ANGALIA LIVE NEWS
Monday, August 27, 2012
MAKALANI ILALA WAGOMEA SENSA,PINDA KUWATOA WASIWASI WA MALIPO YAO
WAZIRI Mkuu, Bw.Mizengo Pinda, amesema posho za wenyeviti wa vitongoji na vijiji ambao wataambatana na makarani wa Sensa ya Watu na Makazi iliyoanza jana, zipo palepale hivyo hakuna sababu ya kujenga hofu juu ya malipo yao.
Bw.Pinda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Sensa, aliyasema hayo jana baada ya kuhojiwa na maofisa wa sensa kijijini kwake Kibaoni, Wilaya ya Mlele, mkoani Katavi.
Aliwasihi wenyeviti hao waendelee na kazi yao bila wasiwasi wowote wa kupata malipo yao.
“Ni kweli malipo yao yamechelewa kwa sababu ni siku ya mapumziko lakini niwahakikishie kuwa stahili zao zipo, wao wachape kazi tu,” alisema Bw.Pinda.
Aliongeza kuwa, baadhi ya vyombo vya habari vimesema wenyeviti hao wameachwa katika malipo ya kazi hiyo. “Nimeona kwenye TV wanadai wameachwa, si kweli watalipwa,” alisema.
Akizungumzia mchakato mzima wa sensa, Bw. Pinda aliwaomba Watanzania watambue kuwa, suala la sensa lilianza tangu mwaka 2004 na lina gharama kubwa ambapo mwaka huu, Serikali imegharamia zaidi ya sh. bilioni 140.
“Hili ni jambo linalopaswa kupewa nafasi kubwa na kila Mtanzania, lengo ni kuiwezesha Serikali kujua idadi ya watu tulionao ili tuweze kupanga maendeleo yetu.
“Serikali inao mpango wa miaka mitano, ifikapo 2013 tunaweza kujua malengo yetu na kuweka mbinu za kuitekeleza,” alisema Bw. Pinda na kuongeza kuwa, ukweli huo unabainishwa na maswali yaliyomo kwenye dodoso la sensa.
Alisema maswali hayo yanalenga kujua jinsia za watu, umri, shughuli zao kiuchumi na kuwaweka katika makundi ili iwe rahisi kuwahudumia, kujua mahitaji yao na kuwafikishia huduma.
“Makarani wataendelea kutembelea kaya kwa siku saba zijazo, cha msingi mkuu wa kaya aandae taarifa za watu waliolala kwenye mji wake, aorodheshe majina yao, umri, elimu, jinsi na shughuli wanazifanya,” alisema.
Akizungumzia baadhi ya watu wanaopinga sensa, Bw. Pinda aliunga mkono kauli ya Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed Shein, kuwataka Watanzania wote washiriki Sensa ya Watu na Makazi.
“Viongozi wetu wa kitaifa wamelielezea vizuri suala hili hasa kipengele cha dini,” alisema Bw. Pinda.
Wakati huo huo, Mwandishi Wetu Grace Ndossa anaripoti kuwa, zaidi ya makarani 100 wa Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, wameulalamikia uongozi wa manispaa hiyo kwa kushindwa kuweka utaratibu mzuri wa kuwapa malipo yao ili waweze kuanza kazi hiyo kama ilivyopangwa na Serikali.
Wakizungumza na Majira jana kwa nyakati tofauti, makarani hao walisema tatizo hilo limewafanya washindwe kwenda katika vituo vyao ili kuanza kazi waliyopewa.
“Leo (jana), tulikuwa tuanze kazi asubuhi lakini hadi sasa hatujui hatima yetu,” alisema karani mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Aliongezea kuwa, baadhi ya makarani wamelipwa lakini hawana vituo vya kazi na wengine ambao wamepangiwa vituo hawajalipwa kabisa.
“Juzi tulizungumza na Mkuu wa Wilaya ambaye alituambia tufike katika Shule ya Msingi Buguruni, leo (jana), asubuhi na mapema ili tuweze kulipwa fedha zetu lakini hadi sasa saa tano na nusu, hatujamuona mtu yeyote,” alisema.
Hata hivyo, makarani hao walisema hawapo tayari kuifanya kazi hiyo hadi watakapopewa fedha zao kwani mkataba waliosaini unaeleza wazi kuwa wanastahili kulipwa fedha nusu ili waanze kazi na kilichobaki watalipwa baada ya mchakato huo kukamilika.
Makarani hao wanatoka vituo vya Madenge, Kisiwani,Vingunguti, Ilala, Kiwalani na Kipawa.
“Katika mafunzo tuliyofanya, kulikuwa na makundi matatu, wengine walilipwa lakini baadhi yao hawakulipwa, makarani wengine wameshiriki mafunzo, kulipwa posho lakini hawajapangiwa vituo,” alisema karani huyo.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw.Raymond Mushi, alikiri kusikia malalamiko hayo na kudai tayari amewataka waorodheshe majina yao ili waratibu wa sensa waweze kuyapitia kama kweli hawajalipwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment