Wednesday, August 31, 2011

Rostam, Mkapa kuungana kampeni za CCM Igunga

ALIYEKUWA Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz ni miongoni mwa makada watakaotumiwa na CCM katika kampeni za kumsaka mrithi wake katika jimbo hilo.Habari zilizopatikana jana kutoka ndani ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM (CC) kilichokutana juzi, Ikulu Dar es Salaam zinasema Rostam amepangwa kuhudhuria uzinduzi wa kampeni za CCM zitakaofanywa na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, Septemba 10, mwaka huu."Labda ratiba ibadilike, lakini ni kweli Rostam amepangwa kwamba ataambatana na Mzee Mkapa kwenda Igunga na yeye atabaki huko kama wiki moja hivi kusaidia kampeni hizo," alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu hiyo ya CCM.


Mjumbe huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe alisema Rostam amepangiwa kwenda Igunga mara tatu: "Baada ya hapo atarudi tena katikati ya kampeni na pia atarudi tena wakati wa hitimisho."

Uamuzi wa CCM kumtumia Rostam katika kampeni zake za Igunga unatafsiriwa kuwa hatua ya kutafuta kuungwa mkono na wakazi wa jimbo hilo ambao "walikasirishwa" na kitendo cha mbunge wao huyo kujiuzulu kwa kile alichokiita "siasa chafu."

CCM kinakabiliwa na makovu huko Igunga yaliyotokana na kujiuzulu kwa Rostam ambaye wakati akitangaza kujiuzulu alitamka bayana kwamba uamuzi wake huo ulitokana pamoja na mambo mengine, wanasiasa uchwara wanaoendesha siasa za kupakana matope baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete kutangaza mpango wa kujivua gamba.

“Nimepata msukumo wa kuamua kuachia nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama, nikianzia na ile ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa nikiuwakilisha Mkoa wa Tabora na hii ya ubunge wa Igunga ambazo kama si kwa baraka za chama changu, nisingelikuwa nazo," alisema Rostam siku alipotangaza kujiuzulu na kuongeza:

“Napenda kuliweka hili sawasawa. Uamuzi wangu wa kuachia nafasi zangu zote za uongozi nilizopata kwa tiketi ya CCM, haukutokana na wala haumaanishi kukubaliana na shinikizo lililopotoshwa kuhusu azma ya utekelezaji wa dhana ya kujivua gamba, la hasha, bali dhamira ya dhati ya kuachana na siasa hizi uchwara na kutumia muda wangu kushughulika na biashara zangu."

Rostam sasa anatarajiwa kushiriki kampeni hizo, akimpigia debe mgombea wa CCM, Dk Dalaly Peter Kafumu aliyepitishwa na CC ya chama hicho juzi.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa kuhusu ushiriki wa Rostamu katika kampeni za Igunga alisema: “Rostam ni mwanachama wa CCM na chama kimetoa mwaliko kwa wanachama wake kushiriki kampeni hizi, hivyo hilo labda ajibu mwenyewe lakini kama mwanachama ana haki ya kushiriki.”

“Labda niseme hivi, ukiachilia mbali watu kama Mzee Mkapa ambaye atakuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi, hatukupeleka mwaliko kwa mtu mmoja mmoja, ila tuliwaalika wanachama wetu kusaidia kampeni hizi, kwa hiyo Rostam akiwa mwana CCM ana haki ya kukipigia kampeni chama chake.”

Nape pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Tanzania Bara), John Chiligati walitajwa na Rostam wakati akijiuzulu kwamba ndiyo waliopotosha dhana ya kujivua gamba kinyume cha uamuzi wa NEC.

 “Walisikika wakitangaza kwamba Halmashauri Kuu ya Taifa ilikuwa imefikia uamuzi wa kuwapa siku 90 wale walioitwa watuhumiwa wa ufisadi ndani ya chama kujitoa katika nafasi zao za uongozi vinginevyo watafukuzwa na chama," alisema Rostam.

Hata hivyo, Rostam hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo kwani alipopigiwa simu yake ya kiganjani hakupokea na alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi alijibu kwa kifupi: “in a meeting, baadaye” akimaanisha kwamba alikuwa kwenye mkutano.

Juzi, Nape akitangaza uteuzi wa Dk Kafumua alisema: “Katika kufanikisha kampeni za CCM wanachama waliowania kuteuliwa katika nafasi hiyo wameahidi kuwa watashiriki kikamilifu katika kampeni hizo.”
Alisema hata wagombea wengine wa chama hicho katika kura za maoni wameahidi kuwa watamuunga mkono Dk Kafumu ambaye aliibuka mshindi kwa kupata kura 588. Hao ni pamoja na aliyemfuatia kwa karibu, Jafari Omari aliyepata 193 na Shams Brahamu aliyepata kura 38. Katika uchauguzi huo wanachama 13 wa CCM waliomba nafasi hiyo.

Nape alisema CCM kitashinda kwa kuwa kina mizizi imara iliyojikita katika vitongoji vyote vya jimbo hilo, tofauti na vyama vya upinzani... “CCM ipo Igunga wakati wote (wa uchaguzi na usio wa uchaguzi). Vyama vya upinzani huonekana kule wakati wa uchaguzi.”


CCM waunda timu nne
Katika kuhakikisha kinashinda uchaguzi huo mdogo, CCM Wilaya ya Igunga kimeunda timu nne maalumu, ikiwamo ya wafanyabiashara maarufu watakaohakikisha kwamba mgombea wa chama hicho, Dk Kafumu anashinda.

Hatua ya kuunda timu hizo inatokana na chama hicho ngazi ya taifa kutangaza kuwa majukumu yote ya kupanga na kuendesha kampeni zake kwa ajili ya uchaguzi huo mdogo utakaofanyika Oktoba 2, mwaka huu, zitasimamiwa na CCM Wilaya ya Igunga.

Katibu wa CCM Wilaya ya Igunga, Neema Adam alisema jana kuwa tayari wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya vyama vitano vya upinzani vilivyosimamisha wagombea.

"Kimsingi uchaguzi unasimamiwa na Kamati ya Siasa ya Wilaya. Hivyo wajumbe wote wa kamati hiyo wataratibu shughuli zote za kampeni," alisema Neema lakini akidokeza kuwa kamati hiyo itasaidiana na timu nyingine tatu.

"Mbali na kamati hiyo, wafanyabiashara maarufu 20 hapa Igunga, wameunda timu itakayosaidiana na wanachama wa CCM kufanikisha kampeni hizo. Vilevile kila tarafa ina timu ya watu wanne na kila kata watu 10. Kwa hivyo ukiangalia utaona kuwa tumejipanga vizuri katika kuhakikisha tunapata ushindi."

Wagombe wengine ni Joseph Kashindye wa Chadema,  Moses Edward (TLP) na John Maguma wa SAU na Leonard Mahona wa CUF. Uchukuaji fomu ulimeanza Agosti 24 na unatarajiwa kukamilika Septemba 6, mwaka huu.

CUF nayo yatamba
Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Julius Mtatiro alisema wamejipanga kikamilifu kukabiliana na CCM kwenye kampeni zijazo.Alisema wakati wa kampeni chama chake kitalipua siri zilizofichuka dhidi ya kiongozi yeyote wa CCM atakayefika Igunga, akiwamo Rais Mstaafu, Mkapa.

Katika kampeni hizo, Mtatiro alisema wataweka hadharani sababu ambazo wapiga kura wanapaswa kuzizingatia na kutoichagua CCM na badala yake kumchagua mgombea wa CUF.

Alisisitiza kuwa CCM wajiandae kukabiliana na maswali mengi ambayo watashindwa kuyajibu mbele ya wakazi wa Igunga.

Mwananchi

No comments: