ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 9, 2012

Aidanganya Polisi kumkomoa ‘mkewe’ atozwa faini 1000/-

MKAZI wa Sumbawanga, Geoffrey Chanzila maarufu Ulaya, amehukumiwa kwenda jela miezi sita kwa kosa la kutoa taarifa ya uongo Polisi kwa nia ya kumkomoa ‘mkewe’ baada ya ugomvi. 

Kabla ya hukumu hiyo iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Sumbawanga mwishoni mwa wiki, Chanzila alidaiwa mahakamani hapo kuwa alifanya kosa hilo Julai 7 mwaka jana saa 5:30 usiku. 

Mkaguzi wa Polisi, Elija Matiku alidai kuwa siku ya tukio, Chanzila aligombana na mkewe ambaye hakutajwa jina aliyekimbilia katika nyumba ya rafiki yake wa kike kujihifadhi. 


Matiku alidai kuwa baada ya Chanzila kuona hivyo, alikwenda Kituo cha Polisi mjini Sumbawanga usiku huo na kutoa taarifa kuwa katika eneo la Kantalamba, kuna nyumba ambayo aliona majambazi wawili wakiingia wakiwa na silaha ya kivita aina ya SMG. 

“Mtuhumiwa aliwaomba askari Polisi wafuatilie taarifa hiyo kwa haraka na maofisa wa Polisi 
waliona ni dharura inayohitaji kufanyiwa kazi haraka. 

“Askari Polisi waliacha kazi ya kuwahudumia wananchi wengine walioonekana kuwa na matatizo madogo madogo na kwenda eneo la tukio,” alidai Matiku. 

Kwa mujibu wa madai ya Mwendesha Mashitaka huyo, askari walipofika katika nyumba iliyotajwa kuvamiwa, walimkuta mke wa mtoa taarifa na mwenyeji wake. 

Matiku alidai walipomhoji, mke huyo akaeleza kuwa alikosana na mumewe huyo na kukimbilia katika nyumba hiyo kwa rafiki yake wa kike kujihifadhi. 

“Hivyo Chanzila alitoa taarifa za uongo Polisi kwa lengo la kuwakomoa waliomhifadhi mkewe,” alidai Matiku na kuongeza kuwa ndipo walipoamua kumfungulia mashitaka ya kutoa taarifa za uongo. 

Baada ya Matiku kumaliza kutoa madai hayo, Hakimu wa Mahakama hiyo, Rosalia Mugissa 
alisema upande wa mashitaka umethibitisha kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo na kutoa hukumu hiyo. 

“Natoa adhabu hii iwe fundisho kwa watu wenye tabia ya kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa Serikali hasa Polisi,” alisema Hakimu Mugissa. 

Hata hivyo, sehemu ya pili ya hukumu hiyo mshitakiwa alitakiwa kulipa faini ya Sh 1,000 ambapo alilipa na kuachiwa huru lakini upande wa mashitaka ukaelezea nia yake ya kukata rufaa kupinga adhabu hiyo kuwa ni ndogo.


CHANZO:HABARI LEO

No comments: