mapema mwaka huu.
No comments:
Post a Comment