Mapato ya mechi ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika kati ya mabingwa watetezi wa soka wa Tanzania Bara, Yanga dhidi ya Zamalek ya Misri, iliyofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Na kuhudhuriwa na maelfu ya watu yanadaiwa kuzua utata mkubwa. Inadaiwa kuwa utata huo ndio uliosababisha pande zinazohusika kushindwa kutangaza kiasi kilichopatikana hadi kufikia jana jioni.
Na kuhudhuriwa na maelfu ya watu yanadaiwa kuzua utata mkubwa. Inadaiwa kuwa utata huo ndio uliosababisha pande zinazohusika kushindwa kutangaza kiasi kilichopatikana hadi kufikia jana jioni.
Mechi hiyo ya awali iliyomalizika kwa sare ya 1-1, ilivutia mashabiki wengi na sehemu kubwa ya viti vya Uwanja wa Taifa unaoingiza mashabiki 60,000 kwa wakati mmoja ilijaa kutokana na sababu kadhaa, ikiwemo ya mvuto wa timu zilizokuwa zikipambana.
Habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana zilisema kuwa tayari fedha zilizopatikana zilikuwa zimeshakamilika kuhesabiwa, lakini tofauti zilizopo kati ya uongozi wa Yanga na kampuni iliyopewa dhamana ya kusimamia mechi hiyo ikiwemo ya matangazo na mauzo ya tiketi ndizo zilizoibua utata unaokwaza mchakato wa kutangaza kile kilichopatikana.
Chanzo chetu kilidai kuwa baadhi ya viongozi wa Yanga wamekuwa sehemu ya utata uliopo kwani bado hawajaridhia kutangazwa kwa kiasi cha fedha kilichopatikana, tena bila ya kuweka wazi sababu ya kufanya hivyo.
Habari zaidi zilidai kuwa kampuni iliyosimamia mechi hiyo haitaki kwenda kinyume na taratibu walizokubaliana na Yanga tangu awali.
"Sisi tunataka kuonyesha tofauti yetu baada ya kuingia katika mpira,” kilisema chanzo kimoja kutoka ndani ya kampuni iliyoingia mkataba na Yanga kuhusiana na mechi hiyo.
Kiliongeza chanzo hicho kuwa kitu kikubwa kinachoonekana kuchelewesha mchakato wa kutangaza fedha zilizopatikana ni nia ovu ya baadhi ya watu wanaotaka 'kuchakachua' mapato hayo kwa kutangaza kiasi kidogo kulinganisha na kile kilichokusanywa, lengo likiwa ni kujinufaisha binafsi.
Jithada za mwandishi kuupata uongozi wa kampuni iliyosimamia mechi hiyo jana zilishindikana.
Hata hivyo, Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema kuwa mapato hayo bado hayajajulikana kwa sababu ya kutokamilika kwa taratibu za kiutendaji, ingawa alithibitisha kuwa tayari wameshamaliza zoezi la kuhesabu fedha zote zilizopatikana.
Sendeu alisema kuwa bado wanajadiliana kutokana na mikataba waliyoingia kabla ya mechi, na kwamba ni lazima hesabu zikokotolewe kwanza kabla ya mgao kwa kuwa kwenye makubaliano yao, Yanga ilishalipwa malipo ya awali ya Sh. milioni 60.
Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa TFF haihusiki na suala la mapato ya mechi hiyo na badala yake, wanaopaswa kuulizwa ni Yanga na kampuni waliyoingia nayo mkataba.
Wambura aliongeza kuwa jukumu la TFF ni kusimamia mchezo, lakini mapato yalisimamiwa na Yanga na kampuni waliyoingia nayo mkataba, hivyo hata wao wanasubiri kuletewa ripoti kuhusiana na kiasi cha fedha kilichopatikana.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment