
Mshambuliaji wa Simba, Felix Sunzu akijaribu kumtoka beki wa timu ya Victors ya Uganda, Katwere Msaac kwenye mechi ya Simba Day kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha jana. Simba ilifungwa 1-0. Picha na Silvan Kiwale
SIMBA..Simba! Aaah! Ndiyo kilichotokea wakati mashabiki wa Simba wakishangilia pasi za timu yao ilipocheza dhidi ya Victors ya Uganda iliyozima kelele hizo ghafla.
Kikosi kikicheza kwa mara ya kwanza kikiwa kamili baada ya usajili kukamilika ndani ya Ardhi ya Tanzania Bara, Simba ilionyesha mabadiliko lakini ikalala kwa bao 1-0 mbele ya Victors ya Uganda.
Kitendo cha beki mpya wa Simba, Victor Costa kumkwatua Abdallah Mohamed dakika ya 57 kilisababisha penalti ambayo Sebuguzi Eric alimfunga Juma Kaseja kilaini dakika ya 59.
Kocha Moses Basena alilaumu washambuliaji wake kwa kuwataja kwa majina Uhuru Seleman, Emmanuel Okwi na Felix Sunzu kwa kukosa nafasi za wazi ambazo zingeweza kuwapa raha zaidi mashabiki katika mchezo huo ambao beki wa zamani wa Simba, Joseph Owino alikuwa jukwaani akishuhudia.
“Kwa nafasi kama alizopata Uhuru, Sunzu yalikuwa ni magoli ya wazi walihitaji utulivu, lakini timu imeonyesha mabadiliko ingawa tumepoteza tunahitaji kubadilika na kujipanga zaidi kwa kuongeza umakini,”alisema Basena.
“Ukiangalia na ulinzi bado hakuna uelewano mzuri kati ya Mungusa na Costa, lakini ni sehemu ambazo tunahitaji kuzifanyia kazi na watu waelewe kwamba kuna wachezaji wako nje kwa Taifa Stars na wengine majeruhi, wasikate tamaa,”alisisitiza.
Mechi hiyo ya Simba Day ilikuwa ni ya kwanza kikosi cha Simba kuonekana Bara baada ya kutangaza usajili ambapo, katika kambi yake ya Zanzibar ilicheza mechi mbili dhidi ya Polisi na Karume Boys na kushinda zote.
Simba ilionyesha kiwango kikubwa na soka la Burudani kwa kushambulia vizuri na kufanya mambo ya aina yake ingawa bado mastraika wake wanne walishindwa kufumania nyavu dakika 45 za kwanza.
Katika kikosi cha jana ambacho mbele kulikuwa na Mzambia Felix Sunzu, Mganda Emanuel Okwi, Gervais Kago wa Afrika ya Kati na Haruna Moshi walitengeneza nafasi zaidi ya tano, lakini umaliziaji ulikuwa tatizo ingawa mabeki wa Victors walikuwa na kazi kubwa.
Kago ambaye katika mechi mbili zilizopita alipachika mabao, alikosa nafasi nyingi za wazi jana alizotengewa na Sunzu na dakika na kufanya Moses Basena kumtoa kipindi cha pili na kumuingiza Uhuru Suleiman ambaye alionyesha kwamba amepona majeraha.
Victors walikuwa na ukuta mzito chini ya kipa Kimera Ally ambapo wachezaji wengi wa timu hiyo walicheza pasi fupi kwa kasi huku winga zote zikionyesha uhai jambo ambalo lilisababisha wakati mgumu kwa mabeki Costa na Obadia Mungusa.
Hatahivyo Mungusa alitolewa kipindi cha pili akaingia Kelvin Yondani. Sunzu ambaye alipachika bao dakika ya 44 kwa shuti mwamuzi Judith Gamba wa Dar es Salaam alilikataa kwa maelezo kuwa aliotea.
Hiyo ni mechi ya tatu kwa Sunzu kuichezea Simba bila kufunga bao ingawa zote ni za kirafiki dhidi ya Police, Karume na Victors lakini amewaambia mashabiki wasiwe na wasiwasi yuko fiti na anahitaji muda jambo ambalo hata kocha Basena aliliunga mkono.
Basena alisema wachezaji hao wamecheza vizuri huku akisisitiza kuwa yalikuwa ni majaribio mazuri kwake wala hana wasiwasi.
Simba inajiandaa na mechi dhidi ya Yanga Agosti 17 kwenye ngao ya hisani pamoja na ile ya ufunguzi wa Ligi Kuu baina ya JKT Oljoro mjini hapa Agosti 21.
Simba: Juma Kaseja,Salum Kanoni, Nasoro Cholo, Obadia Mungusa/Kelvin Yondani, Victor Costa, Patrick Mafisango/Abdala Sesema, Gervas Kago/Uhuru Seleman, Shomari Kapombe,Felix Sunzu/Rashid Ismail,Haruna Moshi, Emanuel Okwi.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment