ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 20, 2012

Viongozi wazidi kuikimbia CUF

Profesa Ibrahim Lipumba



Jinamizi la kufukuzwa uanachama Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohammed, na wenzake 10, limezidi kukitafuna Chama cha Wananchi (CUF), baada ya viongozi watatu waandamizi Taifa, kutangaza kujitoa katika chama hicho, huku wakimshauri pia Mwenyekiti wao, Profesa Ibrahim Lipumba, kufuata nyayo zao ili kulinda heshima na hadhi aliyonayo kitaifa na kimataifa.
Waliotangaza uamuzi huo ni Abubakar Rakesh ambaye ni mtu wa karibu na swahiba mkubwa wa Profesa Lipumba; aliyewahi kuwania ubunge kwa tiketi ya CUF Jimbo la Mwanga, mkoani Kilimanjaro, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Juma Kilaghai. Wote ni wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi wa CUF Taifa; na Mkurugenzi wa Sekretarieti ya Vijana wa Chama hicho Taifa, Omar Constantine.

Walitangaza uamuzi wao huo jana walipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mwezi mmoja tangu Baraza Kuu la Uongozi wa CUF Taifa, litangaze  kuwavua uanachama wa chama hicho Hamad na wenzake, uamuzi ambao wameupinga Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Akitangaza uamuzi huo kwa niaba ya wenzake jana, Rakesh alisema pamoja na mambo mengine, umetokana na kuchoshwa na kile alichokiita Umungu-mtu aliojipachika Katibu Mkuu wa CUF, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, katika chama hicho.
Rakesh alimshauri Profesa Lipumba kutoendelea kuwapo ndani ya CUF akisema kufanya hivyo kunaweza kusababisha apoteze heshima na hadhi aliyonayo kitaifa na kimataifa.
“Simshauri Profesa Lipumba kuendelea kwenye CUF. Namshauri kwamba ndani ya CUF atapoteza heshima yake. Hivyo, akija (kutoka Marekani) awaite waandishi wa habari kama hivi, kisha atangaze kujitoa CUF,” alisema Rakesh.
Alisema Maalim Seif amekuwa Mungu-mtu ndani ya CUF katika maamuzi ndani ya chama hicho hata kama ya kukinyonga chama na kwamba, hataki kuona maendeleo ya chama hicho yakipatikana, hasa upande wa Tanzania Bara.
Rakesh alisema zaidi ya hivyo, anao ushahidi madhubuti kwamba, ndani ya CUF kuna mtu aliyepandikizwa ili kufanya kazi mahsusi ya kukiua chama hicho kwa maslahi binafsi.
Alisema mtu huyo amepewa maelekezo kufanya kila liwezekanalo, ikiwamo kutengeneza migogoro ili ifikapo Juni, mwaka huu, awe amehakikisha CUF inakufa, hasa upande wa Tanzania Bara.
“Na mkimtafuta huyo mtu mtampata. Ni bingwa sana wa migogoro,” alisema Rakesh.
Alisema mtu huyo ambaye ni katika viongozi wakuu wa CUF amekuwa akichochea na kuendekeza migogoro tangu alipokuwa akisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Rakesh alisema kutokana na CUF kuwa katika hali mbaya kutokana na fitina za baadhi ya viongozi wake wakuu, hivi sasa wilaya zaidi ya 250 Tanzania Bara zimetelekezwa kwa kukosa uongozi.
“Hivyo, tumeona tutoke mapema (katika CUF)…Tunajivua nyadhifa zetu na kukihama chama,” alisema Rakesh na kuongeza kuwa baada ya kutangaza uamuzi huo hatua inayofuata itakuwa ni kumuandikia barua Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Lipumba, kumuarifu kuhusu uamuzi wao huo.
Alisema sababu nyingine iliyowafanya kufikia uamuzi huo, ni kesi iliyofunguliwa na Hamad na wenzake kupinga kuvuliwa uanachama.
Rakesh alisema kesi hiyo ni mbaya, hivyo wanaogopa kufungwa jela.
Katika kesi hiyo, Hamad na wenzake walifungua maombi madogo mahakamani wakiiomba mahakama pamoja na mambo mengine iwaite wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi wa CUF, akiwamo Maalim Seif, wajieleza kwanini wasifungwe jela.


Hamad na wenzake wanataka wajumbe wa baraza hilo wajieleze hivyo, kwa madai ya kukiuka amri halali ya mahakama iliyowazuia kuendelea na mkutano wa Baraza hilo, ambao ulitumiwa kuwavua uanachama katika chama hicho.  




Rakesh alisema uamuzi wa kujitoa CUF hauna ushawishi wowote wa Hamad, bali wanachokifanya ni kusimama katika haki na ukweli.
Alisema sababu zote walizozitaja zilizowafanya wafikie uamuzi huo, aliwahi kuzizungumza pia katika vikao vya chama.
Pia alisema hana tabia ya kupindisha ukweli, hivyo wakati wowote akiitwa mahakamani katika kesi ya Hamad na wenzake kwenda kuueleza anachokijua kuhusu mvutano uliopo unaohusu amri ya mahakama iliyozuia mkutano ule wa Baraza Kuu kufanyika, kama CUF waliipata amri hiyo mapema au hawakuipata kabisa, atakuwa tayari kwenda kutoa ushahidi alionao.
Kwa upande wake, Constantine alisema miongoni mwa mambo yaliyomfanya afikie uamuzi wa kujitoa CUF, ni kauli ya ubaguzi wenye misingi ya dini, Ubara na Uzanzibar aliyodai kuwa ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Tanzania Bara, Ismail Jussa Ladhu.
Alidai kauli hiyo ilitolewa na Jussa kufuatia matokeo mabaya iliyoyapata CUF katika uchaguzi mdogo wa uwakilishi katika Jimbo la Uzini, hivi karibuni.
Constantine alisema baada ya CUF kushika nafasi ya tatu katika uchaguzi huo, Jussa ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mjimkongwe, alikaririwa akisema kilichosababisha matokeo hayo kwa CUF, ni wingi wa wananchi wa Tanzania Bara na Wakristo, waliopo katika jimbo hilo.
Alisema kauli hiyo ya Jussa inapingana dhahiri na madhumuni ya CUF namba moja yanayopinga kauli na matendo ya ubaguzi kufanywa na mwanachama yoyote wa CUF kwa misingi yoyote nchini.
“Kauli hiyo ya Jussa inathibitisha kwamba, mahali ambako kuna wananchi kutoka Tanzania Bara na Wakristo hakuna CUF. Huu ni ubaguzi mkubwa usioweza kuvumilika,” alisema Constantine.
Naye Kilaghai alisema wanaCUF hawana sababu ya kumtafuta mchawi kwingine, bali wajue kwamba, anayeibomoa CUF ni Maalim Seif na Kamati Tendaji ya Chama hicho Taifa.
Alisema matokeo iliyoyavuna CUF kwenye uchaguzi mdogo wa uwakilishi katika jimbo la Uzini, ni uthibitisho tosha kwamba, Wazanzibari wameanza kuona ubaya wanaofanyiwa na Maalim Seif na kamati hiyo ambayo ni chombo cha juu cha maamuzi katika chama hicho.
Kilaghai alisema CUF imepoteza mwelekeo na kwamba, ushahidi wa hilo ni kauli za kukinzana ambazo katika siku za hivi karibuni zimekuwa zikitolewa hadharani na viongozi wake wakuu.
Kutokana na hilo, aliwataka wanaCUF waliobaki kuhakikisha wanakiokoa chama chao kutoka katika makucha ya wote waliobainika kuwa na njama za kukiua chama hicho.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Buriani CCM B