ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 7, 2012

Mawaziri mguu sawa



WAKATI mawaziri wapya na waliobadilishwa wizara wakitarajiwa kuapishwa leo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema amesema uteuzi wa Rais Jakaya Kikwete wa wabunge watatu kuwa mawaziri kabla ya kula kiapo bungeni, ni sahihi wala hajavunja Katiba ya nchi. 

Jaji Werema ametoa ufafanuzi huo siku moja baada ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha 
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kudai kwamba Rais amevunja Katiba 
kwa kuwateua wabunge hao kuwa mawaziri kabla ya kuapishwa bungeni. 


Akiwa Arusha juzi, Mbowe alidai kuwa Rais Kikwete amevunja Katiba ya Tanzania kwa kuteua mawaziri ambao amewateua ubunge ndani ya saa moja, na pia kudai amevunja Katiba baada ya kuteua baadhi ya Wizara zisizo za Muungano, kwa kuwapatia mawaziri wa Zanzibar, jambo ambalo ni kosa kubwa kikatiba. 

Mwishoni mwa wiki, Rais Kikwete aliwateua wabunge wanne wapya ambao ni Profesa Sospeter 
Muhongo, Janet Mbene, Saada Mkuya Salum na James Mbatia. 

Kati ya hao, Profesa Muhongo, Mbene na Saada wameukwaa uwaziri baada ya Profesa Muhongo kuteuliwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati wanawake hao wawili wanakuwa naibu mawaziri wa Fedha. 

Katika taarifa yake jana kwa vyombo vya habari, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisisitiza kwamba wabunge ambao hawajaapishwa ndani ya Bunge ni wabunge na wanapoteuliwa kushika nafasi ya Uwaziri au Naibu Waziri ni halali kwa kuwa uteuzi huo haukiuki masharti yoyote ya Kikatiba au Sheria. 

Aidha, alisema Katiba ya Nchi haiweki kwa Rais masharti kwamba kabla ya kumteua Mbunge wa aina hiyo (wa kuteuliwa na Rais) kuwa Waziri au Naibu Waziri Mbunge huyo, awe ameapishwa Bungeni kwanza. 

“Msingi wa Katiba tunaoanza nao ni maelekezo ya masharti yaliyomo kwenye Ibara ya 55(4) kwamba: “Mawaziri na Naibu Mawaziri wote watateuliwa kutoka miongoni mwa Wabunge.” Pili, ni mamlaka ya Rais ya uteuzi wa Wabunge aliyopewa na masharti ya Ibara ya 66(1)(e) 
yenye aina ya Wabunge wasiozidi kumi watakaoteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa zilizotajwa katika aya za (a) na (c) za ibara ya 67 na angalau Wabunge watano kati yao wakiwa Wanawake. 

“Wabunge aliowateua Mheshimiwa Rais wanatokana na Ibara hii,” alieleza Jaji Werema na kuongeza: “Tatu, baada ya hatua zote hizi ikumbukwe kwamba aliyeteuliwa au kuchaguliwa kuwa Mbunge anakuwa Mbunge ama baada ya kutangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi; au baada ya kuteuliwa na Tume ya Uchaguzi kwa wale Wabunge wa Viti Maalumu au 
anapochaguliwa na Baraza la Wawakilishi au anapoteuliwa na Rais akitumia Mamlaka yake ya uteuzi yanayotokana na Ibara ya 66(1)(e). 

“Hivyo Wabunge wanaohusika hawahitaji kuapishwa kwanza Bungeni ili wawe Wabunge. Kiapo cha Mbunge Bungeni kinamwezesha tu kushiriki katika shughuli za Bunge.” Alisema Katiba ya nchi haiweki kwa Rais masharti kwamba kabla ya kumteua Mbunge wa aina hiyo kuwa Waziri au Naibu Waziri Mbunge huyo, awe ameapishwa Bungeni kwanza. 

“Masharti mawili muhimu na ya kuzingatia ni kwamba mteule wa nafasi ya uwaziri au Naibu Waziri hatashika madaraka yake ila mpaka kwa mujibu wa Ibara ya 56 ya Katiba, awe ameapa kwanza mbele ya Rais kiapo cha uaminifu na pia kiapo kingine chochote kinachohusika na utendaji wa kazi yake kitakachowekwa kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge. 

“Sharti la pili, litahusu kiapo cha Uaminifu katika Bunge kabla Mbunge hajaanza kushiriki katika shughuli za Bunge kwa masharti ya Ibara ya 68 ya Katiba. Viapo hivyo havitegemeani na vinaweza kufanyika kwa nyakati tofauti,” alifafanua Mwanasheria Mkuu wa Serikali. 

“Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inasisitiza kwamba Wabunge ambao hawajaapishwa ndani ya Bunge ni Wabunge na wanapoteuliwa kushika nafasi ya Uwaziri au Naibu Waziri ni halali kwa kuwa uteuzi huo haukiuki masharti yoyote ya Kikatiba au Sheria. 

“Aidha, katika kutekeleza madaraka ya kazi ya Uwaziri au Naibu Waziri Mbunge atahitaji kiapo 
mbele ya Rais hata kama hajaapishwa Bungeni. Busara ya uandishi wa Katiba na Sheria imetambua kwamba kunaweza kukatokea uteuzi wa aina hiyo wakati Bunge limeahirishwa 
kama ilivyo sasa. 

Masharti ya Ibara ya 68 ya Katiba yatazingatiwa katika kikao cha Bunge kijacho,” alieleza zaidi Jaji Werema. 

Aidha, Baraza jipya la Mawaziri lililosukwa upya na Rais Jakaya Kikwete, linaanza kazi leo baada ya kuwaapisha mawaziri na naibu mawaziri wapya. 

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, mawaziri wanane wa zamani walioteuliwa kuongoza wizara nyingine, mawaziri saba wapya, naibu mawaziri sita waliobadilishwa wizara na naibu mawaziri 10 wapya ndio watakaoapishwa. 

Mawaziri hao wanane wa zamani walioteuliwa kuongoza wizara nyingine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (Utawala Bora), George Mkuchika, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga 
Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Ali Mwinyi. 

Wengine ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani na Waziri Nchi Ofisi ya Rais asiyekuwa na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya. 

Mkuchika katika baraza lililopita alikuwa Waziri wa Tamisemi, Ghasia (Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Nahodha (Mambo ya Ndani ya Nchi), Dk. Mwinyi 
(Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Chikawe (Ofisi ya Rais, Utawala Bora), Nchimbi (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo), Profesa Maghembe (Kilimo, Chakula na Ushirika), Kombani (Katiba na Sheria) na Profesa Mwandosya (Maji). 

Aidha, watakaopishwa leo pia ni mawaziri saba wapya ambao ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki. 

Mawaziri wengine wapya ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo. 

Kabla ya uteuzi huo, Chiza alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Dk. Mwakyembe Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Mukangara, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Balozi Kagasheki alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi 
na Dk. Kigoda alikuwa Mbunge wa Handeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi. 

Pia naibu mawaziri sita waliobadilishwa wizara watakaoapishwa leo ni Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima aliyekuwa Nishati na Madini, Naibu Waziri wa Mambo ya 
Ndani ya Nchi Pereira Silima aliyekuwa Fedha na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Gregory Teu ambaye pia alikuwa Fedha. 

Naibu mawaziri wengine waliobadilishwa wizara ni Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais 
Charles Kitwanga aliyekuwa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu aliyekuwa Viwanda na Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge aliyekuwa Maji. 

Aidha, manaibu mawaziri 10 wapya watakaoapishwa ni Dk. Seif Suleiman Rashid (Afya na Ustawi wa Jamii), George Simbachawene (Nishati na Madini), January Makamba (Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia) na Dk. Charles Tizeba (Uchukuzi). 

Wengine ni Amos Makala (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo), Dk. Binilith Mahenge 
(Maji), Stephen Maselle (Nishati na Madini), Angela Kairuki (Katiba na Sheria), na wawili wa Fedha, Mbene na Saada. 

Rais Kikwete alitangaza baraza hilo jipya Ijumaa iliyopita akiwatema mawaziri sita ambao ni 
aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Omary Nundu (Uchukuzi), Dk. Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii) na Dk. Cyril Chami (Viwanda na Biashara. 

Wengine ni Mustafa Mkulo (Fedha), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii) na kwa upande wa naibu 
mawaziri ni Athumani Mfutakamba (Uchukuzi) na Dk. Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii). 

Mabadiliko ya baraza hilo yanatokana na kashfa ya ubadhirifu wa mali ya umma iliyoibuliwa katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, ambapo wabunge na baadhi ya wananchi walitaka wahusika wote wakiwamo mawaziri wa sekta husika wachukuliwe hatua.


Habari leo

1 comment:

Anonymous said...

Only in Tanzania stuff like this happens.