ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 18, 2012

Ndugai: Tutajadili kufuta posho mpya za wabunge

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai
Waandishi Wetu
NAIBU Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema wanaangalia uwezekano wa kufuta nyongeza mpya ya posho za wabunge ndani ya siku 10 zijazo, lakini akawashambulia watu wanaoshikia bango nyongeza hiyo aliyoifananisha na tone la maji ikilinganishwa na  mamilioni ambayo alidai vigogo wa mihimili mingine ya dola wanalipana.

Kauli hiyo mpya ya Ndugai inakuja kipindi ambacho nyongeza hiyo ya posho imeibua mjadala mzito, ambao hivi karibuni Naibu Spika huyo alilazimika kujibu mapigo ya Waziri Mkuu Mstaafu,  Frederick Sumaye ambaye alionya kuwa posho hizo zinaweza kufanya taasisi nyingine za dola kudai nyongeza.

Juzi, Ndugai akizungumzia posho hizo alisema hazilingani kwa namna yeyote ile na posho wanazopewa viongozi wastaafu serikalini na Idara ya Mahakama.

Alipomjibu Sumaye kuhusu suala hilo la posho, alimshambulia  kiongozi huyo mstaafu akisema hana usafi wa kuzikosoa kwani aliwahi kufanikisha Sheria ya Mafao ya Viongozi Wakuu Wastaafu ili kujiandalia mazingira ya kula maisha mazuri.

“Hili la posho limesemwa sana na sisi tumelisikia kwa sababu ni wasikivu, kumekuwa na kelele nyingi za posho. Kwa kuwa  tunakutana siku 10 kabla ya kuanza kwa Bunge, tutakaa na kulijadili kisha tutasema tumefikia wapi,” alisema Ndugai wakati akizungumza katika Kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV.

Alisema Watanzania wanapaswa kutambua kuwa posho wanazolipwa wabunge ni kidogo ikilinganishwa na mihimili mingine ya dola huku akienda mbali na kuwagusa viongozi wa dini kwamba kuna baadhi ya maaskofu na wachungaji wanaopiga kelele  kuhusu posho hizo za wabunge bila kujua wanalipwa shilingi ngapi au zinatofautiana vipi na wachungaji wengine.
“Kuna maaskofu ambao wamekuwa wakipiga kelele juu ya hizi posho, lakini hata na wao ukiwaangalia kuna tofauti kubwa sana kwao na wachungaji katika mapato yao,” alieleza Ndugai:

Alisema wakosoaji wamekuwa wakilalamika tu bila kutoa suluhu au njia ya kutatua hali hiyo ikiwa ni pamoja na kupendekeza kiasi cha posho kinachopaswa kulipwa na kushauri kuwa taifa liunde  kamati maalumu ya kuchambua na kuweka bayana viwango vya  mishahara ya viongozi na posho zao ili kila mwananchi aweze kuvitambua.

“Wananchi wanalalamikia sana posho za wabunge kwa kuwa ndicho kitu kidogo wanachojua ambacho wameambiwa na magazeti, lakini wangejua viwango vya posho wanazolipana watu wa Mahakama na viongozi wetu wastaafu, wangeachana kabisa na hili suala la posho za wabunge,” alisema. 

Alisema pia mishahara ya wabunge ni tone tu la mshahara wa ofisa wa kawaida wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ofisa wa ngazi ya chini wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Ndugai alisema kelele hizo za wananchi zinachangiwa zaidi na hali ngumu ya maisha waliyo nayo kwa sasa... “Kama nyumbani kuna chakula kidogo, ukipika nyama na kuwagawia watoto wako finyango mbili tatu wataanza kugombea, huyu kapewa kikubwa na huyu kapewa kidogo.”

“Wenzetu wa Kenya na Mauritius wana tume ambayo ni huru na ina watu ambao wanaaminika kuwa ni waadilifu, ndiyo wanaangalia mishahara ya viongozi wa juu kama hapa kwetu labda ni kuanzia kwa mkuu wa mkoa mpaka hata Rais. Ukienda kwenye mtandao  unaona kila kitu, hakuna usiri, tupate chombo huru ambacho kitatupangia sisi wote ambao tunapata pesa kutokana na kodi za wananchi... nasema Watanzania wangejua maeneo mengine kukoje wangeachana kabisa na suala la posho za wabunge.”

Alipoulizwa kama angetaka tume hiyo ipunguze posho zilizopo, alisema ingekuwa vizuri kama ingepandisha zile zilizo chini ili angalau kuwe na uwiano... “Lakini kama ikibidi sawa, ila ndiyo yatakuwa yaleyale kuwa huyu ana nyama kubwa zaidi.”

Kuhusu posho zenyewe
Kwa mara ya kwanza Novemba 28 mwaka jana, gazeti hili liliripoti kupanda kwa posho hizo za vikao (sitting allowance) kwa wabunge kutoka Sh70,000 kwa siku walizokuwa wakilipwa awali, mpaka kufikia Sh200,000.

Hata hivyo, Katibu wa Bunge Dk Thomas Kashililah alikanusha vikali habari hiyo, lakini siku chache baadaye Spika wa Bunge, Anne Makinda alithibitisha kupandishwa kwa posho hizo ambazo wabunge walianza kulipwa katika mkutano ulioisha.

Kwa sasa inakadiriwa kuwa kila mbunge analipwa zaidi ya Sh7 milioni kila mwezi, ikiwa ni mshahara pamoja na posho nyingine.

Jumuisho hilo ni pamoja na posho ya mafuta Sh2 milioni kwa mwezi ikikadiriwa kuwa atatumia lita 1,000 ambazo makisio ni Sh2,000 kwa lita moja. Nyingine ni posho ya kukaa jimboni Sh800,000 posho ya ubunge Sh1 milioni, kuendesha ofisi Sh700,000, simu Sh500,000 na mshahara ni Sh2.3 milioni.

Wakati wa vikao bungeni, kunaongezeka nyingine za aina tatu ikiwemo ile ya ‘sitting allowance’ ambayo sasa ni Sh200,000 posho ya kujikimu Sh80,000 na usafiri Sh50,000 ambayo hupewa bila kujali kuwa tayari kuna fedha za mafuta ya mwezi mzima.

Habari hii imeandaliwa na Fredy Azzah, Fidelis Butahe, Ibrahim Yamola na Keneth Goliama wa Gazeti la Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Huyu Bwana hajui anachoongea.