Tuesday, August 30, 2011

Aua mwanawe aolewe-HABARI LEO

POLISI wilayani Bariadi mkoani hapa inamshikilia mwanamke mkazi wa kijiji cha Mwamabu wilayani humo kwa tuhuma za kumnyonga mtoto wake wa kumzaa ili aolewe.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Diwani Athumani, alisema ofisini kwake jana kuwa, Tabu Maimatha mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu ameuawa kikatili kwa kunyongwa na mama yake mzazi, akishirikiana na mpenzi wake, Kijiji Nyamagu ambaye alitoroka baada ya mauaji hayo.

Alimtaja mwanamke huyo kuwa ni Limi Limbu (22) mkazi wa kijiji cha Mwamabu kata ya
Bumera na kwamba tukio hilo lilitokea juzi saa saba za mchana kijijini hapo baada ya Limi kurubuniwa na mpenzi wake Nyamagu, kuwa wakimuua mtoto wake wataoana.

Baada ya kukamatwa, Limi alikiri mbele ya polisi kuwa alishirikiana na mpenzi wake huyo
kumwua mtoto wake, ili waishi kwa amani na waoane na kuanza maisha mapya katika ndoa yao.

Inadaiwa Limi baada ya kukubaliana na mpenzi wake huyo walifanya kitendo hicho cha kikatili ili kuondokana na bughudha ya mtoto huyo wa nje ya ndoa na hivyo wazae watoto wao wa ndani ya ndoa.

Kamanda Athumani alisema, katika tukio lingine lililotokea katika barabara ya Old Shinyanga saa 10 usiku wa kuamkia jana, mtu mmoja alikufa na wengine watatu kujeruhiwa vibaya baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugonga mti.

Alimtaja aliyekufa kuwa ni Jean Samson (44) mkazi wa Ngokolo mitumbani na majeruhi ni dereva wa gari hilo Emmanuel Kaleja (57), Mora Sendo ‘Choto’ (58) na Njile Chenya (43) wakazi wa Majengo mapya na Ngokolo katika manispaa ya Shinyanga.

Alilitaja gari lililopata ajali kuwa ni Suzuki Escudo namba T 605 DHW na kuongeza kuwa majeruhi watatu wa ajali hiyo wamelazwa katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga.

No comments: