Kocha Mkuu wa Yanga, Tom Saintfiet.
Na Khatimu Naheka
KOCHA Mkuu wa Yanga, Tom Saintfiet amesema mashabiki wa timu hiyo ndiyo waliosababisha asaini mkataba wa kukinoa kikosi hicho.
Kauli hiyo ya Tom inakuja ikiwa ni siku chache tangu kuenea kwa taarifa za kocha huyo kuchukizwa na kutokamilishiwa mahitaji muhimu yaliyopo ndani ya mkataba wake wa miaka miwili wa kukisuka kikosi hicho.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Tom raia wa Ubelgiji, amesema licha ya kutotimiziwa baadhi ya mambo muhimu ndani ya mkataba wake huo, amesema siri kubwa ya kuwa katika kikosi hicho kama kocha ni mashabiki wa klabu hiyo.
Tom amesema upendo wa mashabiki wa timu hiyo ndiyo silaha kubwa inayomfanya kutulia aifundishe Yanga na ana imani uongozi wa kikosi hicho utakamilisha yale waliyomuahidi wakati wakimpa mkataba.
“Kabla ya kuja hapa Yanga niliona mechi moja katika mtandao na nikavutiwa na mashabiki wazuri wa Yanga ambao walinisababisha nije hapa kufundisha,” alisema Tom na kuongeza:
“Uwepo wangu hapa ni kutokana na heshima yao, siwezi kuzungumzia kwa undani juu ya mkataba wangu lakini naamini uongozi utamaliza yale ya muhimu waliyoniahidi mapema, nina furaha kuwa hapa Yanga kutoka moyoni kwangu, sifikirii kuondoka kwa sasa.”
No comments:
Post a Comment