Mtoto wa mwisho wa Marehemu Galinoma Celina Galinoma akiweka shada la maua katika kaburi la babake marehemu Galinoma
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Deo Sanga, jana aliongoza mamia ya wakazi wa mkoa wa iringa katika mazishi ya Mbunge wa zamani wa Kalenga, mkoani hapa, Steven Galinoma (CCM), aliyezikwa jana katika makaburi ya Kitongoji cha Kihaja, Wilaya ya Iringa Vijijini.
Galinoma alifariki dunia Januari 26, mwaka huu, kutokana na ugonjwa wa saratani akiwa njiani kupelekwa katika Hospitali ya Misheni ya Ipamba iliyopo Iringa Vijijini akitokea kijijini kwake Kalenga.
Mazishi hayo yake yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwamo wa serikali, vyama vya siasa, asasi za kiraia, ndugu, jamaa, marafiki na majirani, akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma.
Wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mjini, Evance Balama, Mwanasheria wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alex Mgongolwa, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kapteni Mstaafu Aseri Msangi, wenyeviti wa CCM wa Wilaya na makatibu wa chama hicho wilaya za Mkoa wa Iringa.
Wabunge wa mkoa wa iringa waliwakilishwa katika mazishi hayo na Mwenyekiti wa Kamati ya Wabunge wa Iringa, Dk. William Mgimwa, ambaye ni Mbunge wa Kalenga (CCM).
Akizungumza katika mazishi hayo, Sanga ambaye ni Mbunge wa Njombe Kaskazini (CCM), alisema CCM imepoteza mpigania haki na mwanasiasa mashuhuri, aliyekuwa kiongozi tangu enzi za TANU mpaka.
Alisema katika uongozi wake tangu alipokuwa Katibu Mkuu wa Kwanza wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), hakuwahi kukumbwa na tuhuma wala kashfa yoyote ya ufisadi wala matumizi mabaya ya madaraka.
Sanga alisema jambo hialo limemfanya Galinoma kuondoka akiwa muadilifu na mtu ambaye hataweza kusahaulika katika taifa.
Alisema kutokana na kifo chake, CCM imebakiwa na pengo kubwa katika medani ya siasa.
Sanga alisema wao kama chama, wataendelea kuiunga mkono familia ya marehemu Galinoma na katika msiba huo, chama kimetoa ubani wa Sh milioni 1.7.
Kandoro akizungumza na NIPASHE alisema amesikitishwa sana kifo hicho kwa kuwa alimtambua marehemu alivyokuwa mchapakazi na mwadilifu katika sekta ya umma.
Dk. Ishengoma alisema serikali na kwa niaba ya CCM imempoteza mtu ambaye alikuwa na mchango mkubwa katika wa Iringa, alikuwa akihamasisha shughuli za maendeleo, ikiwamo ujasiriamali akiwa kiongozi wa mfano.
Alisema kila kiongozi na kila mwananchi hawana budi kujiandaa katika kukabiliana na changamoto iwe katika siasa au katika shughuli za maendeleo
Alisema serikali ya mkoa wa Iringa imepoteza mchango wa marehemu Galinoma katika kukabiliana na umaskini na kuhamasisha shughuli za kujiongezea kipato.
Dk. Mgimwa alisema wabunge wote wako pamoja na familia ya marehemu na wanaungana na wakazi wote wa Mkoa wa Iringa katika msiba huo wakiamini wamepoteza mpigania maendeleo asiyesahaulika haraka.CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment