Hapa namaanisha kuwa wakati tunawaweka sawa masistaduu, inapendeza lile kundi la wanawake wanaojiona wapo makini wakawa mfano wa kuigwa. Waache tabia za mafichoni, hadharani kujionesha ni watu wazuri kimaadili, wakati gizani wao ni wachafu kuliko hata hao wanaoonekana.
Japo natoa mifano mbalimbali, jambo muhimu kwako ni kutambua kuwa ninachokielekeza hapa ni somo kwamba kuna jamii fulani inapotosha tafsiri halisi ya mapenzi. Hii inasababisha maumivu makali kwa watu wanaoyaheshimu. Fikiria wewe unampenda, halafu upo kwenye uhusiano na yule asiyejua maana ya kupendwa.
Wewe unayaheshimu mapenzi na unayazingatia kwelikweli, hivyo unao utambuzi kwamba tafsiri ya kupenda ni kupendwa. Sasa upo kwenye uhusiano na mtu ambaye hajui kurudisha upendo kwa anayempenda. Anachoamini mapenzi ni mtindo huru, kama vile kwenda sokoni na kuchagua sehemu ya kununua bidhaa zako.
Tunaishi kwenye jamii moja, tunaona jinsi masistaduu na mabrazameni walivyochakachua mapenzi. Watoto wadogo siku hizi nao wanayatenda kama game. Tukielewana tunapeana leoleo. Alichoimba Ali Kiba kwenye Single Boy akimshirikisha Lady Jaydee, hakina tofauti na hali halisi iliyopo.
Kwamba hivi sasa hakuna mapenzi zaidi ya kudanganyana. Kwa hiyo, bora ukimpenda mmalizane leoleo. Hoja inayojengwa ndani ya wimbo huo ni kuwa mapenzi yanaumiza kichwa, unaweza kupenda sana matokeo yake ukawa kama mwendawazimu. Wanamaliza kila mmoja akijisifia alivyo singo.
Unaweza kuona wimbo huo kuwa maudhui yake yanalenga kuivuruga jamii kwenye suala zima la mapenzi. Kwa upande mwingine ni vizuri kupata wana fasihi kama Ali Kiba ili waichambue hali halisi kwa mtindo ambao ameuelezea na Jaydee kwenye Single Boy.
Hata hivyo, kama mshauri wa saikolojia ya mapenzi, sikubaliani na hitimisho la Ali Kiba, badala yake nachochea mabadiliko chanya kwa watu ambao wamemfanya mwanamuziki huyo apate sababu ya kuyaponda mapenzi ya sasa, hivyo kutaka kila mtu awe na mtazamo wa kuwa singo.
SULUHU NI NINI?
Hupaswi kuishi singo, kwani athari zake zipo. Ukisema huyataki kabisa mapenzi, kuna kundi litakalokuvalisha kesi kuwa mambo yako si mazuri. Naijua vizuri jamii yetu, mwanaume anaweza kuambiwa jongoo wake hapandi mtungi, wakati ushahidi hana.
Ukisema uwe unarukiarukia watu hovyo, kama ambavyo wengine wanafanya (kumalizana leoleo tu), huko ni kupotea sana. Maradhi yamezunguka kila upande, hivyo utajikuta unatengeneza mtandao mkubwa wa ngono bila wewe mwenyewe kujijua.
Unatakiwa kutulizana halafu ushike maelekezo ambayo tunayatoa ili kuyakabili mapenzi ya sasa. Ukimuona mwenzako bado anasumbuliwa na fikra za usistaduu badala ya kuyaheshimu mapenzi, mpishe mapema kabla hajakuumiza ukalia. Yule anayezuzuliwa na ubrazameni, mpe njia yake aende. Maisha yako ni matamu bila yeye. Zingatia.
Hatua muhimu zinaanza na wewe. Kama tabia mbaya ambazo nimekuwa nikizizungumza zipo ndani yako, tafadhali, jirekebishe haraka. Endapo wewe upo sawa na umebaini kuwa huyo unayemwita mwenzi wa maisha yako ana vitabia visivyofaa, muepuke haraka.
Ninaposema hatua muhimu zinaanza na wewe namaanisha katika pande kuu mbili. Mosi ndiyo hiyo ya wewe mwenyewe kujirekebisha pale unapoona unachemka. Pili ni kuachana na mwenzi ambaye anasumbuliwa na vitabia ambavyo nimevibainisha kinaubaga tangu mwanzo wa makala haya.
UTAMJUAJE SISTADUU/BRAZAMENI?
Nimeshakupa suluhu lakini kuna uwezekano ukawa hujafunguka inavyotakiwa. Hivyo basi, nakupa dondoo kadhaa ambazo nazichambua kwa kifupi ili kukuwezesha kutambua maana halisi ya kile ambacho nimekuwa nikikitambulisha tangu mwanzo mpaka kufikia hapa tunapokwenda kwenye tamati ya mada hii.
MTEGO WA FEDHA
Ipo wazi kuwa walengwa ni watu wanaobudu sana fedha kuliko utu. Unaweza kufanya kila linalohitajika kufanywa na watu wa jinsi yako kwa mpenzi wako lakini mwisho ukaishia kuumia. Utaonesha upendo na namna unavyojali lakini matokeo ya mwisho utaachwa solemba, huku ukilia kilio cha kusaga meno.
Itaendelea wiki ijayo...
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment