
Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama
KATIBU Mkuu wa CCM, Wilson Mukama amesema chama chake hakikushindwa na Chadema katika Uchaguzi Mdogo wa Arumeru Mashariki kutokana na makundi.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Aprili Mosi, mwaka huu mgombea wa chama hicho, Sioi Sumari alishindwa na Joshua Nassari hivyo CCM kupoteza jimbo hilo ililokuwa ikilishikilia hadi aliyekuwa mbunge wake, Jeremia Sumari alipofariki dunia Januari, mwaka huu.
Baada ya matokeo ya uchaguzi huo, baadhi ya wadau wa siasa walihusisha kushindwa huko na makundi ndani ya chama hicho kikongwe Afrika ambayo yamekuwa yakielezwa kubeba ajenda ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Alisema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari katika Ofisi Ndogo za CCM, Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam baada ya kuulizwa juu ya madai kwamba Sioi alitelekezwa na viongozi wa chama hicho Wilaya ya Arumeru na Mkoa wa Arusha ikidaiwa kuwa hakuwa chaguo lao wakati wa kura za maoni.
Mukama alisema: “Kuwa na makundi ni kitu cha kawaida lakini si la mtu fulani, bali ni katika chama ili vitu viende na ni jambo jema katika chama. Kwa mfano, mambo ya urais kikanda Kusini wameshapata, sasa inaweza ikawa Nyanda za Juu Kusini au Kanda ya Kati na upande wa Kaskazini vilevile, juu kule Mwalimu Nyerere alishatoka.”
Alisema hali kama hiyo ndiyo inatengeneza makundi kwa watu wa sehemu fulani kusema: “Mbona kule ameshatoka huku bado hajatoka. Hayo ndiyo mambo yalivyo na si mtu mmoja mmoja kuwa na kundi, hayo yanayosemwa huko siyajui.”
Hata hivyo, alisema tamko la chama kuhusu uchaguzi huo limeshatolewa na Katibu wake wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Baada ya matokeo hayo, Nape alitoa taarifa kwenye vyombo vya habari akikipongeza Chadema kwa ushindi huo na kukitaka kitekeleze ahadi zake kilichotoa kwa wananchi wa jimbo hilo.
Mwanzoni mwa wiki hii, mmoja wa wajumbe wa timu ya kampeni za Sioi anayetoka wilayani Arumeru alisema mgombea huyo alitengwa akitoa mfano wa siku ya kupigakura ambayo hakuna kiongozi yeyote aliyehangaika kuzunguka vituoni kukagua zoezi hilo.
Alisema hali ilikuwa mbaya zaidi ilipofika wakati wa kukusanya masanduku ya kura na matokeo kutoka vituoni kabla majumuisho yaliyofanyika katika Ofisi ya Mji Mdogo wa Usa-River, ambako hakukuwa na kiongozi yeyote aliyejitokeza kusimamia wala kushuhudia majumuisho hayo.
“Huwezi kuamini kuwa hakukuwa na kiongozi wala mwakilishi yeyote wa CCM kwenye chumba cha majumuisho ya kura hadi ilipofika saa 7:00 usiku ndipo mgombea mwenyewe alipoamua kwenda kushuhudia na kusimamia kura zake,” alisema mjumbe huyo ambaye ni kiongozi wa ngazi ya mkoa.
Inadaiwa kwamba wanachama wengi waliokuwa wamejitokeza kugombea na kushindwa katika kura za maoni za chama hicho, hawakuvunja kambi zao.
Pia siasa za makundi ndani ya CCM Mkoa wa Arusha, ambako bado vigogo wa chama hicho, Katibu wa Mkoa, Mary Chatanda na Mwenyekiti wake, Onesmo Nangole hawana uhusiano mazuri kunaelezwa kuwa ni moja ya sababu za kuanguka.
Awali, Chatanda ambaye anadaiwa kuwa na mgogoro na wana-CCM wengine wa Arusha, alitajwa kumpinga waziwazi Sioi katika kura za maoni na alitupa karata yake kwa William Sarakikya na Elishilia Kaaya ambao wote walishindwa.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment