ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, October 22, 2011

UKIMUAMINI MWENZI WAKO, MAISHA NI RAHISI

Wakati mwingine watu wanagombana kwa sababu ya kutoaminiana. Asilimia 95 ya uhusiano uliovunjika, ulizingirwa na mazingira ya mmoja kutomuamini mwenzake au wote wawili kuishi kama paka na panya.

Yaani kila mmoja kuhisi mwenzake anamsaliti. Kudhani ana mtu mwingine anayetenda naye mambo ya faragha ambayo na halali kwake. Hii ni hatua mbaya kabisa, haiwezekani kukawa na maelewano kipindi ambacho kila mmoja ana shaka juu ya mwenzako.


Hii ndiyo sababu ya wengi kuachana, ingawa vipo vyanzo vingine kama vile kufumaniana na mambo mengine ambayo hutokea ghafla na kufanya wahusika kutengana.

Hata hivyo, ukosefu wa uaminifu ndiyo huchukua nafasi pana.

Zipo hisia zinazowaongoza wanaume wengi kuhusu wanawake.

Hawataki wafanye kazi, ikibidi wakae tu nyumbani kwa hoja kuwa wanapokuwa maofisini wataanzisha uhusiano mpya.

Wale wanaoruhusu wake zao wafanye kazi, kila siku roho juu. Macho pima kwenye simu za wenzi wao. Hawana imani ya asilimia 100 kwamba siku hupita bila kusalitiwa. Wanateswa na sononeko la moyo.

Haipendezi kumfikiria mwenzako kwa ubaya. Inashauriwa umuamini na ujiamini. Mawazo chakavu kuhusu mwenzi wako ni sumu. Ukiyaendekeza yanaweza kukufanya ushindwe kutekeleza mambo ya msingi.

Nimewahi kutoa mfano wa wimbo “Wasiwasi wa Mapenzi” wa mwanamuziki Stara Thomas. Aliimba wasiwasi wa mapenzi mwenzangu waua, waweza waza uongo bila wewe kujijua.

Ukikushika, unaweza kumvaa mtu asiye na hatia na kugombana naye kwa sababu tu ya mawazo kwamba anakuchukulia mali yako. Siku zinasogea, baadaye unakuja kugundua kuwa hisia ndizo zilikupeleka ndivyo sivyo.

Busara za kisaikolojia zinakutaka uwe huru, kwa maana unatakiwa ujiepushe na mawazo mabaya. Mtu akipiga simu ya mwenzi wako, si ukurupuke na kuanzisha songombingo, hebu vaa utulivu na usuluhishe kwa nidhamu.

Kushika simu ya mwenzi wako na kukagua simu zinazoingia na kutoka ni alama ya kutomuamini. Ingekuwa humtilii shaka yoyote, usingethubutu kukiganda ‘kiselula’ chake.

Unataka kuona SMS zinazoingia na kutoka. Hulali mpaka uone simu alizopiga na alizopigiwa. Presha hiyo yote ya nini? Jaribu kumuamini na umuoneshe jinsi usivyo na shaka naye. Mwache yeye mwenyewe atumie vibaya imani yako kwake.

Kuna mtu kwa wasiwasi alikuwa anashindwa kutimiza majukumu yake ya kila siku, badala yake anakwenda kujificha nje ya ofisi ya mke wake, anashinda pale, lengo ni kuona wakati wa ‘lunch’ mkewe anaongozana na nani.

Ikiwa siku hiyo mkewe kaongozana na mfanyakazi mwenzake wa kiume kwenda lunch, jioni nyumbani ni kesi. “Nimepata taarifa zako, leo ulikwenda lunch na mwanaume, yule ni nani?” Hana lolote, hajaambiwa na yeyote, yeye mwenyewe na upekupeku wake.

UNAMDHALILISHA MWENZIO
Shika hili; Iwe hutaki mwenzi wako afanye kazi au unamsumbua kwa namna yoyote ile, jawabu ni moja tu kwamba unamdhalilisha na humheshimu.

Kutokuwa na imani na yeye, maana yake ndani yako kuna hisia kuwa hajatulia.

Unadhani ni vema kumuona mwenzi wako hajatulia? Kama ndivyo, unaendelea kuwa naye kwa sababu gani? Asipoheshimiwa na wewe, unataka nani mwingine ampe heshima?
Mwenzi wako anapogundua kuwa humheshimu, taratibu naye atakushusha thamani.

Akigundua huna imani naye, atakosa raha. Hata kama anakustahi leo, ipo siku ataona hana sababu ya kuendelea na wewe.

Mwingine anahaha kuulizia nyendo za mwenzi wake kwa marafiki. Hilo ni kosa kubwa kwa sababu huyo unayemuuliza, mwisho anaondoka na kitu kikubwa kwamba hakuna uaminifu kwenye uhusiano wako.

Kuna mtu ambaye huweka mabodigadi wa kufuatilia nyendo za mke wake kila anapokwenda. Anayedhani kufanya hivyo ni dawa, ameula wa chuya kwa uvivu wa kuchagua. Anakosea kupita kiasi.
Itaendelea wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

No comments: