ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, September 14, 2011

Usikubali kuwa chanzo cha mpenzi wako kukusaliti -2

USALITI ni jambo lisilokubalika, si tu kwenye mapenzi, bali katika eneo lolote kwenye maisha yetu. Msaliti hafai. Hata katika mafundisho ya dini, inashauriwa watu kuacha usaliti. Ndiyo mada ninayoichambua hapa rafiki zangu.

Sina shaka ni wazima...ok! tuendelee na mada yetu ambayo nilianza nayo wiki iliyopita. Pointi kubwa hapa ninayoisimamia ni kumfanya mwenzi asiwe chanzo cha mwenzake kumsaliti.


Mpo rafiki zangu? Kama mtakumbuka wiki iliyopita wakati naanza kuandika mada hii, nilieleza kwamba usaliti wakati mwingine inawezekana kabisa, mwenzi mmoja akamsababisha mwenzake. Kipengele cha kwanza kukianisha ilikuwa ni utambuzi wa majukumu. Hebu sasa twende pamoja tukaone vipengele vingine.

KUACHA KUMJALI MWENZAKE
Wakati fulani, baadhi ya wanawake wakishapata mtoto/watoto humsahau mwanaume wake na kuhamishia mapenzi yake kwa mtoto/watoto. Kwamba wanashidwa kugawanya mapenzi vyema kati ya mumewe na mwanawe.

Hili limekuwa tatizo kubwa sana kwa sababu baadhi ya wanawake wakishapata watoto huwasahau kabisa waume zao na kutumia muda mwingi zaidi kuwa na watoto. Wanawake wa aina hii wapo tayari kulala usiku mzima akiwa amemgeukia mwanaye na kumpa mgongo mumewe hadi asubuhi.

Kwa kufanya hivyo wanashidwa kufahamu kuwa mume ataona kuwa hawajali, hivyo kuchochea hamu ya kutafuta hifadhi nyingine nje ya ndoa. Habari mbaya kwao ni kwamba, wanawake wa nje huwa wataalamu na wajanja sana katika suala zima la mapenzi, hivyo kumfanya mwanaume kuwa mpofu dhidi ya mkewe kutokana na kuzama katika mapenzi mazito ya kiruka njia!

Rafiki zangu, mnapaswa kutambua kitu kimoja, japokuwa una mtoto tena anayehitaji mapenzi na huduma zako lakini tambua kuwa una mumeo ambaye pia anahitaji mapenzi yako. Hakika kilio hiki hakiwezi kuisha kama wanawake wa aina hii hawatabadilika na kuwajali waume zao.

Tambua kuwa bila mumeo huyo mtoto wako unayemjali na kushinda naye kutwa nzima ukimmbembeleza kadhalika usiku kucha akiwa ubavuni mwako asingekuwepo! Jitahidi kugawanya mapenzi kwa mwanao na mume wako.

Tambua kuwa wanawake wa nje maarufu kwa jina la vimada ni wajanja sana tena wenye mbinu nyingi za kuwanasa waume za watu wasifurukute kwa lolote kwa kuwapa mapenzi motomoto kiasi cha kuweza kusahau nyumba zao.

TABIA YA ASILI?
Baadhi ya wanaume wana hulka mbaya za kupenda kuwa na wanawake tofauti tofauti kwa minajili ya kuangalia ladha tofauti za mapenzi! Wanaume wa aina hii wapo, hata wakipewa mapenzi ya aina gani hulka hii mbaya waliyonayo huwasukuma kuwa na wanawake wengine wa nje.

Wanaume hawa hupenda kuwa na wanawake tofauti kutokana na tamaa zao za kimwili. Mwanaume wa aina hii ni rahisi sana kumtambua unapokuwa katika uhusiano naye kabla ya kuingia katika ndoa.

Mara nyingi hata unapotoka naye katika matembezi ya jioni au kwenye kumbi za burudani, huweza kusifia mwanamke mwingine aliyepita karibu yenu. Mwanaume wa aina hii hashindwi kukueleza anavyovutiwa kimapenzi na mwanamuziki, mnenguaji au mwigizaji fulani mnapokuwa pamoja katika matamasha yao au mnapoangalia runinga yenu nyumbani.

Tabia za mwanaume wa aina hii huonekana mapema na hivyo ukiona alama hizi ni vyema ukaepukana naye mapema kabla ya kuingia katika ndoa ambayo kwa hakika itakuwa chungu kwako! Wanaume hawa hata ukiwapa mapenzi kiasi gani bado hutoka nje kutokana na hulka yake hiyo mbaya.

ZINGATIO LA MWISHO
Usiruhusu usaliti katika penzi lako, usaliti siyo mzuri hata kidogo katika maisha ya kimapenzi. Unatakiwa kuhakikisha unatumia kila njia kuhakikisha kwamba kunakuwa hakuna usaliti katika penzi lako.

Kwa vipengele hivyo hapo juu, ninaamini kuna mengi mapya uliyojifunza, unachotakiwa kufanya ni kufanya mabadiliko ya dhati katika ndoa yako. Mahali ambapo unahisi ulikuwa unakosea, anza sasa kufanya mabadiliko na uwe mpya katika penzi lako.

Uwezo wa kuruhusu au kukomesha usaliti katika uhusiano wako upo mikononi mwako. Bila shaka umenielewa na utafanya kitu fulani cha tofauti katika maisha yako. Rafiki zangu, mapenzi ni sanaa, kila siku unapaswa kuongeza ujuzi.

Mwisho wake ni kwamba, utakuwa bora kila siku na suala la maumivu kwako litabaki kuwa historia. Niseme nini zaidi ya kukushukuru kwa kutumia muda wako kunisoma? Ahsanteni sana. Tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine kali.

Joseph Shaluwa ni mshauri wa mambo ya mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love vilivyopo mitaani. Kwa makala zaidi tembelea www.globalpublisherstz.com

No comments: