ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 2, 2012

Mbinu za kumwacha mpenzi wako bila ya kumuumiza-2

MPENZI msomaji wangu, wewe utakuwa ni shahidi kwamba, inauma sana kuachwa hasa na mtu uliyetokea kumpenda na kuamini mtakuwa pamoja hadi mwisho wa maisha yenu. 
Hata hivyo, kila siku wanandoa na wapenzi wanaachana kwa sababu mbalimbali lakini kuna njia ambazo unaweza kuzitumia kumuacha mpenzi wako bila kumuumiza. Ndiyo maana wiki iliyopita nilianza kuzungumzia mada hii na leo nitaimalizia ili wiki ijayo nianze nyingine. 

Kama nilivyosema awali, kila siku watu wanaingia kwenye uhusiano mpya lakini pia wengine wanaachana. Sababu za kuachana kwa wapenzi zinatofautiana ila kikubwa ni kwamba unapoachana na mtu ambaye mlikuwa ‘mwili mmoja’ hutakiwi kumgeuza adui yako kwa asilimia zote, hata kama kakukosea vipi.
Kwa mfano, yawezekana ulitokea kumpenda na kuhisi angeweza kuwa wako wa maisha lakini kadiri siku zinavyokwenda unabaini si mtu sahihi kwako. Katika mazingira hayo suala la kumuacha haliepukiki ila cha kujiuliza ni kwamba utamuachaje?

Je, itakuwa ni sahihi kumuambia laivu kwamba mimi na wewe basi? Inawezekana ukafanya hivyo ila wataalam wa mapenzi hawashauri kwani wanajua madhara ya kutumia mbinu kama hiyo na ndiyo maana wakashauri kutumia njia ambazo zinaweza kusaidia ukamuacha lakini bila kumuumiza na maisha yakaendelea kuwepo.

Jitoe taratibu
Chukulia kwamba umekuwa naye kwa muda mrefu kidogo ukiwa na malengo ya kuingia naye kwenye ndoa lakini katika utafiti wako ukabaini hakufai, unashauriwa kujitoa kwake kimyakimya. Unachotakiwa katika mbinu hii ni kupunguza kumtendea mambo ya kiupendo.
Kwa mfano, unaweza kupunguza kuonana naye, kumpigia simu, kumtumia sms na hata kumsaidia kifedha kama ulikuwa ukifanya hivyo. Kwa kufanya hayo ni lazima ataanza kuona tofauti na kuhisi penzi linaelekea ukingoni.
Aidha, kwa kumfanyia hivyo ni lazima atahoji juu ya mabadiliko hayo. Wewe hutakiwi kutoa maelezo yoyote zaidi ya kuendelea kuyeyusha bila kumwambia wazi kwamba umemtoa moyoni mwako.
Kama huyo mpenzi wako ni mwelewa atagundua kuwa, ndiyo unamuacha kimtindo na yeye ataanza kujiandaa kukukosa, hata pale utakapokata mawasiliano moja kwa moja atakuwa ameshajua kuwa umemuacha hata bila kumueleza.
Ukigundua ameshafahamu kuwa umemuacha, hapo unaweza kumwambia kwa kifupi kwamba umeamua bora kila mmoja aendelee na maisha yake. Kisaikolojia utakuwa hujamuumiza sana lakini tayari utakuwa umemuacha.

Maneno ya busara
Unaweza kumuacha mpenzi wako kwa kutumia lugha ambayo yeye mwenyewe atahisi hukuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima umuache. Mfano: ‘Ashura, kusema ukweli nilikupenda sana na mpaka sasa naamini wewe ni mwanamke wa maisha yangu, sikuamini kama yupo mwanamke mwingine wa kunipa furaha kama wewe lakini kwa hili lililotokea sina jinsi, inabidi nikuache. Utaendelea kuwa rafiki yangu na kama ni kukusaidia nitakusaidia kama rafiki na si mpenzi.”
Hayo ni maneno ambayo mwanaume anamwambia mpenzi wake akimaanisha anamuacha lakini ukiyachunguza utabaini hayachomi sana kwa kuwa anayeachwa bado anapewa nafasi nyingine ya urafiki wa karibu na si mapenzi tena.
Mimi nikushauri tu kwamba, hakikisha unapotaka kuachana na mtu ambaye mmekuwa pamoja kwa muda mrefu unakuwa makini. Hata kama amekukosea vipi lakini busara itumike hasa kwa kuzingatia yale mazuri ambayo aliwahi kukufanyia huko nyuma.

www.globalpublishers.info

No comments: