KARANI wa sensa ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Kawe, iliyopo Kata
ya Kilago, Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, Stanley Mahene, ameuawa
na watu wasiofahamika na kuporwa sh.200,000, alizolipwa baada ya
kuhudhuria mafunzo ya sensa.
Tukio hilo lilitokea juzi baada ya watu
wanaodhaniwa kuwa majambazi, kuvamia nyumbani kwake, kuvunja mlango,
kuingia ndani, kumkata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili, kupora
fedha hizo na mali nyingine.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Evelist Mangalla, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo kijijini hapo.
“Marehemu
alirudi nyumbani kwake akiwa na fedha hizo lakini watu wasiofahamika
walivamia nyumba yake, kumpiga mapanga, kumpora fedha na mali nyingine,”
alisema Kamanda Mangalla.
Aliongeza kuwa, vitu vingine
walivyochukua watu hao ni pamoja na simu ya mkononi, televisheni,
jenereta pamoja na deki ambapo hadi sasa, Jeshi la Polisi linawashikilia
watu watatu kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo baada ya kukamatwa na
baadhi ya vitu vilivyoibwa kwa marehemu.
No comments:
Post a Comment