ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 20, 2011

Wagombea wa CCM, Chadema watakaoumana Igunga hadharani


Neville Meena, Dodoma na John Dotto, Igunga
WAGOMBEA wanaotarajiwa kupeperusha bendera za CCM na Chadema katika kinyang'anyiro cha kumtafuta mbunge wa Jimbo la Igunga, wamefahamika.Wenye nafasi kubwa ya kutangazwa kugombea ni Dk Peter Kafumu wa CCM na Joseph Mwandu wa Chadema ambao wote waliongoza kwenye kura za maoni dhidi ya waombaji wengine.

Wagombea hao walifahamika baada ya kuibuka washindi kwa kura nyingi zaidi katika uchaguzi wa kura za maoni ulizoendeshwa na vyama vyote viwili, jimboni Igunga.Hata hivyo, vikao vya juu vya vyama hivyo ndivyo vitakavyokuwa na uamuzi wa mwisho wa kuwatangaza au kuwapa wengine ambao walishiriki kwenye kura hizo za maoni lakini wakashindwa.


Ushindi wa watu huo ulipatikana huku uchaguzi wa CCM ukidaiwa kuwa uliambatana na vitendo vya rushwa na taarifa zinasema kwamba watu watatu wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa uchunguzi.

Watu hao wanadaiwa kukutwa nyuma ya ukumbi wakigawana fedha zilizodaiwa kutolewa na mmoja wa wagombea.Hata hivyo, Kamanda wa Takukuru Wilaya ya Igunga, John Ngunangwa hakuwa tayari kukubali wala kukataa juu kuwapo kwa watuhumiwa waliokamatwa akisema angetoa ufafanuzi baadaye.

Vyama viwili tayari vimewatangaza wagombea wao kwenye kinyang'anyiro hicho ambao ni Moses Edward kwa tiketi ya TLP na Leopard Mahona wa CUF.

Kura za maoni za CCM
Katibu wa CCM Wilaya ya Igunga, Neema Adam alimtangaza Dk Peter Kafumu kuwa mshindi kwa kura 588, akifuatiwa na Jafari Omari aliyepata 193 na Shams Brahamu aliyepata kura 38 na kushika nafasi ya tatu.

Neema alisema wajumbe 950, walipiga kura kwenye Mkutano huo Mkuu wa CCM wa Wilaya kuwachuja watu 13, ambao walichukua fomu kuomba nafasi hiyo.Alisema kazi iliyobaki sasa ni kamati za chama hicho ngazi za juu kufanya uteuzi wa mgombea wao ambaye atakiwakilisha kwenye uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2, mwaka huu.

Awali, Mweka Hazina wa CCM Taifa, Mwigulu Mchemba ambaye pia ndiye mratibu wa kampeni wa CCCM Igunga, akiwahutubia wajumbe wa mkutano huo mkuu aliwataka kuchagua mgombea ambaye wanaamini atawaletea maendeleo.

Mchuano wa Chadema
Kwa upande wa Chadema, walioshika nafasi tatu za juu walitangazwa kuwa ni Mwalimu Joseph Mwandu aliyeongoza kwa kupata kura 63, Sabela Makelemo kura 53 na Juma Chacha aliyepata 43.

Mratibu wa Uchaguzi Jimbo la Igunga, Mwikabe Mwita Waitara alisema mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe 309 waliopigia kura majina 16 ya walioomba kugombea.

Mwikabe alisema Kamati Kuu ya Chadema ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe inakutana leo Mjini Igunga kupitia majina hayo matatu na hatimaye mgombea wa chama hicho atatangazwa.

Siku chache baada ya Chadema kuwatangazia wanachama wake wajitokeze kuchukua fomu, aliyewahi kuwa Mbunge wa Kisesa Erasto Tumbo alijitokeza.

Hata hivyo, jina lake jana halikuwamo katika orodha ya wagombea kwa kile kilichoelezwa kuwa ametakiwa kujitoa ili kuondoa dhana ya mgombea kuletwa kutoka makao makuu.

"Unajua Tumbo ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chadema Taifa. Angegombea na kushinda ingeleta picha mbaya. Tulimwambia atumie busara aachane na hii kitu na alitusikia," alisema Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Igunga, Hamis Majimoto.

Habari zilizopatikana jana zinasema kwamba Mbowe na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa jana walikuwa njiani kuelekea Igunga ana leo wataongoza kikao cha Kamati Kuu kuchambua na kutangaza mgombea wao.

Kikao hicho kilielezwa kuwa kitatanguliwa na vikao vingine vitatu vya ngazi ya wilaya, vyote vikilenga kumpata mgombea kati ya wagombea wote 16 waliojitokeza kuchukua fomu na kuzirejesha ili kupata ridhaa ya kubeba dhamana ya Chadema jimboni humo.

Mbowe alisema jana Mjini Dodoma kuwa: "Tumeamua kwamba Kamati Kuu yetu ikitane eneo la tukio yaani Igunga na hii itatupa fursa nzuri kwa viongozi wetu wa kitaifa kuifahamu Igunga na pengine kuwapa fursa wananchi wa eneo hili kuwafahamu viongozi wetu."
Mbowe alisema wajumbe wote wa Kamati Kuu walitarajiwa kuwa wamewasili Igunga jana jioni na kwamba kikao hicho pia kitapitia mpango mzima wa ushiriki wa Chadema katika kinyang’anyiro hicho.

Habari zaidi zinasema kuwa Chadema kimepanga wabunge wake wote kuongoza usimamizi katika kata zote 26 za Igunga ili kuhakikisha kinatwaa ushindi katika jimbo hilo ambalo ni ngome ya CCM kwa miaka mingi.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza kufanyika kwa uchaguzi katika jimbo hilo baada ya aliyekuwa Mbunge, Rostam Aziz kujiuzulu katika mpango wa CCM wa kujivua gamba.

Chadema walianza harakati za kuwawezesha kuchukua jimbo kwa kutuma timu ya makada wake ambao kwa mujibu wa taarifa zilizopo waliratibu chaguzi za viongozi wa vijiji na kata ikiwa ni hatua ya kujenga mtandao wake katika jimbo hilo.
Uchaguzi mdogo wa Igunga utakuwa wa kwanza kufanyika tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwaka jana ambao CCM kilipata wabunge wengi na kuongoza katika uchaguzi huo.

Mwananchi

No comments: