ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 6, 2012

KAGASHEKI AZIONYA KAMPUNI ZA UWINDAJI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki, amegeuka mbogo kwa kuwaonya wamiliki wa kampuni kampuni za uwindaji wa wanyapori nchini wasitumie pesa zao kurubuni watendaji wa wizara hiyo katika mambo mabaya kwa lengo la kutaka kujinufaisha na sekta hiyo.

Alisema hayo wakati akizungumza katika mkutano na wamiliki wa vitalu vya kuwinda wanyapori jana jijini Dar es Salaam ambao uliandaliwa na wizara kwa lengo la kujadili mambo mbalimbali ya sekta ya uwindaji na changamoto inazoikabili.



“Natambua mna pesa nyingi sana, nawaomba msizitumie kushawishi watendaji katika mambo mabaya ili mjinufaishe wenyewe badala ya sekta hii kuwanufaisha Watanzania, sitakubali kuona hali hiyo na nipo makini sana kufuatilia,” alisema Kagasheki.

Alisema kama atabaini yupo mtendaji yeyote ndani ya wizara hiyo anamiki kitalu, hatakuwa na mjadala naye isipokuwa ni kumfukuza kazi.

Alisema wapo baadhi ya watu wakipewa vitalu vya kuwinda wanavifanyia ulanguzi kwa kuviuza kwa watu wengine wakati wanatambua kuwa  kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Aliongeza kuwa anatambua kuwa wamiliki wa vitalu wanafanya biashara ili wapate pesa lakini wanapaswa kutambua kuwa pia serikali inatafuta pesa.

“Watu ambao mpo kwenye sekta ya utalii muwe na huruma kwa nchi ya Tanzania, natambua mnataka kutengeza pesa, lakini serikali pia inataka kutengeneza pesa, fuateni taratibu msitumie nyia za mkato,” alisema Kagasheki.

Aliongeza kuwa sekta ya utalii inatakiwa kuingiza mapato mengi kwa serikali, lakini imekuwa tofauti kutokana na ufujaji wa fedha unaofanywa na baadhi ya watendaji wasiokuwa waaminifu.

Kagasheki alisema suala la mgawo wa vitalu vya uwindaji mara nyingi limekuwa likizua mtafaruku  na mjadala mkubwa ndani ya nchi ambapo serikali imejipanga kufanya mabadiliko ya sheria ili sekta hiyo iweze kuwa na manufaa kwa nchi.

“Msione serikali kama adui, nyie ni wafanyabiashara hivyo hakuna haja ya kuiona serikali kama adui, mfano asilimia 25 ya hisa  za makampuni ya uwindaji ni ya wazalendo…najiuliza kwanini isiwe 50 kwa 50,”alisema Kagasheki.

Mapema mwaka jana kulizuka mgogoro  wa vitalu vya kuwinda wanyamapori hali iliyolilazimu Shirikisho la Kimataifa la Wawindaji (SCI) kuanika hadharani mvutano uliopo kati ya serikali na baadhi ya kampuni za uwindaji huku likionya watalii wanaoingia nchini.

Sheria mpya ya Wanyamapori ya mwaka 2009 ambayo ilitumika katika ugawaji huo, inaeleza kuwa kampuni zinazomilikiwa na wageni kwa asilimia 100, zitakazopewa vitalu zitakuwa asilimia 15 ya idadi ya kampuni zote.



CHANZO: NIPASHE

No comments: