ANGALIA LIVE NEWS
Monday, August 8, 2011
Ufisadi wa Meremeta hauna kinga, uchunguzwe
KWA miaka kadhaa sasa wabunge wa Bunge la Bunge la Jamhuri ya Muungano wamekuwa wakipaza sauti zao juu kuhusiana na ufisadi wa zaidi ya Sh205.9 bilioni unaodaiwa kufanywa kupitia Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Meremeta iliyokuwa ikimilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Kilio hichi cha wabunge wenye uzalendo wa dhati katika kusimamia rasilimali za Taifa hili, bila kuchoka walisimama kidete kutaka ufisadi wa aina yake uchunguzwe, lakini baadhi ya viongozi wa Serikali, akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda waliamua kwa dhati kabisa kuziba masikio na kufumba macho yao kwa kutoa visingizio luluki vyenye lengo la kuficha ukweli.
Pamoja na vizingiti vyote hivi, wabunge walivyokumbana navyo, bado waliendelea kusimama kwenye uzalendo na kuendelea kuibana Serikali kwa lengo la kutaka tuhuma hizi za ufisadi wa Meremeta zichunguzwe na ukweli ujulikane kwa maslahi ya taifa.
Ndio maana taarifa za kwamba Bunge kupitia Kamati yake ya Nishati na Madini litachunguza ufisadi huo zinapoza kilo cha wengi kuwa taasisi hili muhimu kwa mustakabli wan chi imesikia kilio cha wabunge wake na Watanzania kwa ujumla.Ndio maana tunaamini kwamba uchunguzi huu utaisaidia kubaini wahusika wa ufisadi huu ili sheria ichukue mkondo wake.
Tunaambiwa kwamba Kamati ndogo ya Madini itafanya uchunguzi wa uhalali wa malipo ya dola milioni 132 (sawa na Sh205.9 bilioni kwa viwango cha sasa vya kubadilishia fedha ambavyo ni Tsh1560 dhidi ya dola) ambazo zilitoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwenda Ned Bank ya Afrika Kusini, kama malipo ya mkopo wa dola milioni 10, uliokuwa umechukuliwa na kampuni ya Meremeta Ltd.
Kwa hiyo, uchunguzi huu ni mwanzo mzuri wa kupima hoja za viongozi wa Serikali ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakidai kwamba suala la Meremeta lisingeweza kufanyiwa uchunguzi kutokana na “sababu za kiusalama”.
Ndio maana sisi tunasema kwamba uchunguzi wa kina wa sakata la Meremeta ni muhimu kwa kuwa hakuna usalama ambao unalea ufisadi mahali popote duniani.Tunaamini kwamba wanasiasa ambao walikuwa wakitumia mwavuli wa usalama au vyombo vyetu vya ulinzi kuficha uovu watatoa ushirikiano kwa Kamati ya Bunge.
Hata hivyo, wajumbe wa Kamati hiyo ndogo tunawaasa kwamba endapo watakutana na vizingiti kama vya huko nyuma basi wasisite kupaza sauti zao juu kuubarisha umma wa Watanzania ambao ndio wadau wakuu wa rasilimali za nchi.
Hatupendi kuamini na wala kushawishika kwamba Jeshi letu ambao lina kazi muhimu ya kulinda mipaka ya nchi yetu na watu wake limejiingiza kwenye biashara ya madini. Ndio maana tunasema kwamwe hatupendi JWTZ ipakwe matope kwa ufisadi wa watu wa chache ambao hawalitakii mema Taifa hili.
Kama walivyo Watanzania wote, tunatambua kazi nzuri ambayo Jeshi letu limefanya ndani na nje ya mipaka yetu, hivyo tusingependa baadhi ya viongozi wa Serikali walitumie kama kichaka cha kuficha uozo wa wachache.
Ni kweli tunambua unyeti wa kazi za jeshi letu, lakini kwa hili la ufisadi wa Meremeta, JWTZ wasibebeshwe mzigo; hivyo tunataka wenye mzigo wajulikane na wafikishwe kwenye vyombo vya dola.
Kila wakati msimamo wa gazeti ni kwamba ufisadi wowote wa fedha za umma hauwezi kuvumilika kwa visingizio vya namna yoyote ile, ndio maana tuaamini kwamba uchunguzi utasaidia kuwekla wazi kila kitu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment