ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 2, 2012

Simba yaua Oljoro, Boban ala nyekundu

JKT RUVU                                                  SIMBA SPORTS CLUB
Mchezaji aliyeingia kutokea benchi, Emmanuel Okwi, alifunika mapungufu ya Simba kubaki 10 uwanjani kwa kufunga magoli mawili yaliyowapa Wekundu wa Msimbazi ushindi wa 2-0 dhidi ya wageni wa ligi kuu JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.
Kiungo mtata Haruna Moshi 'Boban' alitolewa na refa Isihaka Shirikisho wa Tanga kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja katika dakika ya 42 baada ya kumpiga kiwiko mchezaji wa Oljoro, Kalage Mgunda. Boban alionekana kufanya kitendo hicho kama kulipiza kisasi baada ya kufanyiwa madhambi na mchezaji wa Oljoro.

Nyota wa kimataifa wa Uganda, Okwi aliyeingia katika dakika ya 46 kuchukua nafasi ya mshambuliaji Gervais Kago, aliifungia Simba goli la kuongoza katika dakika ya 59 akimalizia kazi nzuri iliyofanywa kwa ushirikiano wa viungo Uhuru Selemani na Mwinyi Kazimoto.


Simba licha ya kuwa pungufu uwanjani walipata goli la pili dakika saba kabla ya mchezo kumalizika wakati Okwi tena alipotumbukiza mpira wavuni kufuatia pasi fupi ya Uhuru ambaye, dakika chache zilizopita angeweza kuipa Simba goli kama asingepaisha mpira akiwa amebaki na nyavu.    


Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha pointi 34, tatu juu ya mabingwa Yanga walio katika nafasi ya pili baada ya mechi 15. Azam ni ya tatu ikiwa na pointi 29 na Ojoro imebaki katika nafasi ya nne kwa kuwa na pointi 26.
Magoli mawili ya jana yamemfanya Okwi kufikisha mabao 7, huku orodha ya wafungaji ikiongozwa na John Bocco wa Azam mwenye magoli 10 anayefuatiwa na Keneth Asamoah wa Yanga aliyefunga mabao 9.
Katika mechi nyingine ya jana, African Lyon iliifunga Polisi Dodoma 2-0 kwenye Uwanja wa Chamazi.


Sammy Kessy aliipatia Lyon goli la kwanza katika dakika ya 30 baada ya kuwapiga chenga mabeki wa Polisi na kupiga shuti lililomshinda kipa Gerald Mwingira na Sunday Juma akaongeza la pili katika dakika ya 76 kufuatia kazi nzuri ya Sino Augustino na Samwel Ngassa. Ushindi huo umeifanya Lyon kufikisha pointi 18.      


Kulikuwa na kosa kosa kadhaa tangu mapema kwenye Uwanja wa Taifa na beki wa Simba, Nassoro Said 'Chollo' alikuwa ngangari akidhibiti mashambulizi ya timu yake hiyo ya zamani ya Oljoro aliyoihama mwanzoni mwa msimu huu wakati ilipopanda daraja kwa mara ya kwanza na kutua Msimbazi.
Uhuru Selemani wa Simba alipiga pembeni shuti katika dakika ya 52 na kipa wa Simba, Juma Kaseja aliwanyima wageni goli kwa kupangua kiufundi shuti la Bakari Kigodeko wa Oljoro.
Kigodeko alipoteza nafasi nzuri ya kuisawazishia timu yake katika dakika ya 72 pale aliposhindwa kufunga wakati kipa Kaseja akiwa ametoka langoni huku mabeki wa Simba, Kelvin Yondani na Shomari Kapombe wakigongana katika harakati za kuokoa.
Vikosi kwenye Uwanja wa Taifa vilikuwa; Simba: Juma Kaseja, Amir Maftah, Shomary Kapombe, Kevin Yondani, Jonas Gerald, Mwinyi Kazimoto, Patrick Mafisango, Gervais Kago/Emmanuel Okwi (dk. 46), Haruna Moshi 'Boban' na Uhuru Suleiman/ Ramadhani Singano (dk. 89).
JKT Oljoro: Said Lubawa, Omary Hamis, Ali Omary, Omar Mtaki, Marcul Ndeheli, Kalage Mgunda/ Meshack Nyambele (dk. 50), Allykhan Mkanga, Sunday Paul, Bakari Kigodeko, Amir Omary/ Paul Nonga (dk. 57), Rashid Nassoro.
CHANZO: NIPASHE

No comments: