ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 11, 2012

Genge la wahalifu lateka nyara Polisi


  Ni yule aliyeshiriki operesheni Bandarini
  Latoa masharti ya kuachiwa huru wenzao
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova
Katika tukio linalofanishwa na vita ya vigogo wa dawa za kulevya dhidi ya mamlaka za serikali nchini Mexico, limetokea nchini kwa askari wa Bandarini jijini Dar es Salaam, Cornel Kufaizalu, ambaye alishiriki katika operesheni ya kukamata watu waliovamia bandari kwa lengo la kuiba madini ya shaba na petroli, kutekwa nyara na watu wasiojulikana ambao pia inadaiwa wametishia kumuua kama masharti yao hayatatimizwa na polisi haraka.

Askari huyo ambaye anaonekana kama shujaa kwa kujitoa muhanga kupambana dhidi ya askari wenzake walioamua kuasi na kujiunga na magenge ya wizi na uhalifu bandarini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, sasa ametekwa nyara na hajulikani aliko.



Askari huyo alikuwa mwiba dhidi ya watuhumiwa wa wizi wa mali bandarini Dar es Salaam akipambana na watu hao miongoni mwao wakiwamo askari waliokuwa doria na taarifa kuhusiana na sakata hilo zilitolewa na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe,wakati akizungumza na waandishi wa habari Jumamosi iliyopita.

Taarifa ambazo NIPASHE imezipata ambazo zilithibitishwa na viongozi wa bandari hiyo pamoja na Wizara ya Uchukuzi zinasema kwamba askari huyo alitekwa Septemba 8, mwaka majira ya jioni na watu wasiojulikana ambao wamempeleka kusikojulikana.

Waziri Mwakyembe alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, alisema amepewa taarifa za kutekwa kwa askari huyo ikiwa ni siku moja tu baada ya kukamatwa kwa watu 14 waliovamia bandari usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na viongozi na wafanyakazi wa bandari, watu waliomteka askari huyo wametoa masharti kwamba watamuachia huru iwapo tu wenzao watuhumiwa waliokamatwa wakati wa mapambano kati yao na polisi wa bandarini katika tukio hilo wataachiwa huru.

Walisema watekaji hao ambao wametuma ujumbe mfupi wa maneno katika simu ya askari huyo aliyetekwa, wametoa muda wa saa 24 kuachiliwa kwa watu hao waliokamatwa katika tukio hilo na kama hawataachiwa, watachukua uamuzi mwingine dhidi yake.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema taarifa walizopata ni kwamba askari huyo amepatikana Mafinga mkoani Iringa.

Wakati Kova akieleza hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, alipoulizwa alisema hana taarifa za askari huyo wa bandari aliyetekwa kupatikana mkoani kwake.

Dk. Mwakyembe akizungumza na waandishi wa habari Jumamosi iliyopita baada ya kutokea tukio hilo, aliagiza watu wote waliohusika na wizi huo wakamatwe na kufunguliwa mashitaka, wakiwemo askari waliokuwa doria ambao baada ya kufika eneo la tukio walianza kuiba mafuta badala ya kusaidia askari wa bandarini kupambana na wezi.

Alisema ofisa wa bandarini aliyehusika kufunga kontena namba MSKU 268357(6) ameshafahamika na yeye atakamatwa ili afunguliwe mashitaka.

Akielezea zaidi kuhusiana na tukio hilo, Dk. Mwakyembe alisema Jumamosi usiku kulitokea matukio mawili ya wizi. La kwanza lilitokea saa 9:00 ambalo injini ya treni yenye kichwa namba CK620006 ilikuwa inakwenda bandarini kwa ajili ya kubeba mabehewa manane.

Waziri Mwakyembe alisema kati ya hayo, matano yalibeba mbolea na matatu yalikuwa tupu.
Alisema katika treni hiyo kulikuwa na wafanyakazi wanne ambao ni dereva Abdallaham Shebe (dereva), Bakili Kitanda (muongoza treni), Polisi PC Abubakar mwenye namba F 8784 na msimamizi wa treni Gideon Anyona.

Dk. Mwakyembe alisema wakiwa bandarini, walivunja kontena ambayo ilikuwa na shaba na kuanza kupakua na kuihamishia kwenye makontena ya treni ya Tazara na kufanikiwa kuhamisha vipande 19.

Wakati wakiendelea na harakati hizo, kulizuka mapambano kati ya polisi wa bandarini  na wafanyakazi hao ambayo dereva pamoja na muongozaji walifanikiwa kukimbia na kwenda eneo la Yombo na wengine wawili walikamatwa.

Tukio la pili lililotokea saa 10 alfajiri katika depo ya Oryx ambako kulikuwa na kundi kubwa la watu waliokuwa wanaiba madumu ya mafuta na kuyatupia upande wa pili wa bandarini. Madumu yalikuwa tisa ya lita 20 kila moja lilikuwa na petroli.

Alisema wakati wanaendelea na harakati hizo, polisi waliokuwa doria walifika eneo la tukio na kukuta polisi wa bandarini wakipambana na kundi la wezi, lakini polisi wa doria badala ya kuwasaidia polisi wa bandarini kupambana na wezi hao, walianza kuiba madumu hayo ya mafuta na kuchukua manne na kuondoka nayo.

Aidha, alisema bosi aliyewatuma wafanyakazi kuiba shaba kwenye kontena anaonekana kuwa ni mzoefu hivyo watamkamata kwa sababu wameshamfahamu.

WATU 14 WATIWA MBARONI


Kamanda Kova jana alizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa Septemba 8, mwaka huu majira ya saa 8:00 usiku katika eneo la Shedi No. 7, polisi waliwakamata watu 14 kwa kosa la kuvunja kontena na kuiba vipande 19 vya madini ya shaba, mafuta ya petroli lita 360 na dizeli lita 60.

Aliwataja waliokamatwa kwa kuiba madini ya shaba kuwa ni Askari Polisi kikosi cha Tazara mwenye namba F. 8774  PC Abubakar; Charles Rejino (49), mkazi wa Tandika Azimio;  Range Boaz (40),  mkazi wa Kichemchem Mbagala na Willy Mwamlima (20), mkazi wa Kiwalani.
Wengine ni Ally Rwanda (28), mkazi wa Tandika Azimio; Said Salum (39), mkazi wa Tandika Azimio; Shabani Matimbwa (33), mkazi wa Tandika; Salum Kinyama (34) mkazi wa Tandika Azimio na Gideon Anyina (35) mkazi wa Mbezi Louis.

Kuhusu tukio la wizi wa mafuta ya petroli lita 360 na dizeli lita 60 yaliyoibwa katika yadi ya Oryx, aliwataja waliokamatwa kuwa ni Mohamed Said (18), mkazi wa Mtoni Mtongani na Fadhili Said (18), mkazi wa Mtoni kwa Azizi Ally.

Wengine ni Ailaji Bakari (19), mkazi wa Kurasini na Erasto Adam (18), mkazi wa Kurasini Shimo la Udongo.

Kamanda Kova alisema kimeundwa kikosi kazi cha watu 10 kinachojumuisha askari polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Polisi  bandari na Polisi Tazara kwa ajili ya kuhakikisha kuwa matukio ya wizi  bandarini yanakomeshwa.



 
CHANZO: NIPASHE

No comments: