Friday, August 31, 2012

WASOMI WATAKA RAIS APUNGUZIWE MADARAKA,ASHITAKIWE

 MH RAIS JAKAYA KIKWETE
Waadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua) mkoani Morogoro wametoa maoni yao kuhusu marekebisho ya katiba mpya, wakipendekeza  Rais aondolewe madaraka ya kuteua majaji na kushtakiwa muda wote itakapobainika ametumia vibaya madaraka yake.

Aidha, wamependekeza  mawaziri wanaoteuliwa na Rais wasitokane na Bunge, iundwe serikali ya Tanganyika na kuwepo kwa mgombea binafsi.

Waadhiri hao walitoa maoni yao  wakati wa mjadala kuhusu katiba mpya uliandaliwa Chama cha Wanataaluma wa Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Suasa), Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Vyuo (Raawu), Umoja wa Wanafunzi wa Sua (Suaso) na Umoja wa Vyuo vya Elimu ya Juu (Thtu) uliofanyika mjini Morogoro.

Waadhiri hao walisema katiba ya sasa  inampa madaraka makubwa Rais kuwa na uwezo wa kuteua viongozi wa mihimili ikiwemo mahakama, hivyo katika katiba mpya anapaswa kupunguziwa madaraka hayo.

Profesa Bukheti Kilonzo, alisema kuwa katiba mpya lazima iunde chombo cha kitakachoweza kumteua Jaji Mkuu na majaji badala ya nafasi hiyo kubakii kwa Rais na kuwa kwakufanya hivyo chombo hicho cha maamuzi kitakuwa huru na kuweza kutenda haki.

Alisema kuwa pia katiba hiyo inapaswa kumuondolea kinga ya kutoshtakiwa Rais anayekuwa madarakani na anapomaliza kipindi chake pale itakapobainika ametumia nafasi hiyo vibaya ili kuongeza uadilifu kwa kiongozi huyo wa nchi.

Profesa Andalwiye Katule kutoka Kitivo cha Sayansi ya Wanyama, alisema katiba mpya itenganisha nafasi ya ubunge na uwaziri pamoja na nafasi ya mkuu wa mkoa ambao wanateuliwa  na Rais.

Alisema mbunge anapaswa kutoteuliwa kuwa waziri, mkuu wa mkoa wala wilaya, badala yake aachwe kutumikia wananchi waliompigia kura ili awakilishe matatizo kwa serikali.

Aidha, alisema kuwa hata mbunge anapochaguliwa kuwa Spika wa Bunge anapaswa kujiuzulu nafasi ya ubunge kupitia chama chake ili kutoa maamuzi pasipo upendeleo wa chama chake.

Kadhalika alipendekeza kufutwa viti maalumvya ubunge kwa kuwa havina uwakilishi wa wananchi.

“Hatutaki Spika wa Bunge mkeleketwa wa chama fulani na kutoa upendeleo kwa wabunge wa chama chako, ukichaguliwa Spika lazima ujiuzulu ubunge unaotokana na chama chako ili utoe haki kwa wabunge wote,” alisema.

Profesa Andrew Talimo, alitaka katika katiba mpya ya mwenyekiti wa chama chochote cha siasa asigombee nafasi ya urais huku akitaka kutungwa kwa chombo ambacho kitawachukulia hatua vyombo vya usalama vinavyo kiuka haki za binadamu, ikiwemo ya kuwapiga watu wasio na hatia na hata kuwaua.

Mhandeni Abdulkarim kutoka idara ya Sayansi Jamii, alitaka umri wa kugombea urais upunguzwe na kuwa miaka 35.

 

No comments: