INADAIWA kwamba askari waliokuwa katika operesheni ya kuzuia mkutano wa
Chadema katika eneo la Nyololo wilayani Mufindi, Iringa na ambayo
ilisababisha kifo cha Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi walitolewa
katika mikoa ya Dodoma, Morogoro na Mbeya.
Tayari tukio hilo
limeibua mjadala mzito kiasi cha kumfanya Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi kuunda tume huru kubaini chanzo cha tukio
hilo. Marehemu Mwangosi alizikwa juzi nyumbani kwao Tukuyu, mkoani
Mbeya.
Habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili jana zilisema
kuwa polisi hao kutoka mikoa hiyo mitatu wakiwa wamesheheni vifaa
mbalimbali likiwamo gari la maji ya kuwasha, walisafiri siku moja kabla
ya mkutano huo wa Chadema na baadaye kuzuka vurugu zilizosababisha kifo
hicho.
Marehemu Mwangosi aliuawa kwa mlipuko unaodhaniwa kuwa ni wa bomu ambao ulisambaratisha vibaya sehemu kubwa ya mwili wake.
Chanzo
cha habari kutoka mkoani Dodoma kilisema: “Hapa kwetu kuna askari 10 na
tunawafahamu kwa majina. Waliondoka hapa siku moja kabla ya tukio hilo
wakiwa na gari la washawasha.”
Chanzo hicho kilisema kwamba awali,
hawakuwa wakifahamu kama baadhi ya wenzao walichukuliwa na kupelekwa
Iringa. “Tulikuja kuona kwenye gazeti picha na tulipofuatilia tukaelezwa
kuwa ni kweli Dodoma ilitoa askari kwenda Iringa.”
Askari
mwingine aliyekuwa katika operesheni hiyo ambaye jina lake tunalihifadhi
kwa sababu za kitaaluma, alikiri kuwa hadi jana baadhi yao walikuwa
bado wako Iringa na kwamba walikwenda kwa agizo la wakubwa wake wa kazi.
“Sisi
ni Watanzania, lakini tumelazimika kuyafanya hayo kwa sababu ya mkate
(malipo). Kwa kweli haikuwa haki, kuwatoa askari na silaha kutoka mikoa
mitatu kana kwamba wanakwenda kupigana vita!”
Alidokeza kwamba,
askari wote waliotoka Dodoma walikuwa njiani kurudi mkoani humo, jana
lakini gari la maji ya kuwasha liliendelea kubaki huko Iringa likiwa na
dereva wake na askari mmoja mwenye cheo cha inspekta. Askari huyo
alisema kwamba gari hilo lililazimika kubaki kutokana na hitilafu.
“Wengine
wamerudi lakini, kuna wengine wenye gari la kuwasha bado walikuwa
Iringa, gari lao limepata hitilafu kidogo,” kilisema chanzo hicho kutoka
mjini Dodoma.
Mmoja wa askari hao alidaiwa kwamba hiyo inaweza
kuwa moja ya sababu ya askari hao kumshambulia marehemu Mwangosi wakati
mwenzao anayemfahamu akijaribu kuwazuia. "Hii inaonyesha kuwa askari hao
waliompiga walikuwa hawamjui na huyu aliyekuwa akiwazuia, alimjua.”
Makamanda watupiana mpira
Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo,
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen hakukubali wala
kukanusha na badala yake alisema: “Mambo yote hayo yanatakiwa kujibiwa
na Kamanda wa Iringa.”
Aidha, alisema sakata la kifo cha mwandishi
huyo kwa sasa liko katika vyombo vya uchunguzi hivyo asingekuwa tayari
kulizungumzia.
“Siwezi kusema kama askari wangu walikwenda huko
au hawakwenda, isipokuwa ninachoweza kusema ni kwamba suala hilo lipo
katika vyombo husika hivyo waachiwe wao au Kamanda wa Iringa ndiye
mwenye majibu.”
Alipotajiwa jina la mmoja wa askari aliyeonekana
katika picha za video na magazeti za tukio hilo kwamba anatokea katika
moja ya vituo vyake, kamanda huyo alisema: “Mimi yakitokea Dodoma
nitazungumza wala siyo mtu mwingine kwa hiyo, mambo ya Iringa siwezi
kuyazungumza na kama tutaanza kila Kamanda kuzungumza jambo hilo hamuoni
kuwa itakuwa ni kama vurugu?”
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda alipopigiwa simu yake iliita tu bila kupokewa.
Kwa
upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Faustine Shilogile
alisema kwa kuwa tukio hilo limefanywa na polisi, mambo mengi
yatazungumzwa lakini akasisitiza kwamba hajapeleka askari Iringa.
Alisema
hakukuwa na agizo kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi wala ombi
kutoka Polisi Iringa kutaka askari wa kuongeza nguvu... “Taarifa hizo ni
za uzushi kwani hazina ukweli wowote.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mbeya, Athuman Diwani alikanusha pia kuwapeleka askari wake Iringa
akisema: “Hizo taarifa siyo za kweli. Hakuna askari yeyote aliyekwenda
Iringa wakati wa vurugu zile.”
Mkutano wa DCI wavunjika
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya
Jinai (DCI), Robert Manumba hakutaka kuzungumzia suala hilo akisema:
“Hayo yote yameundiwa tume ngoja tuiachie ifanye kazi yake.”
Awali,
DCI Manumba aliitisha mkutano na waandishi wa habari mkoani Iringa,
ambao hata hivyo, ulivunjika baada ya kutokea kutoelewana baina yao.
Manumba
alitaka kueleza ripoti ya uchunguzi wa kifo cha Mwangosi, lakini
waandishi hao walikataa kumsikiliza wakisema hawauamini uchunguzi huo
kwa kuwa ulifanywa na polisi peke yao.
Kabla Manumba, hajaanza
kuzungumza, Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Iringa (IPC), Frank
Leonard alisema kutokana na msimamo wa waandishi wa habari wa mkoa huo
hakutakuwa na uhusiano wa kikazi na polisi hadi pale tume zilizoundwa
kuchunguza kifo hicho zitakapotoa taarifa sahihi juu ya mauaji hayo.
“Msimamo
wetu ni kusitisha uhusiano wa kikazi baina yetu na jeshi la polisi
hususan Mkoa wa Iringa, tumekuja hapa kwa sababu DCI umetuita na kama
unataka kutupa taarifa ya kifo cha ndugu yetu basi waambie hao maofisa
wa jeshi wa Iringa watoke nje,” alisema Leonard.
Akijibu madai
hayo Manumba alisema: “Nia yangu ni kutoa taarifa ya uchunguzi wa kifo
cha Mwangosi, ndiyo maana niliwasiliana na mwenzenu ili tuweze
kuzungumza, Polisi Iringa wataendelea kuwepo na waandishi wa habari
mtaendelea kuwepo, matukio kama haya yapo na yataendelea kuwepo.”
Licha ya maelezo hayo, hakuna mwafaka uliofikiwa na mkutano huo ukavunjika.
Akizungumza
kwa simu na gazeti hili baadaye, DCI Manumba alisema: "Ni vyema wao
wangenisikiliza kujua ninataka kuwaambia nini. Lakini, kwa kuwa kuna
mkanganyiko, nimeona ni vyema jambo hili lisubiri tume ndipo watakuja
kulizungumza.”
Imeandikwa na Habiel Chidawali, Dodoma, Hamida Sharrif Morogoro, na Tumaini Msowoya, Iringa na
Lasteck Alfred na Juliana Malondo.
1 comment:
CHADEMA CHUKUENI NCHI KWA SABABA HATAWALIKI HIVI SASA HA HA HA KILA MARA RAI WANAPIGWA NA MABOMU,MLIWACHEKA WAZANZIBARI SANA YAKO KWENU, DUWA LA KUKU HALIMPATAI MWEWE
Post a Comment