Friday, August 31, 2012

DAWA YA MWANAUME ANAYENG’ANG’ANIA KUTAKA KUONJA PENZI LA MUMEO!


HUKO mitaani kuna wanaume ambao wanafahamika kuwa ni viwembe ile mbaya. Yaani wao wakiona msichana mzuri mbele yao, hawaoni hatari kutumia gharama kubwa kuhakikisha wanamnasa.
Mbaya zaidi hawaangalii kama huyu ni mke wa mtu au yupo singo, wao kila msichana mrembo ni halali yao. Hawa ndiyo ambao wamekuwa wakisababisha ndoa nyingi kusambaratika.

Kwa harakaharaka, wanaume hawa tuwaite ni sumu na kwa mwanamke yoyote ambaye ameolewa na anataka kudumu kwenye ndoa yake, anatakiwa kuwa makini sana na sampuli hii ya wanaume.
Ni kweli kutongozwa kupo kwa kila mwanamke aliyekamilika. Usipotongozwa jiangalie mara mbili mbili ila utawezaje kukabiliana na mwanaume ambaye kila siku anakushawishi umuonjeshe penzi kwa madai kuwa amekuzimikia?
Hapa kuna mtihani mzito lakini wapo ambao wanafaulu. Wanafanyaje? Kwanza unatakiwa kuwa mkali sana kwa mwanaume ambaye anakutongoza ilihali anajua wazi wewe ni mke wa mtu au una mpenzi wako. Kwa taarifa yako, mwanaume ambaye anajua umeolewa/una mpenzi wako na bado anakutongoza, huyo amekudharau sana.
 Yaani atakuwa amekuchukulia wewe ni changudoa kaisi kwamba anahisi hata kama una mtu wako lakini na yeye unaweza kumpa ‘mambo’. Huyu unatakiwa kumkaripia sana na kumtaka akuheshimu kama anataka na wewe uendelee kumheshimu.
Lakini wengine ni ving’ang’anizi kweli, yaani hata uwatukane vipi wataendelea kukufuata. Hawa hutakiwi kudili nao kimyakimya, mumeo lazima ajue na mshirikiane kukabiliana naye.
 Sishauri kila mwanaume atakayekuchomekea umwambie mumeo. Nasema hivyo kwa kuwa, natambua itageuka kero kwa mwenza wako ila kwa kufanya hivyo naamini itasaidia kwani mumeo anaweza kuchukua hatua zinazostahili dhidi yake na hatimaye kuweza kupunguza kasi ya usumbufu huo. Kamwe usithubutu kukaa kimya.
Mbaya zaidi ni kwamba unaweza kukuta shemeji yako ambaye ni rafiki wa karibu wa mpenzi wako ama mwanaume anayemfahamu vilivyo mumeo akakutongoza. 
Huyu ni hatari sana na wala usisubiri akutongoze mara mbili. Siku ya kwanza tu atakayokutamkia maneno yake ya kipuuzi, kwanza geuka mbogo, mkaripie kwa ukali, akiendelea na kuonesha yuko ‘siriasi’ mpe taarifa mpenzi wako.
 Niseme tu kwamba, wanaume siku hizi wametawaliwa na tamaa zisizokuwa za kijinga. Ukiwalegezea watakufanya jamvi la wageni licha ya kwamba umeolewa. Aibu iliyoje? Nadhani ni vyema ukauheshimu uhusiano ulionao, mheshimu mumeo kwa kuhakikisha humfanyi akachangia penzi lako na wanaume wengine ambao ni wa kupita tu.
Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo.

www,globalpublishers.info

No comments: