Chama cha Wananchi (CUF) kimetangaza kuwa kitachukua hatua dhidi ya viongozi wandamizi wa kitaifa waliojizulu nyadhifa zao hivi karibuni kama itathibitika kuwa shutuma walizozielekeza kwa chama hicho hazina ukweli.
Waliojiengua ni Abubakar Rakesh na Juma Kilaghi ambao ni wajumbe wa Baraza Kuu la Taifa na Mkurugenzi wa Sekretarieti ya Vijana, Omary Constantine, kwa kile walichodai kuchoshwa na ukiritimba wa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Shaweji Mketo, aliiambia NIPASHE jana kuwa tuhuma zilizotolewa na viongozi hao wakati wanatangaza kujivua uongozi zitajadiliwa katika Kikao cha Baraza Kuu la Taifa kitakachofanyika mwezi ujao. Alisema pamoja na mambo mengine, kitajadili hatua iliyochukuliwa na viongozi hao kwa kuelekeza shutuma dhidi ya chama na endapo watakutwa na hatia chama kitachukua hatua za kinidhamu .
Mketo alisema suala la kujivua nyazifa za uongozi ni moja ya ajenda za chama, lakini kiongozi anapojivua hana sababu za kutoa tuhuma za uongo dhidi ya chama kwa lengo la kutaka kupata umaarufu wa kisiasa.
Mketo aliwatupia lawama viongozi hao kwa kutokuweka wazi sababu zilizopelekea wajioe ndani ya chama na badala yake wanazungumzia suala la mtu. Alisema uongozi hautalalamika juu ya kujitoa kwa viongozi hao bali utalalamika kwa nini wanataka kukiharibu chama.
“Mwenyekiti wa Taifa Profesa Ibrahimu Lipumba amepata taarifa, lakini bado hajasema chochote juu ya suala hilo ingawa hawezi kuingilia maamuzi ya mtu zaidi ya kubariki maamuzi yao,” alisema Mketo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment