ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 20, 2011

Tanesco yalipa mabilioni kesi ya Dowans



REX ATTONEY YAHUSISHWA NA MALIPO YA SH7 BIL. YA UENDESHAJI KESI, DHAMANA YA SH8 BIL. NAYO YALIPWA LONDON
Neville Meena, Dodoma
WAKATI nchi ikiwa gizani kutokana na makali ya mgawo wa umeme, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limelipa mabilioni ya shilingi yanayotokana na kesi baina yake na Kampuni ya Dowans Holdings ya Costa Rica na mshirika wake, Dowans Tanzania Ltd.Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa hadi kufikia Machi mwaka huu, Tanesco ilikuwa imelipa Sh7.05 bilioni kwa Kampuni ya Uwakili wa Rex Attorneys kwa ajili ya kugharamia shughuli mbalimbali katika kesi dhidi yake na Dowans kwa upande mmoja na Kampuni ya Richmond kwa upande mwingine.

Malipo hayo kwa Kampuni ya Rex Attorneys yaliyofanywa kati ya Oktoba 6, 2008 na Machi 23, 2011 ni kwa ajili ya kesi namba 15910/VRO ambayo ni baina ya Tanesco na Richmond pamoja na kesi namba 15945/VRO ambayo ni baina ya Tanesco dhidi ya Dowans.


Moja ya taarifa rasmi za Tanesco ambayo Mwananchi limeiona, inathibitisha kwamba shirika hilo limekuwa likilipa fedha hizo kwa Rex Arttoneys katika vipindi tofauti kutokana na huduma ambazo hutolewa na kampuni hiyo ya uwakili.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, William Mhando, inabainisha baadhi ya huduma ambazo Tanesco imezilipia na gharama zake kwenye mabano.

Kupitiwa kwa Mkataba wa Tanesco na Richmond (Sh29 milioni), gharama za uwakilishi kwenye mahakama (Sh67.8 milioni) na gharama za uwakili (Sh4.13 bilioni).

Hata hivyo, Meneja Uhusiano wa Tanesco, Badra Masoud alipoulizwa kuhusu malipo hayo, hakukanusha wala kuthibitisha, huku akitaka apewe muda hadi jana saa nane mchana kwa ahadi kwamba angetoa majibu wakati huo.

Ulipofika wakati huo Badra alisema: “Nimefuatilia lakini tumeshauriana hapa kwamba muandike barua mkiuliza maswali yenu, halafu tutawajibu kwa maandishi.”

Mmoja wa mawakili katika Kampuni ya Rex Attoneys, Dk Thomas Nguluma alisema jana kuwa, kampuni yao haikunufaika na kiasi chote cha Sh7 bilioni na kwamba fedha nyingine zilikuwa zikipitia mikononi mwao kwa ajili ya kulipia gharama nyingine za kuwezesha uendeshaji wa jumla wa kesi hiyo.

"Sidhani kama hizo fedha zote zimelipwa kwetu. Japokuwa sina takwimu kwa sasa, lakini mnatakiwa kufanya uchambuzi ili kufahamu ni kiasi gani cha fedha ambacho kimetumika na fedha hiyo imetumika kwa ajili gani," alisema Dk Nguluma na kuongeza:

"Kesi hii ilikuwa ni kubwa sana na si kesi ndogo kama wengi wetu tunavyodhani. Ni kesi ambayo ilituchukua zaidi ya mwaka mmoja na wakati huo ilibidi tusitishe kazi zetu zote. Hatukuweza kufanya kazi nyingine, ilikuwa ni hiyo Dowans tu."

Alitoa mfano wa Sh111.4 milioni ambazo zilitumika kukodi ukumbi kwa ajili ya kuendeshea usuluhishi huo wa kimahakama, kwamba fedha zote hizo zililipwa katika Hoteli ya Kilimanjaro Kempinsk ambako kikao hicho kilifanyika kwa siku nane mfululizo.

“Hizo ni gharama za ukumbi, hapo kampuni yetu haikugusa hata senti tano, hapo ni kila kitu pamoja na vifaa vyote vya kurekodia mwenendo wa kesi, inawezekana pia majaji wale waliokuja kutoka huko ICC, kwa ufupi kuna mambo mengi sana,” alisema Nguluma.

Alipotakiwa kueleza kuhusu Sh67.8 milioni ambazo zimeandikwa kuwa ni ada ya uwakilishi wa Tanesco/Dowans, alisema kuwa fedha hizo ni gharama za mawakili wa nyongeza kutoka Uingereza ambao walikuwa wakiongoza jopo la watetezi wa Tanesco.

"Tukichukua mawakili kutoka Matrix Balisters nchini Uingereza ambao walitupa mawakili wawili, hawa ndiyo waliokuwa wakiongoza jopo letu katika kesi hii. Sasa hizo zote ni gharama hivyo hiyo (ada ya uwakilishi) ndiyo kazi yake hiyo," alisema Dk Nguluma.

Utata Rex Attorneys
Hoja zimekuwa zikitolewa kuhusu sababu za Tanesco kuendelea kufanya kazi na kampuni hiyo ya uwakili hali kukiwa na taarifa kwamba imeshindwa kufanya vizuri katika kesi dhidi ya Dowans.

Kadhalika, kumekuwa na hoja kwamba Rex Attorneys ndiyo iliyoishauri Tanesco kulipa tuzo hiyo badala ya kwenda mahakamani na kwamba kama hivyo ndivyo, kampuni hiyo haifai kuendelea kufanya kazi na Tanesco katika mchakato wa kukata rufaa.

Hata hivyo, Dk Nguluma alikanusha taarifa hizo akisema Rex Attorneys ndiyo iliyowezesha tuzo iliyotolewa kwa Dowans kupungua kutoka madai ya awali ya Dola za Marekani 149 milioni hadi kufikia Dola 65 milioni.

Kuhusu kukata rufaa, alisema taarifa yake kwenda Tanesco baada ya hukumu ya ICC ilikuwa na ushauri wa kitaalamu unaoonyesha pande mbili ambazo Serikali ilikuwa na uwezo wa kutumia mojawapo.

Alisema baada ya Tanesco kuamriwa kulipwa fedha hizo, Rex Attorneys iliandika waraka wa kisheria unaoishauri ukieleza wazi hasara na faida za kulipa fedha hizo au kinyume chake. Hivyo Serikali kupitia shirika hilo kuamua kupinga tuzo hiyo mahakamani.

“Sisi tuliweka wazi faida na hasara za pande zote, kwamba kama wanaamua kulipa basi watakuwa wametekeleza hukumu ya mahakama na kuachana na suala hilo lakini pia tuliwaeleza udhaifu wa hukumu ambao wangeutumia kukata rufaa,” alisema.

Malipo ya Sh8 bilioni
Taarifa za malipo hayo zimekuja wakati Tanesco imeshalipa Sh8 bilioni katika Mahakama Kuu, Uingereza ikiwa ni dhamana ya kutaka kuchelewesha ukazaji wa hukumu dhidi yake baada ya maombi yaliyowasilishwa katika mahakama hiyo na Kampuni ya Dowans.

Uamuzi wa kutaka kulipwa kwa fedha hizo ulitolewa na Jaji Burton wa mahakama hiyo baada ya Tanesco kupitia kwa mawakili wa kampuni ya Matrix kutaka uamuzi dhidi ya ombi la Dowans la kupewa tuzo uahirishwe hadi kesi iliyopo Mahakama Kuu ya Tanzania itakapotolewa uamuzi.

Rex Arttoneys pia inadaiwa kwamba ndiyo iliyokuwa mtetezi wa Tanesco katika kesi hiyo ambayo Dowans ilitaka Mahakama Kuu ya Uingereza kukazia hukumu ili ilipwe tuzo iliyopewa na ICC ya Dola za Marekani milioni 65 sawa na wastani wa Sh104 bilioni kwa viwango vya sasa vya kubadilisha fedha.

Hata hivyo, Dk Nguluma alikanusha kwamba Rex Attorneys inahusika na utetezi katika shauri hilo ambalo limeahirishwa hadi Novemba 22, mwaka huu kusubiri uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, lakini akakiri kwamba wao hushirikiana na mawakili wa Matrix katika kazi zao.

“Sisi hapa ni mawakala tu na hatulipwi hata senti tano labda kama zitakuwa ni gharama za upatikanaji wa nyaraka za kusaidia hao mawakili wa Kampuni ya Matrix ambao wametafutwa na Tanesco,” alisema Dk Nguluma na kuongeza:

“Ila kwa sababu sisi ndiyo tunafanya kazi ya huo uwakala, nina taarifa kwamba Tanesco wamelipa hiyo dola milioni tano kwa ajili ya kuwezesha shauri lililofunguliwa na Dowans kuahirishwa hadi Novemba 22, mwaka huu.”

Habari zilizopatikana zinadai kwamba mawakili wa Matrix pia walidai kulipwa fedha za utangulizi kutoka Tanesco kiasi cha Paundi 500,000 za Uingereza zaidi ya Sh1 bilioni na kwamba fedha hizo zilikuwa katika mchakato wa kulipwa.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taratibu za kisheria iwapo Tanesco watafanikiwa kuzuia malipo ya Dowans pale Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi wake, basi fedha zilizowekwa kama dhamana nchini Uingereza zitarejeshwa.

Dk Nguluma alisema ikiwa Tanesco itashindwa basi fedha hizo zitakuwa mali ya Dowans na kwamba Tanesco italazimika kulipa fedha nyingine zilizobaki, gharama za kesi husika na riba ya fedha zinazopaswa kulipwa Dowans.

Hali ya Umeme
Jana, Serikali iliwasilisha bungeni taarifa kuhusu hali upungufu wa umeme ikisema kuwa tatizo kubwa ni kuharibika kwa mfumo wa kusafirisha gesi kutoka Songosongo na uhaba wa mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL.

Juzi, Spika wa Bunge, Anne Makinda aliitaka Serikali kutoa maelezo bungeni kuhusu sababu za hali hiyo nchini kutokana na hoja iliyotolewa na Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekia Wenje.

Wenje alitaka bunge kuahirisha mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, ili kujadili dharura ambayo alisema ni maeneo mengi nchini kutokuwa na umeme.

Sambamba na tatizo hilo, Serikali hivi sasa inasaka Sh408 bilioni kwa ajili ya kutekeleza mpango wa dharura wa kuondokana na giza ambao uliowasilishwa bungeni Agosti 13, mwaka huu na kupigiwa vigelegele na wabunge wengi.

Mwananchi

No comments: