ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 18, 2012

Tanesco hakukaliki


Waziri mpya wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Katika kile kilichotafsiriwa kwamba ni hatua za kulisafisha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), shirika hilo limeanza mkakati wa kuhakiki vyeti vya wafanyakazi wake.

Habari ambazo gazeti hili limezipata zinaeleza kuwa zoezi hilo linatekelezwa kufuatia maelekezo kutoka kwa viongozi wa ngazi za juu wa Wizara ya Nishati na Madini ili kuhakikisha kwamba malalamiko na tuhuma zilizokuwa zikitolewa dhidi ya ajira za shirika hilo vinafanyiwa kazi.

Kumekuwapo na madai kuwa baadhi ya wafanyakazi wa Tanesco wamekuwa wakiajiriwa kwa upendeleo.



Kutokana na hali hiyo, habari zinasema kuwa uongozi mpya wa wizara hiyo umetoa maelekezo ya kufanyika kwa zoezi hilo ukiwa mkakati wa kuondokana na wafanyakazi wasiostahili.

Habari zaidi zinasema kuwa katika kutekeleza zoezi hilo, kila mfanyakazi atatakiwa kuwasilisha cheti halisi cha kuzaliwa na vya taaluma ili vihakikiwe.

Shirika hilo limethibitisha kuwepo kwa zoezi hilo kupitia Kaimu Meneja wa Uhusiano, Adrian Severin.

Hata hivyo,  Severin alisema zoezi la kuhakiki vyeti vya wafanyakazi wa Tanesco nchi nzima linafanyika katika utaratibu mzima wa kusimamia ufanisi wa wafanyakazi.

“Ni zoezi la kawaida ambalo hufanyika kila baada ya miaka miwili au mitatu na malengo yake pamoja na mengine, ni kuhakikisha kuwa kila mfanyakazi anafanya kazi kulingana na elimu aliyonayo,” alisema.

Severin alisema malengo mengine ya kufanya zoezi hilo ni kuhakikisha kwamba wafanyakazi wa Tanesco wanapanda vyeo kutokana na nafasi, elimu na uzoefu walionao pamoja na kuziainisha sehemu za ndani ya shirika ambazo wafanyakazi wanatakiwa waongeze elimu kutokana na mpango kazi wa shirika.

Zoezi la kuhakiki vyeti linafanyika wakati shirika hilo likiwa katika uchunguzi na ukaguzi unaofanywa na vyombo vya dola.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) inaendelea kuchunguza tuhuma mbalimbali za ubadhirifu ndani ya Tanesco, hatua ambayo ilitokana na jitihada za Waziri mpya wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) nayo ilipewa jukumu la kukagua hesabu za Tanesco baada ya kutolewa kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha katika shirika hilo.

Kadhalika, zoezi la kuhakiki vyeti vya wafanyakazi linafanyika wakati vigogo kadhaa wa shirika hilo wakiwa wamesimamishwa kazi kwa tuhuma mbalimbali.

Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco ilimsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, William Mhando na wafanyakazi wengine watatu ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka unaoikabili menejimenti hiyo.

Wengine waliosimamishwa ni pamoja na Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Huduma za Shirika, Robert Shemhilu; Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi Manunuzi, Harun Mattambo.

Vile vile, Tanesco inaendesha zoezi hili kwa wafanyakazi wake katika kipindi ambacho iko kwenye kampeni maalum ya kukamata wezi wa umeme kwa lengo la kuhakikisha kwamba umeme unaosambazwa unauzwa na mapato ya serikali hayapotei.

Katika kipindi cha mwaka mmoja (kati ya Agosti, 2011 hadi Agosti, 2012), shirika hilo limegundua matukio 3,858 ya wizi wa umeme kati ya wateja 71,080 waliokaguliwa.

Tanesco iligundua wizi wa umeme unaofanywa kupitia tokeni hewa za Luku, uniti hewa, service line za wizi na mita mbovu ambapo hujuma hizi pamoja na kukutwa kwa wateja, lakini wananchi pia wamewanyoshea mkono baadhi ya wafanyakazi wa shirika hilo kuwa ni washirika wa hujuma hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba, alithibitisha kuwa shirika lake limewachukulia hatua wafanyakazi 29 wa ngazi mbalimbali, wakiwemo mameneja wakihusishwa na makosa tofauti, likiwemo lile la kulihujumu shirika.

Mramba alisema baadhi ya hatua walizochukuliwa wafanyakazi hao ni pamoja na kushtakiwa, kufungwa na kuteremshwa vyeo.



 
CHANZO: NIPASHE

No comments: