ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 7, 2012

Kikwete awafuata wabunge Dodoma

Rais Jakaya Kikwete akiteta jambo na Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid (kushoto), baada ya Rais kuwasili Uwanja wa Ndege wa Dodoma jana akitokea jijini Mwanza.(PICHA: OFISI YA WAZIRI MKUU)
  Ni kupata ukweli wao sheria ya katiba mpya
  Wabunge wa CCM wanadaiwa kuukataa
  Dk. Slaa amshauri Kikwete avunje Bunge
Baada ya kutokea kutokuelewana baina ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yao kuhusu maudhui ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, jana Rais Jakaya Kikwete, aliwasili mjini Dodoma kwa kile kinachoelezwa ni kukutana na wabunge hao.

Rais Kikwete alilakiwa katika uwanja wa ndege wa Dodoma na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kisha kuelekea Ikulu ya Chamwino, na wabunge wa CCM tangu Bunge linaahirishwa baada ya kipindi cha maswali na majibu jana asubuhi, walielezwa wasizime simu zao kwani wangeliweza kuitwa wakati wowote.
Ilipofika saa 12:44 jioni, baadhi ya wabunge walilithibitisha NIPASHE kuwa walikuwa wamepelekewa ujumbe mfupi wa simu za mkononi (sms) wakielezwa wakae tayari (standby) kwani wangeweza kuitwa wakati wowote.
Ijumaa iliyopita wabunge hao waliwachachamalia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, ambaye aliwaeleza wabunge waliokuwa wanaupinga muswada huo ambao walidai kuwa marekebisho ya sheria hiyo yalikuwa yanakiweka kitanzini chama chao huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ikipewa nguvu kubwa kisiasa baada ya kuenguliwa kwa wakuu wa wilaya katika sheria ya kusimamia mchakato wa kukusanya maoni ya katiba mpya na badala yake kuingizwa kwa wakurugenzi watendaji wa halmashauri nchini.
Wabunge hao walichachamaa baada ya kuelezwa kuwa mabadiliko hayo yalikuwa na baraka za Rais.
Pia wabunge hao katika kikao chao kilichofanyika usiku Ijumaa iliyopita walidai kuwa Chadema walikuwa na nafasi ya kushiriki katika upitishaji wa muswada huo wakati wa mkutano wa Bunge wa Novemba mwaka jana, lakini walisusa na kutoka nje, lakini wakaenda kuoanana na Rais Kikwete, kitu ambazo wanatafsiri kuwa ni sawa na kutumia njia za mlango wa nyuma kulazimisha mambo yao katika sheria hiyo.
Habari za ndani ya mkutano huo zilisema kuwa baadhi ya wabunge walikuwa na jazba kubwa, kiasi cha kutamani kutikisa nguvu za rais, ingawa wengine walionya kuwa mwelekeo huo unaweza kuwa na hatari kubwa ya kisiasa si kwao tu bali kwa chama kwa ujumla kwani wabunge wote wa CCM wapo kwa ajili ya kumsaidia Rais na si kumuhujumu.
Ingawa hoja inayopigiwa chapuo kwa wazi zaidi ni suala la kubebwa kwa Chadema katika maudhui ya muswada huo, kuna hisia za ndani miongoni mwa wabunge hao katika suala zima la kuzimwa kwa ndoto yao ya nyongeza ya posho za kikao cha Bunge kutoka Sh. 70,000 kwa siku hadi Sh. 200,000.
Posho hizo pamoja na Spika wa Bunge, Anne Makinda na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutangazia wabunge kuwa zilikuwa na baraka za Rais Kikwete, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais ilikanusha vikali habari hizo na kusema “Rais hajabariki ongezeko la posho.”
Safari ya Rais Kikwete Dodoma inaelezwa ni juhudi za kutaka kujua hasa wabunge hao wana malalamiko gani, kwani kiasi cha kutishia kukwamishwa muswada wa marekebisho ya sheria ya katiba mpya ya mwaka 2011.
Muswada huo ulikuwa ujadiliwe kuanzia jana, lakini uliondolewa kwenye ratiba ya shughuli za Bunge dakika za majeruhi, taarifa kutoka Ofisi ya Katibu wa Bunge ilisema kuwa Kamati ya Uongozi ndiyo ilikuwa inasubiriwa kupanga siku ya kuwasilishwa.
Jana Kamati ya Uongozi inayokutanisha Spika wa Bunge, naibu wake, Waziri Mkuu, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Waziri Mwenye Dhamana na Bunge na wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge, haikuwa imekutana hadi tunakwenda mitamboni.


Mkutano wa sita wa Bunge ulioanza Jumanne iliyopita unatarajiwa kumaliza wiki hii. Jana wabunge walikutana kwa kipindi cha maswali na majibu tu. 


SLAA: JK VUNJA BUNGE
Katika hatua nyingine, Chadema kimemshauri Rais Kikwete kuvunja Bunge endapo wabunge wa CCM wanaojali maslahi yao binafsi wataendelea na msimamo wa kutaka kukwamisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011.
Ushauri huo ulitolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, akisema hakuna sababu kwa Rais Kikwete kuendelea kuchezewa na wabunge ambao ni idadi ndogo ikilinganishwa na Watanzania zaidi ya milioni 40 ambao watanufaika na muswada huo.
Dk. Slaa aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa kusingizia bungeni huku idadi ndogo isiyozidi wabunge 100 ikichangia mawazo kunaweza kukwamisha muswada mzuri wa serikali, hivyo ni bora Rais Kikwete afanye maamuzi magumu ikibidi kulivunja Bunge.
Alisema kila siku CCM imekuwa ikisema ni sikivu kwa wananchi wake, lakini anashangaa kuona suala linachohusu wananchi moja kwa moja wanashindwa kulisikia na badala yake wanalipinga kwa nguvu zote.
“Haiwezekani Rais Kikwete awakubalie wabunge 350 wa CCM huku akiacha maoni ya wananchi walio wengi ambao wametoa maoni yao ambayo yamo katika muswada huo wa Sheria wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema Dk. Slaa.
Alitaja baadhi ya marekebisho yaliyomo katika muswada huo kuwa ni pamoja na kutaka wakuu wa wilaya wasiwe sehemu ya mchakato wa kupata katiba mpya na Rais kuteua wajumbe wa Tume ya kuratibu maoni kwa kushauriana na vyama vya siasa, mashirika yasiyokuwa ya serikali na wananchi wengine.
Dk. Slaa alisema mambo hayo ni mazuri, lakini CCM wao wanayaona ni mabaya na kusema kuwa hatua hiyo wanastahili kuondolewa baada ya Rais kuvunja Bunge.
Aliongeza kuwa Bunge halipo makini kwani baadhi ya wabunge wako tayari kutetea ongezeko la posho, lakini wanakataa kupitisha muswada ambao una faida kwa wananchi wote wa Tanzania.
Inadaiwa kuwa wabunge wa CCM wanasema kwamba marekebisho hayo yanalenga kukimaliza chama chao na kukiweka madarakani Chadema baada ya kuondolewa kwa wakuu wa wilaya kushiriki mchakato wa katiba na kazi hiyo kukabidhiwa wakurugenzi wa halmashauri.
Imeandikwa na Richard Makore, Dar; Sharon Sauwa na Abdallah Bawaziri, Dodoma.
CHANZO: NIPASHE

No comments: