ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 7, 2012

Mwenyekiti achafua hali ya hewa bungeni

Naibu Spika, Job Ndugai.



Mvutano mkubwa umezuka bungeni jana baada ya wabunge wawili kuomba mwongozo wa Spika kuhusu uamuzi wa Mwenyekiti wa Bunge, Sylivester Mabumba, kuondoa marekebisho ya moja ya kifungu cha Muswada wa Sheria ya Kudhibiti Fedha Haramu bila kufuata kanuni.

Hali hiyo imelazimu serikali kutoa hoja ya kukirudisha tena kifungu hicho ili kipitiwe upya na Bunge ili kuondoa mgongano huo.
Baada ya kipindi cha maswali na majibu, wabunge kadhaa walisimama wakitaka muongozo wa Naibu Spika, Job Ndugai.
Kifungu hicho kimo katika muswada huo ambao ulipitishwa na wabunge Ijumaa iliyopita.
Wabunge  waliomba kuongezwa kwa kiwango cha adhabu kwa mtu anayekamatwa kwa makosa hayo kutoka  kifungo kisichozidi miaka mitatu hadi kifungo kisichopungua miaka 10.
Waliotoa mapendejezo hayo ni Mbunge wa Ubungo, (Chadema), John Mnyika na Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi) Felix Mkosamali.


Baada ya Mnyika kutoa pendekezo hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji  Fredrick Werema, alitoa ufafanuzi kuwa kurekebisha kifungu hicho kutakinzana na sheria mama ya makosa ya jinai.
Lakini wakati Bunge likiwa limekaa kama kamati kupitisha vifungu, Mabumba (Dole-CCM), alisema kifungu hicho kimepitishwa pamoja na marekesho yake, bila ya kuzingatia maoni ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Baada ya hatua zote za kupitisha Muswada huo kukamilishwa, Mbunge wa Simanjiro, (CCM), Christopher  Ole Sendeka, aliomba mwongozo na kukosoa uamuzi huo kuwa haukuzingatia maoni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mabumba alisema yeye ni binadamu na anaweza kukosea kabla ya kuyaondoa mapendekezo hayo yaliyotolewa na Mnyika na Mkosamali.
Hata hivyo, jana muda mfupi kabla ya kuahirishwa kwa kikao cha Bunge, Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali, alisimama na kuomba mwongozo wa Spika.
“Mheshimiwa Spika Ijumaa iliyopita Bunge lilipokaa kama kamati na kupitisha kifungu hiki, marekebisho yalifanywa na kiti pekee bila ya kulishirikisha Bunge hivyo naomba suala hili tulijadili,” alisema.
 Baada ya hapo, Mnyika alisimama na kuomba mwongozo wa Spika juu ya suala hilo, akisema Mwenyekiti amekwenda kinyume na kifungu cha 88 (8) kinachosema mtoa hoja akishamaliza Spika anatakiwa kuwahoji wabunge kama wameafiki au la.
Alisema pia muswada huo umesomwa mara mbili na kisha kujadiliwa kinyume cha kanuni ya 89 (1) kinachotaka muswada usomwe mara tatu kabla ya kujadiliwa.
 Baada ya Mnyika kusema hayo, Sendeka, naye aliingilia kati baada ya kuomba mwongozo wa Spika. “Kanuni ya 53 (8) inasema mtu yoyote hatafufua jambo lolote lililopitishwa na Bunge na kama atakuwa hajaridhika anatakiwa kuwasilisha malalamiko yake kwa Spika kwa mujibu wa kifungu 5 (4),” alisema.
Hata hivyo, Sendeka, naye alitaka kifungu hicho kifanyiwe marekebisho na kupitishwa upya ili kuondoa mgongano kisheria kama ilivyoshauriwa na Jaji Werema. 
Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, alipigilia msumari wa mwisho, akisema kifungu cha 54 (4) kinazungumzia kwamba hairuhusiwi kubadilisha maamuzi ya bunge hakihusiani na suala hilo, kwani bunge lilishafanya uamuzi, lakini Mwenyekiti akatoa uamuzi wake hivyo marekebisho hayo ni batili.
Baada ya hapo Werema alisimama na kufafanua kuwa kama uamuzi uliofaanyika una makosa, kanuni ya 24 inaruhusu kufanyika marekebisho na kwamba serikali inaandaa marekesho hayo ili kifungu hicho kirudishwe bungeni na kufanyiwa maarekebisha na kupitishwa upya.
Akitoa uamuzi wake baada ya kusikiliza hoja za wabunge, Ndugai, aliagiza suala hilo lipelekwe kwenye Kamati ya Kanuni za Bunge kwa ajili ya kushughulikiwa kwa kina kabla ya kurudishwa tena bungeni.
CHANZO: NIPASHE

No comments: