ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 15, 2012

Vumilia, endelea kuwa ‘singo’ kuliko mpenzi pasua kichwa-4


MATHALAN, mpenzi wako anakuwa na urafiki na watu mpaka anafikiriwa anatembea nao. Hii ni tabia mbaya na haikubaliki, ingawa wapo wazuri wa kutetea. Watasema, sisi ni washkaji ila fahamu mapenzi yenu yanazikutanisha familia mbili. Una ndugu, marafiki, wazazi.
IInakuaje mpenzi wako anahisiwa anatoka na mwanamke mwingine na taarifa zinafika mpaka kwa wazazi wako? Watajua mkwe wao ni kicheche na hilo litakugharimu kwa kiasi kikubwa. Unatakiwa kulinda thamani, heshima na utu wako, kwahiyo achana na mtu asiyejua maana!

Unaweza kuona leo inakuuma kwa sababu unaepukana na mtu ambaye unampenda lakini hiyo ni nafuu kwako kesho. Amini kwamba mwisho wa mateso hayo ya moyo ni furaha kubwa, mwisho utajiuliza: Ni kipi kilichokuwa kinakufanya uumie kwa muda wote? Upo huru sasa!
Mapenzi maana yake utulivu wa moyo, yaani wewe na mtu wako spesho muogelee katika dimbwi maalum, ninyi wote mkiwa na amani. Mkishirikiana katika hali zote. Inakuwa hakuna anayewaza la kwake peke yake isipokuwa kwa ajili yenu.
Ukilia anakuwa wa kwanza kukubembeleza, anapogundua amekuudhi ni mwepesi kukuomba msamaha. Anasoma mabadiliko yako na kukuuliza kile kinachokusumbua. Anaficha siri zako, anazungumza lugha tamu na hisia zake zote zipo kwako. Kwa wengine haoni hatamani.
USITHUBUTU KULAZIMISHA PENZI
Yamewafika wengi na wameumia, kwahiyo ni vizuri kuwa makini. Utauguza donda la moyo lisiloweza kutibika, utakonda wenzako watakucheka, atakugeuza punda afanye anachokitaka. Ni kazi bure kumpenda mtu asiyekupenda.
Pamoja na maumivu unayoweza kuyapata lakini kuna vitu hivi lazima vikukute kwa huyo mwenzi wako wa kulazimisha.
ATAKUTESA KWA UBINAFSI WAKE
Hana mapenzi ya kweli na wewe, kwahiyo si kila wakati atakufikiria. Kama hamjawa kwenye ndoa itakusumbua kwa sababu ni ngumu kufikiria kwa ajili yenu, isipokuwa atawaza kwa matilaba yake. Kama kuoana, utalazimisha wewe lakini yeye hatokuwa na habari.
Mkiwa kwenye ndoa, hatojisikia fahari kutoka na wewe atalazimisha maisha ya kila mmoja kuwa huru kufanya mambo yake. Nguo atanunua za kwake na hata siku moja hutoona amekununulia. Wewe utafanya mengi kwa ajili yake lakini yeye atabaki na ubinafsi wake. Atakutesa, pasha moto ubongo!
AKIONA WENGINE ATAHISI NI WAZURI ZAIDI YAKO!
Mtu huishi kwa fikra zake, kwahiyo kwa sababu hakupendi kwa moyo wake wote inakuwa ngumu kukukubali, hivyo anapokutana na watu wengine barabarani atadhani ni wazuri kuliko wewe. Atababaika hata mbele yako.
Unahitaji heshima ya kiwango bora na kwa kawaida mpenzi wako anapaswa kukuona wewe ni mtu namba moja. Kama hakupi nafasi hiyo maana yake anapenda nusunusu au hapendi kabisa. Usikaribishe mateso, fikiria kesho, chukua uamuzi leo.
HASIFU MUONEKANO WAKO, ANA LAKE KICHWANI!
Hujiulizi, kila siku anakuona na hakusifii! Ni wazi kuwa hata kama wewe ni mzuri kiasi gani, unavaa na kupendeza kwa namna bora kabisa lakini mwenzi wako hawezi kukupa pongezi kwa sababu ana lake kichwani.
Ukiona hilo ujue kwamba yupo mtu ambaye anamsifu kwa sababu ndiye anayemkubali, na wewe utasifiwa na wengine. Inauma mwenzi wako kukuacha nyumbani na kwenda kumwaga sifa pembeni, wakati na wewe unazihitaji. Una thamani kubwa, pigania utulivu wa moyo wako!

www.globalpublishers.info

1 comment:

Anonymous said...

kweli kabisa..asilimia 100..kimbia bila kuangalia nyuma...maana ataupende vipi ukatoa na roho yako nje kumuonyesha jinsi unavyompenda ktk shida na raha...ndio kwanza atakunyanyasa na kukuita majina...mbaya zaidi umefanikiwa kujua ukweli ulio jificha kwa miaka kadhaa kama anampenzi mwingine pembeni ambaye ametokanae mbali.