KAMA nilivyoeleza wiki iliyopita, wivu mara nyingi huanza kutokana na kukosa kujiamini. Jiulize, unajisikia salama wewe mwenyewe? Je, unaogopa kwamba mpenzi wako anaweza kukuacha kwa sababu kupungukiwa sifa kadhaa? Mambo mengi kati ya hayo yanapogota kichwani, huyafanya maisha yako yatawaliwe na wivu.
Inawezekana mwenzi wako anakupenda kuliko
wewe unavyompenda. Si ajabu, akawa anawaza kufanya maisha bora zaidi akiwa na wewe. Amekukubali kwa namna ulivyo kiasi kwamba hawazi kukupoteza. Tofauti na mawazo yake, tabia yako ya kutojiamini, hufikiria kwamba hakupendi.Inawezekana mwenzi wako anakupenda kuliko
Ikitokea akawa anafanya mawasiliano na mtu wa jinsia kama yako, hapo unaanza kuweweseka, mara ukasirike, upekue simu yake bila sababu, umkaripie, unune na kususa kuzungumza naye. Hiyo ni kujipa jakamoyo. Unashindwa kujiamini kama wewe ni zaidi ya huyo anayewasiliana naye. Unaogopa atakupora mpenzi.
Kwa mwanamke, kama anamuona anamhofia mwenzi wake kwamba anaweza kumsaliti kwa kutoka na mtu ambaye huwa anawasiliana naye, hiyo ni sawa na kujiwashia taa nyekundu. Si ajabu kutokujiamini kwako kukamfanya mwezi wako aone bora amalize kesi moja kwa moja. Vilevile, kwa mwanamke mwenzako atavimba kichwa, kuona hujiamini kwa sababu yako.
Kwa mwanaume, itakufanya ukose sifa za kuonekana kidume. Mwenzio wako atakuona msumbufu na unamkosea heshima kumtuhumu kwamba anaweza kukusaliti. Amini kwamba wewe ni wa ukweli na mpenzi wako anatosheka kwa makali ambayo unayo.
Usipojiamini, utampa kichwa huyo unayemuogopa. Muamini kuwa hatakusaliti na endapo unadhani anaweza kukuendea kinyume, huna haja ya kuishi naye. Ni rahisi kuonekana katuni kwenye jamii, mjinga, bwege kama hujiamini.
Linda heshima yako, dhibiti wivu wako, jiamini. Hayo ni mambo ambayo yanaweza kukupa uwezo wa kukabili changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kuusumbua moyo wako kwa kuupa wasiwasi kuwa mwenzi wako anakuendea ndivyo sivyo.
“Yule ndugu ananiogopa kweli, anahisi namchukua mtu wake,” hii kauli anaweza kuitamka huyo ambaye wewe huna imani naye. Tambua kuwa unampa kichwa kwa maana hata jinsi anavyozungumza anaashiria kuwa yeye ndiye amebeba amani yako. Usimfanye binadamu mwenzako akajiona hivyo.
6. WASILIANA MARA KWA MARA
Una wasiwasi na mahali ambako mwenzi wako yupo? Huna amani na unahisi anakusaliti. Moyo wako umefunikwa na jakamoyo na kila hatua mapigo yanaongezeka kasi au yanashuka. Kimsingi huna sababu ya kuwa hivyo. Usiishi kwa dhana, ila simamia vitu vinavyoonekana.
Mawasiliano ni njia bora kabisa ya kudhibiti wivu. Mnapozungumza mara kwa mara au ‘kuchati’ kwa SMS, Facebook au mitandao mingine ya kijamii, huwaweka karibu. Kama una hali ya wasiwasi, itakwisha au kupungua kwa sababu muda wote utajiona kama mpo pamoja.
Je, mkiwa wawili chumbani au sehemu yoyote ya faragha, bila simu wala mtu wa tatu anayeweza kuingilia ukaribu wenu, mnaweza kuanza kulumbana kwa sababu ya kuoneana wivu? Jibu ni hapana. Hivyo basi, mawasiliano ya mara kwa mara huwaweka karibu na ni salama zaidi kuliko hata mngekuwa wawili chumbani.
Mawasiliano yasiwe yenye kuishia katika simu au mitandao, kama hamjafunga ndoa au tayari ni wanandoa lakini hamuishi pamoja, jitahidini kukutana mara kwa mara. Ikiwa mnaishi eneo moja, wekeni utaratibu wa kuonana kila inapobidi, hiyo itasaidia kukuza upendo na amani ambayo itayeyusha hulka za wivu.
Wakati ukitekeleza hili la kuonana mara kwa mara na mwenzi wako, si vibaya ukamwambia jinsi unavyoumizwa na tabia ya yeye kufanya mawasiliano ya karibu na watu wenye jinsia tofauti na yeye. Ukizungumza naye kwa upole, hali itakuwa nzuri kuliko kulaumu au kulalamika.
Hoja ya wivu iwekwe mezani halafu muijadili kwa upana. Kitendo cha kujadili na mwenzi wako jinsi wivu unavyokutesa, kitasaidia kuweka mwanga na kupata ufumbuzi wa tatizo husika. Kama atajua mambo ambayo akiyafanya utaumia halafu akatekeleza bila woga, maana yake atakuwa amedhamiria kukuumiza, hivyo hakufai kwa maisha yako.
No comments:
Post a Comment