Saturday, September 3, 2011

Hasara ya uongo katika mapenzi

NINA imani wote mu wazima baada ya kusherehekea sikukuu ya Idd el Fitr kutokana na kumalizika kwa mfungo wa mwezi wa Ramadhan, japo kuna wengine wanaendelea na sita.

Kama ilivyo ada tumekutana tena kuendelea na kiporo chetu kilichozungumzia juu ya faida na hasara ya uongo katika mapenzi. Wiki iliyopita tuliona faida ya uongo katika mapenzi.

Siku zote faida ya uongo ni kuficha hila zako bila mlengwa kukugundua, lakini hasara zake ni kubwa, mara nyingi unapogundulika kwamba umeongopa, hupoteza uaminifu na kuonekana mtu usiyefaa kwenye jamii.


Katika mapenzi ya sasa, wengi huishi katika ngozi ya uongo ili kuendesha maisha yao au kumpata mtu ambaye anaamini akimueleza ukweli anaweza kumkosa.

Kweli umefanikiwa kumficha mwenzako kuwa hujaoa au hujaolewa kumbe umo ndani ya ndoa, wengine huficha hata kama wana watoto ili kufanikisha wanavyovitaka na kusahau hakuna uongo wa milele.

Wengi wanaoishi katika uongo, hua ni watu wa mashaka kwa kuhofia siri zao kuvuja. Hata kama akiwaona watu wakizungumza pembeni yake anaanza kujihisi kutetwa. Mwisho wake siku siri inabainika unajikuta ukimpoteza mpenzi wako ambaye hawezi kukuamini tena.

Huenda umemdanganya zaidi ya miaka 10 ukiamini siri ile itaendelea milele. Napenda kuwaeleza watu kuhusu uongo katika mapenzi, mwanzo huweza kuona upo sawa lakini unasahau umezungukwa na jamii ambayo inakufahamu toka nitoke. Kwa vile hakuna siri ya watu zaidi ya mmoja ipo siku itamfikia mwenzako.

Kwa vile ulimfanya mjinga miaka mingi, basi anakuona humfai maishani na kuamini mambo mengi unayoyafanya huwa unadanganya hata kama umefanya jambo la kweli. Kwa vile umeonekana una rekodi ya uongo, hutaaminika tena.

Kwa wenye moyo mdogo wakijua kuwa wewe si mkweli, lazima watauvunja uhusiano kutokana na kukosa sifa za mpenzi wa kweli, mwaminifu na muwazi.

Hebu tuache kujificha nyuma ya kivuli cha uongo ambacho ni sawa na kukata tawi ulilokalia ukianguka utakosa wa kumlaumu. Katika kutafuta mpenzi wa kweli vitu hivi vinatakiwa kuzingatiwa: Uwazi na ukweli ndivyo vinavyolinda mapenzi ya kweli.

Unapokuwa muwazi na mkweli kwa mpenzi wako inakufanya uishi kwa uhuru zaidi na unapomueleza ukweli mpenzi wako mpya kuwa una mtoto au ulioa au kuolewa na kuachwa na kumuona mtu huyo anaruka futi 100, amini huyo si mtu sahihi kwako.

Kuolewa na kuachwa au kuzaa si kigezo cha mtu kukuruka futi 100, ukiona hivyo amini mtu huyo yupo na wewe kwa ajili ya tamaa zake za mwili na si kuishi pamoja.

Si vizuri kuwanyanyapaa waliokuwa na matatizo mwanzoni mwa uhusiano wao, kufanya hivyo ni kuwalazimisha kusema uongo ili kulilinda penzi lao. Tukubali ukweli, pia tuwe tayari kuonyesha moyo wa upendo na si wa matamanio.
Kwa hayo machache tukutane wiki ijayo.
Na Ally Mbetu 'Dr ambe' Simu: 0713 646500, Email: ambedkt@yahoo.com

No comments: