ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 30, 2012

ZAMBIA YATINGA ROBO FAINALI

Kiungo wa Zambia, Christopher Katongo (katikati) akishangilia bao aliloifungia timu yake dhidi ya Equatorial Guinea jana kwa staili ya sarakasi. Picha na AFP
FRANCEVILLE, Gabon 
Zambia imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Can 2012) baada ya kuifunga Equatorial Guinea bao 1-0, huku Senegal ikimaliza michuano hiyo kwa aibu baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Libya.
Zambia ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa d’Angondje ambapo mfungaji alikuwa ni Christopher Katongo dakika ya 67, hivyo kuiwezesha timu yake kufikisha pointi saba na kuwa kinara wa kundi A, wakati Equatorial Guinea ikishika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi sita.
Zambia ilionyesha uwezo mzuri na kutoa upinzani mkali kwa wenyeji hao ambao walikuwa wamejihakikishia nafasi ya kufuzu hatua ya robo fainali hata kabla ya mchezo wa jana.
Libya imeambulia nafasi ya tatu baada ya kufikisha pointi nne, ambapo mabao yake katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Bata yalipatikana kupitia kwa Ihaab Albusaifi dakika ya tano na 84, wakati lile la Senegal lilifungwa na Deme N’Diaye dakika ya 10.
Katika mechi za juzi, Ghana ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mali, Botswana ikipata kipigo cha kihistoria cha mabao 6-1 kutoka kwa Guinea. Mechi za leo, Sudan itakipiga dhidi ya Burkina Faso, huku Ivory Coast ikiivaa  na Angola.

No comments: