Sosthenes Nyoni
MABINGWA wa soka Tanznaia, Yanga, wataweka kambi jijini Mwanza kujiandaa na mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri, mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika, CAF, mwishoni mwa mwaka jana, Yanga itaanza nyumbani, kati ya Februari 17, 18 na 19 kabla ya kurudiana mjini Cairo kati ya Machi 2, 3 na 4.
"Kama uongozi wa timu ya Yanga tunafanya mpango wa kukihamisha kikosi chetu kutoka kwenye kambi ya sasa iliyoko makao makuu ya klabu hiyo ,Mtaa wa Twiga na Jangwani na kukipeleka jijini Mwanza.
"Tumedhamiria kikwelikweli kupambana na Zamalek...hatutaki kuweka unyonge kwa kufungwa, tumepokea ushauri kwamba tunatakiwa kufanya maandalizi ya dhati kuliko ilivyo sasa, sasa tumepanga kufanya mazoezi ya siku 10 ngumu jijini Mwanza," alisema Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga.
Nchunga alisema kuwa mpango wa kuihamishia kambi ya timu hiyo umepangwa kutekelezwa baada ya wiki mbili kuanzia sasa na kwamba wataomba Shirikisho la soka Tanzania, TFF, kurekebisha ratiba ya ligi kwa mechi zake.
"Kwanza tutakuwa klabuni kwa ajili ya maandalizi ya mechi dhidi ya Zamalek na Ligi Kuu, lakini baada ya wiki mbili tunakusudia kuihamisha kambi Mwanza.
"Lengo ni kuhakikisha tunataka kuvunja mwiko wa timu za Misri kutufunga kila mara tunapokutana nazo na kubadili historia," alisema Nchunga.
Nchunga pia alizungumzia mpango wa baadaye wa klabu yake kwa kusema kuwa watalamizika kupunguza idadi ya wachezaji hadi kufikia 25 ili kuondokana na mzigo mkubwa wa gharama unaoilelemea klabu yake kwa sasa.
"Ukweli ni kwamba klabu inakabiliwa na mzigo mzito kwa sasa unaotokana na idadi kubwa ya wachezaji tunaowahudumia,hawa ni pamoja na wale walioko kikosini na wale waliowapeleka timu mbalimbali kwa mkopo ambapo pia tunawalipa sisi.
"Hivyo basi ili kupunguza mzigo huu huko mbele tunalazimika kupunguza idadi ya wachezaji kwenye usajili wetu hadi kufikia 25," alisema Nchunga.
Katika hatua nyingine, Kampuni ya Clouds Media Group kupitia kampuni tanzu ya Prime Time Promotions na uongozi wa klabu ya Yanga jana zilitangaza kuingia makubaliano kwa ajili ya kuitangaza mechi baina ya timu hiyo na Zamalek.
"Tumeingia maelewano na Clouds Media Group kupitia Prime time Promotion ambao watachukua jukumu la kuitangaza mechi yetu na Zamalek pamoja na gharama nyingine za maandalizi ya mchezo huo," alisema Nchunga
Mwananchi
No comments:
Post a Comment