ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 7, 2012

‘Aibu walarushwa wa rada kuongoza kamati Bunge’

Ezekia Wenje 
Mzimu wa kashfa ya rushwa ya ununuzi wa rada ya kijeshi ambayo Tanzania iliinunua kutoka Uingereza umeibuka kwa mara nyingine bungeni, baada ya wabunge wa Kambi ya Upinzani kuchachamaa na kutaka waliohusika na ununuzi wa rada watajwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Wabunge hao walikuwa wakichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa iliyowasilishwa na Waziri Bernard Membe.



 Msemaji wa Wizara hiyo, Ezekia Wenje (Chadema-Nyamagana), alihoji: “Tunaendelea kuhoji kwa nini mpaka sasa watuhumiwa wa kashfa hiyo wanaendelea kutembea kifua mbele dhidi ya serikali bila hatua zozote kuchukuliwa?.”

Alisema hadi sasa haieleweki ni kwa sababu gani Tanzania  pamoja na kudai kuwa ina uhuru wa kujiamulia mambo yake yenyewe iliamua kuliachia suala hili kufanyiwa kazi na Serikali ya Uingereza, kuanzia uchunguzi hadi kurudishiwa fedha zilizotokana na rushwa ya rada, ambazo kwa sasa zimebatizwa jina tamu la ‘chenji ya rada.’

“Katika hali inayoonesha kuwa baniani mbaya kiatu chake dawa, pamoja na serikali hii kushindwa kufanya uchunguzi na hatimaye kuwashtaki watuhumiwa wa rada, bado ilipobainika mahakamani kuwa tunatakiwa kurudishiwa chenji iliyotokana na rushwa, serikali ilikuwa mstari wa mbele kwelikweli katika kufuatilia chenji ya rada na katika kuipangia matumizi,” alisema na kuongeza:

“Tunashindwa kuelewa umakini wa serikali hii uko wapi kwamba inaweza kuweka msisitizo pekee katika kuhakikisha fedha za rushwa ya rada zinarejeshwa nchini, lakini haiwezi kuthubutu kabisa kushughulikia wale waliosababisha upotevu huo wa fedha za nchi kwa njia ya mikataba.”

Alihoji usikivu wa serikali ambayo pamoja na kelele zote za wananchi walioiweka madarakani kutaka watuhumiwa ufisadi kupimwa kwa kipimo kile kile katika mizani ya sheria na utoaji haki kama wanavyofanyiwa Watanzania wengine wanyonge.

“Bado serikali imetia masikio pamba na kufumba macho yake kwa mikono, kwamba haiwaoni mafisadi hao wala haisikii kelele za wenye nchi. Taarifa mbalimbali zinazotokana na utafiti na uchambuzi wa kina, zimeweka wazi wahusika wa kashfa ya ununuzi wa rada, zikieleza mchakato mzima namna wizi huo ulivyofanyika,” alisema na kuongeza:

“Ukiwahusisha Watanzania wengine wakiwa ni viongozi waandamizi wa serikali ya CCM na sasa Watanzania wanashangaa kuona watuhumiwa hao hao waliopaswa kuwa mikononi mwa sheria, sasa wanachaguliwa kuongoza mhimili muhimu wa Bunge! Kambi Rasmi ya Upinzani tunahoji je, hii ni dalili ya kuwa dola imetekwa na mafisadi?.”

Ingawa Wenje hakuwataja watuhumiwa hao kwa majina, lakini mmoja wa watuhumiwa hao anayeongoza moja ya kamati za Bunge ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi.

Chenge wakati wa mchakato wa ununuzi wa rada hiyo kutoka Kampuni ya BAE Systems mapema miaka ya 2000, alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Chenge alikutwa na Dola za Marekani milioni moja katika benki moja iliyoko katika Kisiwa cha Jersey nchini Uingereza.

Hata hivyo, mara kadhaa Change amekuwa akikanusha kuhusika katika wizi wa fedha za rada hiyo na kudai kuwa Taasisi ya Kuchunguza Makosa Makubwa ya Udanganyifu ya Uingereza (SFO) ilishamsafisha.

Mbunge wa Viti Maalum, Rachel Masishanga (Chadema), aliitaka serikali kueleza ni kina nani waliohusika na kuibia serikali katika kashfa ya rada.

“Tumepata chenji ndio tuwajue ni kina nani waliohusika na kama anawafahamu kwa majina naomba leo hii awaambie Watanzania waliohusika kuiibia serikali katika suala hilo la rada,” alisema.

Mbunge wa Gando, Khalifa Mohamed Khalifa  (CUF), alihoji: “Nyie ndio mnatuletea wawekezaji, lakini nyie ndio mnapaswa kuangalia huko nje maslahi ya taifa. Wewe ni mwanadiplomasia namba mbili, wa kwanza ni Rais na wewe mwenyewe uliwahi kufanya kazi katika balozi,  hivi kweli unataka kutuambia hujui watu wanaotuibia fedha zetu?” alisema na kusisitiza:

“Kweli hujui, hivi kweli hujui wawekezaji matapeli ukatuambia unaruhusu wanakuja tu hapa kila siku vinasemwa vitu hivi na watu wanafanya utafiti, hii ni aibu kubwa sana, hatuwezi hata siku moja tukavumilia nchi inadhalilishwa na watu na nyie nawajua mnawanyamazia, utakapokuja kufanya majumuisho utawatajia Watanzania,” alisema.

Alisema hata kama yeye (Khalifa) yumo katika orodha ya watu hao waliohusika na rushwa Membe amtaje.

 Akijibu katika majumuisho ya hotuba ya Waziri Membe jana jioni, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, alisema hakuna mtu yeyote kutoka Tanzania  ambaye anaweza kushtakiwa mahakamani kwa mashitaka ya rada.

“Kama kuna mtu yeyote ndani ya Bunge ama nje ya Bunge mwenye ushahidi juu ya mtu yeyote kama walimpiga picha ama mlikuwa naye atuletee huo ushahidi na tutapeleka mahakamani,” alisema.

Alisema jana asubuhi alizungumza na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), Eliezer Feleshi pamoja Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hoseah, ambao walisema hakuna kitu kipya na wala hawafanyi uchunguzi kuhusu sakata la rada.

Wiki iliyopita, Rais Kikwete, alisema hakuna mtuhumiwa katika sakata ya rushwa na kwamba walioanzisha suala hilo ni SFO.

Rais alisema baada ya kuwahoji maofisa hao, SFO walirudi Uingereza na kukaa kwa muda mrefu pasipo taarifa yoyote, lakini walishangaa kusikia kwamba kampuni iliyokuwa imetuhumiwa kwa rushwa ya BAE System ikikiri mahakamani kwamba ilifanya makosa ya kutoweka kumbukumbu za kiuhasibu tu, hivyo kuamua kulipa fidia kwa nchi iliyokuwa imefanya nazo biashara ikiwamo Tanzania, Saudi Arabia na Marekani.

“Sasa aliyekuwa anatuhumiwa kwa rushwa amekataa kuhusika na rushwa, amekiri kosa la kiuhasibu la kuweka hesabu vibaya, hapa unamshitaki vipi mtu wakati kampuni yenyewe (BAE) haipo,” alihoji Rais Kikwete na kuongeza:

“Hata jaji (wa Kiingereza) aliyeamua kesi hiyo hakufurahishwa na utaratibu uliotumika.”

Tanzania iliuziwa rada ya bei mbaya ya Sh. bilioni 70 wakati huo na baada ya sekeseke kubwa BAE waliamua kuirejeshea Tanzania Sh. bilioni 72 za fedha  zilizobatizwa jina la chenji ya rada, ilhali watu wengine wakisema si chenji ila ni rushwa ya rada.

 
CHANZO: NIPASHE

2 comments:

Anonymous said...

Very sad

Anonymous said...

Kuna siri kubwa sana hapo,Mbona kazi ipo?Na huyo Andrew Chenge alipata wapi pesa zote hizo za dola milioni moja alizokuwa nazo kwenye akaunti yake ya uiengereza?Kwa mshahara gani anaolipwa hadi akutwe na pesa nyingi hivyo?Andrew chenge na Edward Lowassa wasingepaswa kuwa serikalini tena!Maana ndiyo Mafisadi wakubwa wa nchi!Na Mh. Rais JK anawakingia kifua na kuwafumbia macho kwa yote waliyoyafanya!Wanazidi kuifilisi nchi yetu!