Na Luqman Maloto
Bado una mabaki ya Sikukuu ya Eid el Fitry? Kama ndiyo, basi yaondoe ili tuchape kazi. Shukurani za kipekee ziende kwa Mola aliyeumba kila kitu na kutufanya mimi na wewe tuishi juu ya mgongo wa ardhi. Anastahili sifa zote zenye utukufu.
Nakukaribisha msomaji kwa uadilifu mkubwa. Mada yetu tulianza nayo wiki iliyopita. Nakuomba aya zake zikupe muongozo wa kutambua namna ya kuepuka mawazo mabaya kwa mwenzi wako.
Watu wenye mawazo mabaya juu ya wapenzi wao mara nyingi wanakuwa na misukumo ya kufanya uamuzi ambao siyo sahihi. Yupo anayeweza kukatisha shughuli zake za siku kwa ajili ya kumfuatilia mwenzake.
Mwingine anahaha kuulizia nyendo za mwenzi wake kwa marafiki. Hilo ni kosa kubwa kwa sababu huyo unayemuuliza, mwisho anaondoka na kitu kikubwa kwamba hakuna uaminifu kwenye uhusiano wako.
Kuna mtu ambaye huweka mabodigadi wa kufuatilia nyendo za mke wake kila anapokwenda. Anayedhani kufanya hivyo ni dawa, ameula wa chuya kwa uvivu wa kuchagua. Anakosea kupita kiasi.
Kumuwekea mwenzi wako bodigadi ni sawa na kumtoa sadaka. Kama hujui, basi wapo wenzako leo hii wanalia kwa kusaga meno. Kiherehere chao kiliwaponza. Binadamu hafugwi kama kuku wa kisasa.
Wapo wengi ambao walipowaweka mabodigadi, ikawa ni kama wamerahisisha maisha. Wenzi wao wakatoka na hao hao mabodigadi. Kwa mwenye mali inakuwa ngumu zaidi kujua. Bodigadi atajitaja?
Bila shaka haiwezekani. Hii ina maana kuwa bodigadi ataendelea ‘kula’ chakula cha bosi wake bila mhusika mwenyewe kujua. Mwenye mali akingoja aambiwe mwizi ni nani, kumbe kikulacho kipo nguoni mwake.
Siku anagundua inakuwa kilio na majuto. Haitasaidia, kwani majuto ni mjukuu! Ulisikia jinsi mke wa Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, Nompumelelo Ntuli alivyopewa mimba na bodigadi wake wa Ikulu. Yanatokea na yapo.
Ni wivu lakini huu ni ule ambao huzidi hisia za ndani. Ukikaa peke yako unakosa amani kwa kudhani kuwa kule ambako mwenzi wako yupo, atakuwa anakusaliti kwa mwanaume/mwanamke mwingine.
MTAGOMBANA KILA SIKU
Ukiachana na pointi hiyo kwamba anaweza kukusaliti, kubwa zaidi ni jinsi ambavyo uhusiano wenu unavyoweza kuingia kwenye misukosuko ya mara kwa mara. Wasioaminiana, hawawezi kupitisha wiki bila ugomvi.
Mwenzi wako akichelewa kurudi nyumbani, jambo la kwanza utashikwa na wasiwasi. Hautakuwa wasiwasi wenye maumivu ya hofu kwamba pengine yupo kwenye matatizo, la hasha!
Si ajabu hapo ulipo utavuta picha kwamba yupo kitandani na mtu mwingine kwenye nyumba ya kulala wageni, wote wawili hawana nguo hata moja. Ukifumba macho unaona ‘live’. Kichaa kinazidi kukupanda.
Akirudi nyumbani, badala ya kumuuliza za huko atokako, utamvaa huku kifua chako kikiwa kimejaa jazba. Atakalokujibu hutalielewa kwa maana ndani ya ubongo unamfikiria vibaya na umeshamjaza tuhuma nyingi.
Maskini wa Mungu, kumbe mwenzake alicheleweshwa na foleni za njiani. Inawezekana kazi za siku hiyo zilikuwa nyingi kuliko kawaida. Pengine ofisini kwake kulikuwa na wageni ambao walimfanya ashindwe kutoka kwa wakati muafaka.
Endapo atakujibu ukweli alionao lakini wewe ukawa unasisitiza ugomvi, mwisho mtagombana kweli. Baadaye ataona kama noma na iwe noma, hivyo ukipanda naye atakupandishia. Mapenzi hayapo hivyo.
Kuna faida kubwa unapomuamini mwenzi wako. Busara zikuongoze kuwa mtulivu. Hata kama anakusaliti, hutakiwi kupandisha mizuka na kumwaga tuhuma zisizo na uthibitisho, vaa hekima kukusanya ushahidi.
Ni kosa kubwa kuishi na mwenzi wako kwa mtindo wa kuwindana. Kwamba ndani ya ubongo wako unaamini anakusaliti, kwa hiyo unamtega aingie kwenye 18 zako muachane. Huo ni uhusiano ambao hauwezi kuwa na furaha.
Itaendelea wiki ijayo.
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment