ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, December 23, 2012

Lema spidi 120


“LEMA, jembeee, jembe limerudi, wamebana wameachia.” Ni baadhi ya maneno yaliyosikika kutoka kwa maelfu ya wafuasi wa Chadema, kumsifia Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, wakati wa mapokezi makubwa ya mbunge huyo mjini Arusha jana.
Aidha, Chadema kimetangaza kuwadai Sh250 milioni, wanachama watatu wa CCM waliomfungulia kesi Lema, ikiwa ni gharama za kesi hiyo.
Mapokezi hayo yalifunika na kusababisha shughuli mbalimbali kusimama kwa takriban saa 5, huku barabara nyingi na mitaa ikifungwa.
Lema alikuwa akirejea Arusha kutoka jijini Dar es Salaam, baada ya Mahakama ya Rufani Tanzania kumrejeshea ubunge wake, aliovuliwa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Aprili 5, mwaka huu.
Jaji Gabriel Rwakibarila alimvua Lema ubunge, baada ya kuridhika na ushahidi wa wanachama watatu wa CCM, Mussa Mkanga, Agnes Mollel na Happy Kivuyo na mashahidi wao kuwa mbunge huyo alitoa kauli za kashfa dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Batilda Burian.
Mbali na nyimbo za kumsifu Lema, wafuasi hao wa Chadema walikuwa wakikiponda Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Msafara wa mapokezi ya Lema aliyevaa fulana nyeupe iliyokuwa na maandishi kifuani yaliyosomeka; ‘Usiogope, Mungu yupo kazini G. Lema’, ulianzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ukiwa na magari na pikipiki zaidi ya 100 za wanachama na wapenzi wa Chadema, waliojitolea kuzijaza mafuta na kupakia abiria bila kulipwa.
Shughuli zote za kijamii, zikiwamo safari za magari na biashara katika barabara zote ulipopitia msafara wa Lema, zilisimama kwa muda kupisha msururu huo wa magari na watu kupita, huku waliolazimika kuegesha magari yao pembeni kupisha msafara wakionyesha alama ya vidole viwili inayotumiwa na Chadema.
Msafara kuelekea KIA ulianzia eneo la Phillips jijini Arusha, ukiongozwa na viongozi wa Chadema wilaya na mkoa wa Arusha.
Waliokosa nafasi katika magari ya wanachama na wafuasi wa chama hicho waliamua kusimamisha magari aina ya Coaster, yanayofanya safari kati ya Arusha-Moshi na kuyakodi kwa kujilipia Sh5,000 kama nauli ya kwenda na kurudi KIA.
Baada ya kufika KIA, msafara kutoka Arusha uliungana na uliotoka mkoani Kilimanjaro na kuanza safari ya kurejea Arusha Saa 4:00 asubuhi, safari iliyochukua zaidi saa tano, ambao uliwasili Uwanja wa Soko la Kilombero jijini Arusha saa 9:30 alasiri.
Kwa kawaida, safari kutoka KIA hadi Arusha mjini huchukua dakika 40 hadi 45, lakini jana, safari hiyo ilichukua muda mrefu kutokana na msururu mrefu wa magari, pikipiki na watu waliokuwa wakijitokeza njiani kuusimamisha wakishinikiza kusalimiana na Lema.
Kutokana na  hali hiyo, Lema, alilazimika kusimama katika vituo zaidi ya 20 ili kusalimiana na wananchi, ambao wengi wao walishika matawi ya miti mikononi kuashiria amani.
Vituo ambavyo Lema alilazimika kusimama baada ya wananchi kufunga barabara ni pamoja na Njia Panda ya KIA, King’ori, Kikatiti, Maji ya Chai, USA-River, Tengeru, Chama, Kwa Pole, Shangarai, Kambi ya Chokaa, Kwa Mrefu, Ngulelo, Kimandolu, Phillips, Mount Meru Hotel na Sanawari.
Mbunge huyo aliyepanda gari la wazi ili kukata kiu ya wananchi waliokuwa na hamu ya kumwona tangu KIA hadi Arusha mjini pia alisimama katika maeneo ya Clock Tower, Metro Pole, Friends Conner, Kilombero Sokoni kabla ya kuingia kwenye uwanja wa Kilombero National Housing, alikohutubia mkutano mkubwa wa hadhara.
Mapokezi hayo yalihudhuriwa na viongozi kadhaa wa kitaifa wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha), John Heche na wabunge Israel Natse wa Karatu, Joshua Nassari wa Arumeru Mashariki, Cecilia Paresso na Grace Kiwelu wa Viti Maalumu.
Katika hatua nyingine, Chadema, kimetangaza kudai fidia ya zaidi ya Sh250 milioni kwa wanachama watatu wa CCM, waliofungua kesi dhidi ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
Akihutubia mkutano wa hadhara baada ya mapokezi ya Lema jana, Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa alisema kuwa Chadema kimewasamehe wote waliohusika kutunga na kufungua kesi hiyo, lakini, hakitawasamehe kulipa gharama za shauri hilo kuanzia Mahakama Kuu hadi Mahakama ya Rufani.
“Chadema tumewasamehe bure, wote waliomhangaisha mbunge wetu kwa kipindi chote cha miaka mitatu, tangu uchaguzi mkuu uliopita kwa sababu tunajua walitumika kwa  tamaa na ushawishi wa fedha. Lakini, gharama zetu lazima walipe,” alisema Golugwa.
Akizungumza jana, Lema alisema kuwa kiasi cha Sh250 milioni kilichotajwa na Golugwa ni hesabu za haraka haraka na kwamba kiasi hicho kinaweza kuongezeka, baada ya mawakili wake na wataalamu wa hesabu kukokotoa hesabu.
Lema aliuchekesha umati uliohudhuria mkutano huo aliposema kuwa mnunuzi wa nyumba za mmoja wa waliomfungulia kesi, aliyemtaja kwa jina la Mussa Mkanga tayari amepatikana na yuko tayari kutoa malipo ya awali.
Mkanga ni mdai namba moja katika shauri la kupinga ushindi wa Lema lililokubaliwa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kabla ya kubatilishwa na Mahakama ya Rufani iliyomrejeshea Lema ubunge wake.
Pamoja na Mkanga, wadai wengine katika shauri hilo walikuwa ni Agnes Mollel na Happy Kivuyo ambao Mahakama ya Rufani imewaamuru kulipa gharama za shauri hilo tangu hatua za awali.
Lema  aliyekuwa amesindikizwa pia na baba yake mzazi alisema  kuwa amerudi kuwa Mbunge wa Jimbo la Arusha, kutetea watu wake na siyo masilahi yake, wala ya familia yake kwani kurejea kwake kumetokana na mshikamano wa wananchi.
“Kuna watu waliwahi kumfuata baba yangu na kumshauri eti aniambie, mimi sasa nimechaguliwa  kuwa mbunge, nikae na kujenga familia yangu, lakini nilimwambia hapana, mimi sikuchaguliwa kwa manufaa ya familia,”alisema Lema.
Lema aliwataka wakazi wa Arusha, kuwa na mshikamano na kupinga unyanyasaji wa aina yoyote, kwa kuwa chombo pekee chenye mamlaka ya kutoa hukumu ni mahakama.
“Kuanzia sasa nimerudi, ni marufuku mgambo kuwakamata ovyo na kuwapiga  vijana mitaani, maarufu wamachinga na akina mama ntilie kupigwa kama ambavyo imekuwa ikitokea, cha msingi muwe kitu kimoja, mjikinge na wasaliti kutetea haki zenu,”alisema Lema.
Lema alisema anarudi bungeni  ambapo atahakikisha  anashirikiana na  wabunge na viongozi wengine wa chama hicho kufa na kupona katika kuwatetea  Watanzania ili kunufaika na rasilimali zao.
Naye Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), John Heche, alitangaza kuwa Chadema kimejipanga kumpeleka Ikulu Katibu wake Mkuu, Dk Willbrod Slaa katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015, kutokana na wananchi kuchoshwa na uongozi wa CCM.
“Dk Slaa amewashinda CCM katika kiti cha ubunge Jimbo la Karatu kwa miaka 15 na alipojitokeza kuwania urais uchaguzi wa 2010 alitoa ushindani mkubwa, ambao bado unawatia hofu CCM uchaguzi ujao wa 2015. Ndiyo maana wanawatumia wasaliti wachache kujaribu kumdhoofisha,” alisema Heche.
Mwenyekiti huyo aliikumbusha CCM kuwa Dk Slaa wala Chadema siyo adui yao wala siyo sababu ya chama hicho kukosa haiba machoni pa umma, bali adui wa CCM ni CCM yenyewe iliyoshindwa kutimiza mahitaji ya umma.
Heche aliwataka Watanzania kupuuza kampeni za kumchafua Dk Slaa alizosema zimeanzishwa na kuratibiwa kwa  mamilioni ya fedha na watu kutoka ndani ya CCM wanaowatumia baadhi ya vijana wasaliti ndani ya Chadema.
Hata hivyo, Chadema hakijatangaza rasmi iwapo Dk Slaa ndiye atakuwa mgombea urais kupitia chama hicho mwaka 2015.
Mwananchi

No comments: