ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 16, 2012

Mapenzi ni fursa, iheshimu kwa maana haiji mara mbili-4

Na Luqman Maloto
Mada hii ikufumbue macho kwamba mapenzi ni fersa na mara nyingi haiji mara mbili, hivyo kuwa na heshima kwa mwenzi wako. Bado tunao mfano wa mapenzi ya Shania na Shadrack, hapa inakupa picha jinsi mrembo huyo alivyo macho-juu lakini huwezi kuamini, hivi sasa anajuta, ni balaa. Endelea…
Shadrack alipofika chuo kikuu, alipata ajira ya muda, hivyo akawa anapanga muda wa kazi na masomo. Asubuhi anakwenda kazini, jioni chuo. Kazini malipo yalikuwa si haba, hivyo kwa kipato, alimshinda yule mfanyakazi wa ofisi ya mkuu mkoa. Shania kuona hivyo akarudi tena kwa Shadrack.

Mapenzi yakaendelea. Shadrack alijifanya kusahau yaliyopita lakini kila kitu kilikuwa akilini mwake. Alishajua kwamba Shania si mtu mwenye mapenzi ya kweli kwake, ila humfuata pale anapoona mambo ni mazuri. Japo alikuwa na kinyongo, safari hii Shadrack alijitahidi kuonesha mapenzi makubwa kuliko mwanzo.
Alijitahidi kumjali zaidi, akahakikisha anatimiza kila hitaji la Shania. Siku za mwanzoni Shania alijitahidi kumuonesha Shadrack mapenzi ya kweli lakini kadiri muda ulivyosogea, ndivyo ilivyothibitika kuwa mja asili hasahau asili yake. Shania alianza kumtesa kihisia mwenzake, Shadrack akawa mtu wa kulalamika.
Wakati Shadrack analalamika, Shania hakujirekebisha. Akikaa na marafiki zake wanacheka, anasimulia jinsi wakiwa chumbani na Shadrack anavyomwaga machozi kwa ajili yake. Wenzake nao walishangilia, huku wakitamka waziwazi kwamba Shadrack ana tabia kama Bushoke. Eti ni mume bwege.
Kumbe Shania alikuwa na mwanaume mwingine anayeitwa Adili ambaye alimzuzua akili. Adili ni mfanyakazi wa kampuni moja ya bima, kwa hiyo kwa wakati huo alikuwa na kipato kikubwa kuliko Shadrack. Shania alisahau yote aliyopanga na Shadrack, akaamua kumtesa.
Siku moja Shadrack alinasa ujumbe kutoka kwa Shania kwenda kwa Adili. Ujumbe huo ulikuwa ni malalamiko ya Shania akimlaumu Adili kwamba hamjali, anamtesa licha ya kwamba yeye anampenda sana. Ukitazama ujumbe huo, kile anachokilalamikia Shania kwa Adili, hakitofautiani na malalamiko ya Shadrack kwa Shania.
Ukiutazama kwa makini ujumbe huo, ni kama Shania aliamua kuugeuza ujumbe wa Shadrack kwake, halafu akautuma kwa Adili. Shadrack aliumia kupita kiasi, akaona kumbe Shania hampendi ila anampenda Adili, kwani pamoja na kutendwa bado analalamika na anahitaji apewe nafasi.
Kutokana na sura aliyoipata katika ujumbe huo, Shadrack aliinua mikono juu. Shania hakujali, akaendeleza mapenzi yake kwa Adili. Miezi 10 baadaye, Shania alipata mimba lakini Adili aliikataa, akaamua kuitoa. Mimba ilikuwa kubwa, kwa hiyo chupuchupu Shania apoteze maisha.
Shadrack alipomaliza chuo kikuu, alipata ajira kampuni moja ya kimataifa, tawi la Dar es Salaam. Kwa mara nyingine, Shania baada ya kuona mambo safi kwa Shadrack, huku penzi lake kwa Adili likiwa limekufa, alirudi tena. Safari hii Shadrack akawa muoga wa kutendwa lakini Shania akadai amejirekebisha, kwamba matukio ya nyuma yalisababishwa na utoto.
Kwa awamu nyingine wakarejesha mapenzi yao. Baada ya muda mfupi, Shadrack akawa anagusia suala la kufunga ndoa, Shania akawa mgumu kukubali. Badala ya kuendeleza stori za ndoa, Shania akawa anamwambia Shadrack kwamba yeye hawezi kumuacha, eti hata akiolewa atakuwa anamsaliti mume wake na kwenda kumpa mapenzi.
Kilichokuwa kinamdanganya Shania ni mwanaume mfanyabiashara mwenye fedha zake. Alimuingilia kwa gia ya kuoa, naye kwa tamaa ya fedha akakubali. Kuanzia hapo, akawa anamchukulia Shadrack kama kipozeo. Akiwa na hamu, anamtafuta lakini hakuwa na matarajionaye yoyote.
Usiku mmoja akiwa amelala, Shadrack alikurupushwa na mlio wa SMS, aliposoma kumbe ulitoka kwa Shania akimtaarifu kwamba siku iliyofuata ndiyo ndoa yake. Shadrack alichanganyikiwa, akaja kugundua kwamba kumbe muda wote Shania alikuwa na mchumba lakini akawa anamdanganya.
Itaendelea wiki ijayo.

www.globalpublishers.info.

No comments: