Timu ya taifa ya Zambia kesho itajaribu kuandika historia mpya ya soka Barani Afrika kwa kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika, itakapokabiliana na Ivory Coast katika mchezo wa fainali.
Zambia hadi kufika fainali, imepita vikwazo vingi na kubwa zaidi kukiangusha kigogo cha mashindano hayo, Ghana kwenye mechi ya nusu fainali.
Mafanikio ya majirani zetu wa Zambia hatuna budi kuyapongeza, lakini kwa upande mwingine iwe changamoto ya Tanzania kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa.
Timu zetu hazijafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa kwa ngazi ya klabu na kuwa wasindikizaji katika kombe la Shirikisho na klabu Bingwa Afrika.
Wawakilishi hao wa ngazi ya klabu kimataifa, wanatokana na timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara na Visiwani, ambayo kimsingi ndizo hutoa wachezaji wengi wa timu ya taifa.
Kufuatia hali hiyo kuna haja ya kuiboresha Ligi kuu kwa wadhamini kuziwezesha kifedha timu zinazoshiriki ligi hiyo ili ziweze kufanya usajili wa uhakika na kuhudumia wachezaji ipasavyo.
Timu hizi zikiwezeshwa kifedha zinaweza kutoa ushindani mkubwa zenyewe kwa zenyewe na hivyo kupanda kiwango cha soka cha wachezaji wa timu zetu.
Kwa upande mwingine ushindi wa Zambia wa kuingia fainali unatuachia somo kubwa Watanzania kufanya mabadiliko makubwa ya mfumo wa uendeshaji soka kuanzia chini ili kuwepo na wachezaji walioiva na kufundishika watakapofikia hatua ya kukomaa na kucheza mechi za kimataifa.
Ligi zetu ziendeshwe kwa mtazamo wa kujenga misingi imara ya kuwa na wachezaji watakaokuwa na uwezo wa kushindana na wenzao, kama ilivyokuwa katika miaka ya zamani.
Soka la Tanzania linatakiwa libadilike kuanzia shule za msingi, timu za Vijana, Ligi za Taifa za TFF , Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Kuu Tanzania Bara ili tuweze kutoa wachezaji watakaokuwa na ubora wa kimataifa.
Bila ya kufanya mabadiliko katika mfumo wa soka letu, kufanya vizuri katika mechi za kimataifa itakuwa ni ndoto kutokana na kutegemea wachezaji ambao hawajajengeka kutoa ushindani wa kimataifa wanapokutana na wenzao wa mataifa yaliyo juu katika soka au yanayopanda kiwango.
TFF na wadau wa soka ni wakati muafaka wa kuwa na wivu wa kimaendeleo kuwaona jirani zetu Zambia waking’ara Barani Afrika na Tanzania ikiendelea kuwa katika orodha ya timu za chini.
Mikakati endelevu ya kuinua soka la Tanzania ianze sasa na washika dau la kuongoza mchezo huo wabadilike ili heshima ya nchi katika soka irudi.
Soka la Tanzania halijawahi kupatwa na majanga makubwa tofauti na Zambia ambayo mwaka 1993, ilipatwa na pigo kubwa kutokana na wachezaji wake wote wa timu ya Taifa kufariki katika ajali ya ndege wakiwa njiani kulekea Gabon.
Baada ya pigo hilo Zambia imejipanga na kujenga upya soka lake na matunda yake ndiyo haya yanaonekana ikiwa ni miaka 19 tangu kutokea ajali ile ya kusikitisha inafika fainali za Mataifa ya Afrika.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment