Hupaswi kufanya uamuzi ambao baadaye utakuja kubaini kuwa kuna eneo ulikosea. Makosa yako yatakufanya ujute.
Kwa nini ujute? Kila siku unapopatwa na jambo, unapaswa kutafakari kabla ya kuamua. Ukijijengea kanuni hiyo, utafika mbali katika maisha yako ya uhusiano. Siyo kimapenzi tu, bali pia hata kijamii.
Uamuzi wa jazba, kukimbilia kuacha ni tatizo lingine. Hapo sasa kirusi kinaweza kuwa wewe mwenyewe. Unatakiwa kujiangalia kwa makini mno. Pima kiwango chako cha hasira na tukio lenyewe halafu jikosoe. Jitahidi kupiga moyo konde mara nyingi iwezekanavyo.
Penda sana kujirudi, uamuzi wa kuacha uje baada ya kujiridhisha kwamba hakika mwenzi wako uliyenaye hawezi kukidhi viwango vya moyo wako. Uwe umejitahidi kumkosoa na kumsahihisha mara kadhaa. Ukiwa na tabia ya kuacha na kukimbilia kuanzisha uhusiano mpya, maana yake wewe ni kirusi.
Ni kweli kuwa mlango wa furaha unapofungwa, mwingine hufunguliwa lakini mara nyingi huwa hatujui thamani ya kitu tunachopata au tulichonacho mpaka pale tunapokipoteza. Sasa usifike huko, fanya upembuzi na uchambuzi wa kina. Heri kumsahihisha leo kwa udhaifu wake mdogo ili baadaye akupe furaha kamili na ya kudumu, kuliko kumuacha kisha ujute kwa miaka mingi wakati akiwa ameshakupa kisogo.
Naendelea kukubali kuwa kumpa mtu mapenzi yako yote haimaanishi naye atakupa au atakurejeshea kwa kiwango kilekile ambacho wewe umekitoa. Zingatia kwamba umeamua kupenda, usipende kwa matarajio ya kwamba naye atakupenda na kukujali kwa kiwango unachokiwaza.
Timiza wajibu wako, ukiona hakupi unachotaka tambua kwamba unayo nafasi ya kumuelewesha kile ambacho anatakiwa kukifanya ili ufurahie mapenzi yake. Fanya kazi nzuri kila siku, tambua kwamba wanaofanikiwa katika maisha ya kimapenzi ambao leo wanajisema wanakula bata ni wale walioamini katika kufundisha.
Pengine kuna vitu unavyotegemea kuvisikia au kuvipata kutoka kwake lakini haujaambulia chochote. Kabla ya kukimbilia kumtoa kasoro kwamba hakufai, hebu jiulize mwenyewe, ni lini ulimwambia unachopenda kusikia kutoka kwake? Umetaka awe anakwambia anakupenda, je, wewe umemwambia unampenda mara ngapi?
Usidai kile ambacho wewe mwenyewe hutekelezi. Unataka mwenzi wako awe anaonesha hisia za juu pindi mnapokuwa faragha, je, wewe huwa unamuonesha hizo hisia? Utagundua kwamba wewe unadai kile ambacho hukitekelezi kwake. Pengine hakuoneshi kwa kuamini hupendi.
Upo kwenye uhusiano, inapita miezi mitano hujawahi kumtamkia mwenzi wako neno “nakupenda”. Siku moja unajitahidi, unajitutumua unamwambia mpenzi wako “nakupenda sana my sweet love”. Kutokana na ugeni wake, anakujibu “asante.” Sasa jibu lake linakukera nini?
Ingekuwaje kama ungemwambia hivyo halafu naye akakujibu “najua”, si ndiyo pangechimbika. Mapenzi yanahitaji moyo wa subira. Akikujibu “asante” au “najua”, chukulia kwamba yote ni majibu, unachotakiwa kufanya ni kumfanya mwenzi wako atambue jibu la kukupa ili uwe na furaha. Wengine haya mambo ni ‘mashokolo mageni’, kwa hiyo hawajazoea.
Unaweza ukafanya uamuzi halafu baadae ukajutia, usiseme kwa heri kama unajisikia kuendelea, usiseme humpendi mtu tena kama unajua huwezi kumuacha aondoke . Hii ndiyo sababu ya kukutaka uishinde jazba. Amekuudhi leo, hebu lala kwanza ili kesho ulitafakari tukio ndiyo utoe uamuzi.
Kumbuka inachukua dakika kumuona mtu na kumtamani, ila baada ya huyo uliyemtamani, ukimuingiza ndani ya moyo wako na kumpenda, ni ngumu kumsahau. Wapo wanaoteseka maisha yao yote kwa kushindwa kuwaondoa kwenye vichwa vyao wale ambao waliachana nao. Wengine, hugharimu kabisa maisha yao. Acha jazba, uamuzi wako wa hasira leo, unaweza kukutuma kubwia sumu. Mimi nimeyaona.
KWA KUMALIZIA
Chunga sana ulimi wako. Maneno yako yanaweza kumfanya mpenzi aliyekupenda kwa moyo mmoja, akimbie. Tamka maneno matamu kwake, siyo yake la kumkera. Hakuna adhabu kubwa kwa mtu kama kumsemasema. Atakukimbia tu
CHANZO:GPL
No comments:
Post a Comment