ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 30, 2011

Rage, Saad Kawemba wazikunja TFF


TFF yaigomea Yanga nembo mpya Voda
Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage
Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, alikaribia kuzipiga na Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Saad Kawemba, nje ya ofisi za TFF jana baada ya kutokea kutoelewana kwa wawili hao.
Taarifa kutoka kwa mashuhuda wa tukio hilo zilidai kuwa kutofautiana kwa wawili hao kulifuatia maneno ya dharau yaliyotolewa Rage kuhusu suala la uhamisho wa mshambuliaji wa Simba, Gervais Kago, ambaye tishio la kuzuiwa kwake kucheza mechi ya Ngao ya Hisani dhidi ya Yanga, lilihatarisha kutofanyika kwa mechi hiyo ambayo Wekundu wa Msimbazi walikuja kushinda 2-0.
Rage, ambaye aliitwa TFF pamoja na Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, ili wakajieleze kwa kauli zao za kutishia kugomea mechi hiyo, alidaiwa kutoa kauli hiyo ya dharau akiwa mbali na Kawemba lakini kiongozi huyo wa TFF alifikishiwa taarifa hizo na akatoka ndani ya ofisi aliyokuwa wa shirikisho hilo na kuja moja kwa moja kutaka kumvaa Rage na ndipo kizaazaa kilipozuka na watu kuanza kujaa kabla ya Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah na Sendeu kuwaamua wawili hao.

Alipoulizwa kwa njia ya simu jioni jana, Osiah alithibitibisha kutokea kwa kutofautiana baina ya wawili hao.
"Tukio lilikuwepo lakini si kubwa kama linavyovumishwa, ilitokea kutofautiana kidogo baina yao na tukawepo kusaidia kuweka hali sawa," alisema Osiah bila ya kutaka kueleza kwa undani zaidi.
Wiki iliyopita, Rage alimuomba radhi Kawemba kufuatia kugongana kwa kauli zao kuhusu utata uliojitokeza wakati wa sakata la usajili wa Kago ambalo lilikuwa likikwamishwa na kutofuatwa kwa taratibu ya kumhamisha mchezaji huyo kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa kutumia njia iliyoamrishwa na FIFA ya kutumia mtandao ya TMS baada ya kuwa kibali cha uhamisho wa nyota huyo kutumwa kwa njia ya zamani ya fax.
Katika hatua nyingine, Mgogoro kati ya klabu ya Yanga na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusiana na jezi zenye nembo nyekundu ya mdhamini mkuu wa ligi ya Bara, kampuni ya simu ya Vodacom, umechukua sura mpya baada ya ‘Wanajangwani’ kuambiwa kuwa ni lazima wavae jezi hizo ili wasikumbane na hatua kali zaidi dhidi yao.
Yanga wameapa mara kadhaa kuwa kamwe hawatavaa jezi zenye nembo nyekundu ya Vodacom kwa sababu rangi hiyo inayotumiwa na wapinzani wao wa jadi, Simba, haitambuliwi na katiba yao na kwamba kuivaa ni sawa na kuisigina katiba hiyo wanayopaswa kuilinda kwa namna yoyote ile.
Juzi na jana, Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga na Katibu Mkuu Selestine Mwesigwa, walisema kuwa tayari wamezungumza na Vodacom na kampuni hiyo imetumia busara kwa kuheshimu mila na tamaduni za Yanga kabla ya kuwaruhusu kuvaa jezi zitakazokuwa na nembo ya rangi nyeusi badala ya rangi nyekundu.
Hata hivyo, TFF imepinga mabadiliko yoyote ya rangi ya nembo ya Voda na kusisitiza kuwa Yanga ni lazima wavae nembo nyekundu kama ilivyo kwa timu nyingine zinazoshiriki ligi ya Bara.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema jana kuwa TFF haiwezi kuyumbishwa na klabu hiyo kwani wakifuata matakwa yao, wanaweza kukaribisha usumbufu zaidi pindi klabu nyingine zikitaka pia kubadilishiwa rangi za nembo ya mdhamini.
Akieleza zaidi, Osiah alisema kuwa, kama Yanga itaendelea na hatua yake ya kutovaa jezi za nembo nyekundu, haitapewa nauli wala zawadi ikiwa itatwaa ubingwa na kwamba, zaidi ya hapo, watakuwa wakitozwa faini ya Sh. milioni moja katika kila mechi na vilevile, hatua zaidi zitachukuliwa dhidi yao.
"Tumeamua hivi kukwepa timu nyingine kufanya kama Yanga (kugomea jezi)… kwa kuwa kila timu ina rangi yake, hivyo Yanga inapaswa kutumia jezi hizo na wakiendelea kugomea TFF itawatoza faini katika kila mchezo watakaocheza wa ligi kuu Tanzania Bara,” alisema .
Wakati TFF ikitoa msimamo huo, Mwesigwa aliiambia NIPASHE jana jioni kuwa hawajapata taarifa rasmi juu ya vitisho hivyo vya TFF na kwamba wakijulishwa kiofisi, watajua ni kitu gani cha kufanya.
Tunasubiri taarifa yao rasmi… ila msimamo wetu bado ni huo wa kutovaa jezi yoyote yenye nembo nyekundu,” alisema Mwesigwa.
Yanga ilizigombea kitambo jezi zenye nembo nyekundu na hata wakati wa hafla ya kukabidhiwa kwa jezi hizo, hawakujitokeza kuzichukua kwa madai kwamba hawako tayari kukiuka katiba yao.
Katika mechi zao mbili za ufunguzi wa ligi hiyo, Yanga walitumia jezi za mdhamini wa klabu yao, bia ya Kilimanjaro inayozalishwa na kampuni ya bia (TBL).
CHANZO: NIPASHE

No comments: