WAANDISHI WA HABARI MKOA WA IRINGA WAKIMSIKILIZA DCI MANUMBA
WAANDISHI WA HABARI WAKITOKA NJEE YA UKUMBI BAADAYA YA KUSHINDWA KUFIKA MUAFAKA MZURI NA DCI MANUMBA
MANUMBA AKIONGEA NA WAANDISHI IRINGA
WAANDISHI
wa Habari wa mkoani Iringa wamekataa kupokea kupokea taarifa ya awali
ya uchunguzi ya mauaji ya mwanahabari Daudi Mwangosi iliyofanywa na
jeshi hilo iliyokuwa itolewe jana na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai
(DCI), Robert Manumba.
Hatua
hiyo imekuja baada ya Manumba kukataa kuwaondoa katika mkutano wake na
waandishi wa habari maafisa wa jeshi la Polisi wanaofanya kazi mkoani
hapa huku kukiwepo na tamko la waandishi hao kusitisha kufanya nao kazi
ya kihabari mpaka tume huru zilizoundwa zitakapotangaza matokeo ya
uchunguzi wao.
Pamoja
na wanahabari kukataa kupokea taarifa hiyo, Manumba alikanusha taarifa
zingine zinazodai kuwepo kwa waandishi wa habari wawili wanaodaiwa
kuwepo katika mpango wa kuuawa na baada ya mmoja wa wanahabari hao
Francis Godwin kujisalimisha na kumuhoji sababu za kutakiwa
ajisalimishe polisi.
Katika
kikao hicho kilichoitishwa majira ya saa sita mchana katika ukumbi wa
mikutano uliopo katika ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa,
wanahabari walionesha msimamo wao kwa kumtaka Manumba awatoe maafisa wa
jeshi hilo wa mkoani hapa.
“Waandishi
wa Habari wa Mkoa wa Iringa walikwishatangaza katika tamko lao kwamba
wamesitisha ushirikiano wa kihabari na jeshi hilo la Polisi mkoani hapa
mpaka pale tume huru zilizoundwa kuchunguza kifo cha mwanahabari huyo
zitakapotoa majibu yao,” alisema Frank Leonard ambaye ni Katibu Mtendaji
wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa.
Leonard
alimwambia Manumba kwamba waandishi wa habari hawana tatizo lolote na
yeye na kwamba wapo tayari kupokea taarifa yake hiyo ya uchunguzi ila
kwa sharti kwamba ni lazima maafisa polisi wote wanaofanya kazi mkoani
hapa na ambao walikuwepo katika chumba hicho cha mikutano watoke.
“Huu
ni msimamo wetu, hatupo tayari kufanya kazi na maafisa wa jeshi lako na
tunamuomba IGP Said Mwema ampumzishe kazi kwa muda Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Iringa bwana Michael Kamuhnada mpaka pale tume huru
zilizoundwa zitakapotoa taarifa za matokeo ya uchunguzi wao,” Leonard alisema alipokuwa akitoa ufafanuzi juu ya tamko la wanahabari hao.
Akiwasihi
wanahabari kushirikiana na jeshi la Polisi, Manumba alisema mara baada
ya mauaji hayo kutokea jeshi la Polisi makao makuu liliunda tume ya
uchunguzi akiwemo yeye mwenyewe ambayo kwa kiasi kikubwa imeifanya kazi
hiyo.
“Leo
nilikuwa nataka niwape taarifa ya uchunguzi ya mauaji hayo, lakini kwa
sharti mnalonipa sidhani kama hilo litawezekana,” alisema.
Alisema kila mtu ameguswa na mauji ya Mwandishi huyo na kwamba kosa lililofanywa na wahusika haliwezi kuwa kosa la kila mtu.
Bila
kufafanua Manumba alisema matukio ya aina hiyo yapo katika jamii yetu,
na yanaweza kuendelea kutokea ikiwa ni pamoja na kwake au maafisa wa
jeshi hilo.
“Jambo
hili baya limetokea na sisi Polisi tuna regret na hata serikali ina
regret, ndio maana tume iliundwa na mara moja tukakimbia kuja hapa ili
kupata ukweli baada ya kupeleleza na tukaona ni vizuri uchunguzi
tuliofanya tuutoe kwenu” alisema.
“Hata
hivyo kwa kuwa huu ni msimamo wa waandishi na wote mmeuunga mkono
mbele yangu, nadhani uchunguzi uliofanywa na jeshi letu itabidi upitiwe
na tume nyingine badala ya kuutoa kwenu,” alisema.
Hata
alipoombwa akatoe taarifa ya uchunguzi huo ambayo hata hivyo baadhi ya
wanahabari walisema inaweza kuwa na lengo la kuvuruga ushahidi
unaokusudiwa kukusanywa na tume zingine ikiwemo ile iliyoundwa juzi na
Waziri wa Mambo ya Ndani, Emanuel Nchimbi, DCI alisema tume iliyoundwa
na waziri inatakiwa iachwe ifanye kazi yake kwahiyo itapata fursa pia
ya kupitia uchunguzi wao huo.
Katika
kipindi hiki kigumu kwa wanahabari na wadau mbalimbali wa tasnia hiyo,
Manumba alisema yapo mengi yatakayozungumzwa kuhusu kifo cha Mwangosi
zikiwemo taarifa za uzushi, za kupikwa na za ukweli.
Kuhusu
kuwepo kwa taarifa ya orodha ya waandishi wahabari wengine wawili
wanaotakiwa kushughulikiwa na jeshi hilo, Manumba alisema hazina ukweli
kwani mbali na kufanya kazi na wadau wengine, jeshi hilo linawategemea
sana wanahabari katika kazi zake.
“Kwahiyo ndugu zanguni mkutano umefungwa na sasa tuiache tume ifanye kazi yake,” alisema.
IMEANDALIWA NA FRANCIS GODWIN IRINGA
1 comment:
Waandishi wa habari simamemi imara. Tanzania ni ya wote, hawa CCM na polisi wao hawawezi kuua na kisha mambo yapite tu hivi hivi. Hapana, haiwezekani.
Post a Comment