ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 30, 2011

Stars yanoga Dar es Salaam


Image

WACHEZAJI wanaounda timu ya taifa ‘Taifa Stars’, wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi wamewasili kambini kwa ajili ya mchezo wa kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika dhidi ya Algeria utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Jumamosi ijayo.

Wachezaji waliowasili ni pamoja na Danny Mrwanda na Abdi Kassim wanaocheza soka la kulipwa nchini Vietnam katika klabu ya DT Long An, Mbwana Samatta anayekipiga TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kiungo Henry Joseph wa Konsivinger ya Norway, Athumani Machupa wa Vasuland IF ya Sweden na beki Idrissa Rajabu wa Sofapaka ya Kenya. 



Akizungumza jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Boniface Wambura alisema Kassim, Mrwanda na Samatta waliwasili juzi, wakati Joseph, Rajabu na Machupa waliwasili jana.

Wambura alisema kiungo wa kimataifa wa Tanzania anayecheza soka la kulipwa Canada katika klabu ya Vancouver Whitecaps, Nizar Khalfan anatarajiwa kuwasili leo usiku tayari kujiunga na kambi ya timu hiyo.

Pia alisema kiungo Nurdin Bakari amerejea katika hali ya kawaida na tayari ameanza mazoezi na wenzake kama kawaida.

Akizungumzia hali ya mchezaji huyo, daktari wa timu ya taifa, Mwanandi Mwankemwa alisema hali yake ni nzuri na anafanya mazoezi na wenzake kama kawaida.

Alisema kulikuwa na hofu ya kumtumia mchezaji huyo lakini walihakikishwa na madaktari wa Yanga na baadaye kumfanyia uchunguzi na kujiridhisha kuwa amepona maumivu ya kifundo cha mguu.

Wakati huohuo, TFF jana ilitangaza viingilio kwa ajili ya mchezo huo, ambapo cha juu kitakuwa Sh 30,000 na cha chini Sh 3,000.



Habari Leo

No comments: