MAISHA yakaendelea, Khalid hakuwa mtu mwenye pesa nyingi lakini aliamua kutumia akiba yake kuhakikisha Gift anakuwa na furaha, anatimiza pia ndoto zake. Khalid alieleza ombi lake la kumtaka wawe na uhusiano wa kimapenzi na panapo majaliwa, waweze kufunga ndoa.
Gift ombi hilo alilikubali. Wiki moja baadaye, Khalid alimsafirisha Gift kwa ndege kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kufuatilia nafasi za kujiunga na Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Gift kusafiri kwa ndege, aliona ndoto, akamshukuru sana Khalid.
Alipata chuo, Khalid akamlipia ada, bweni na matumizi mengine. Kwa kifupi Khalid aligeuka baba kwa Gift, alimhudumia kila kitu. Gift alipopatwa na tatizo lolote, mtu wa kwanza kumpigia alikuwa ni Khalid ambaye alitatua bila kusita, akijua anajenga maisha ya mkewe mtarajiwa.
Kuna wakati ubinadamu ulimuingia Khalid, akawa anaomba kufanya mapenzi na Gift lakini hakufanikiwa. Siku zote Gift alimwambia asubiri mpaka watakapofunga ndoa. Japo Khalid ilimuuma lakini upande mwingine aliona msimamo wa Gift ni mzuri na alilegea kila alipokumbuka kauli tamu ya Gift: “Usijali mpenzi wangu, mimi ni wako, tutafanya mpaka utachoka.”
Siku, wiki, miezi, ikawa mwaka, miaka ikapita, Gift akamaliza chuo. Hakutaka hata kurudi Mwanza. Alichokikataa ni kuonana na Khalid. Alimuona mwanaume asiye na elimu, kwa hiyo kuwa na mume aina yake aliona kama ni kupoteza dira ya maisha. Wanaume wasomi ni wengi.
Khalid alijitahidi kufika Dar es Salaam, akaa mwezi mzima bila kuonana na Gift ambaye kwa kuona kero, akaamua kubadili na namba ya simu. Kutokana na uhusiano wao kutambuliwa mpaka na wazazi pamoja na ndugu wengine, aliwashirikisha lakini hakuna alichoambulia.
Sabrina ni rafiki yake Gift, akaamua kuingilia kati, kumshauri Gift atambue umuhimu wa Khalid kwa sababu pale alipo asingefika kama siyo mwanaume huyo lakini ushauri huo ulionekana sawa na takataka: “Sikiliza Sabrina, mimi ni msomi, daktari, natakiwa niwe na mwanaume msomi mwenzangu.”
Akaendelea: “Nilikuwa na Khalid kwa sababu alijipendekeza kwangu na alionesha anao uwezo wa kunisaidia. Nisingeweza kuacha hiyo nafasi lakini sasa hivi nimefanikiwa, Khalid kwangu wa nini tena? Ataniharibia tu maisha yangu. Lazima niyatengeneze maisha yangu kisomi.”
Gift alipoona msimamo wa Sabrina kwa Khalid umekuwa mkali, akimsisitiza anachokifanya siyo kizuri, alimjibu: “Hivi Sabrina, na wewe si mwanamke? Kama unamuona Khalid ni mwanaume wa maana sana, si uende akakuoe wewe? Tusisumbuane, kwanza yule siyo mwanaume wangu, sijawahi kutembea naye.”
Khalid alilia, machozi yakakauka, akaamua kuongeza juhudi kwenye biashara zake.
Hatua zilikuwa ndefu na mafanikio yaliendelea kwa Khalid. Akafanikiwa kuanzisha maduka ya nguo, Dar es Salaam, Mwanza na Arusha. Vilevile akaanzisha biashara mbalimbali ambazo zilimfanya kuwa anasafiri kwenda nchi mbalimbali.
Kutokana na historia yake ya kukosa mke kwa sababu ya elimu, aliamua kutumia utajiri wake kuanzisha mfuko kwa ajili ya kuwasaidia vijana wa kiume kujiendeleza kielimu. Alifanya mambo mengi makubwa, ikiwemo kujenga majumba ambayo baadhi aliyafanya kuwa ofisi zake kwa ajili ya kuratibu biashara zake.
Khalid alipotaka kufunga ndoa, akamuona Sabrina ndiyo mke sahihi kwake. Japo mwanzoni ilikuwa ngumu kueleweka lakini baadaye kilieleweka. Gift aliposikia Sabrina na Khalid wamefunga ndoa, moyo ukamuuma sana, aliumia zaidi kwa sababu wanaume wasomi aliowataka walimtesa sana.
Hata hivyo, hiyo haikumuuma kama siku alipoomba kazi kwenye hospitali binafsi inayoitwa KS Health Centre bila kujua inamilikiwa na nani. Siku anaitwa kwenye usaili ndipo aliposhtuka, kugundua kwamba hospitali hiyo ni ya Khalid lakini inasimamiwa na mkewe (Sabrina) ambaye naye ni daktari.
Gift baada ya kufanyiwa usaili, aliondoka kichwa kikiwa kizito. Wakati yeye alikwenda kwenye usaili akiwa na taksi na kuondoka kwa taksi, kwa macho yake alimshuhudia Sabrina anaendesha gari la kifahari aina ya BMW X6rangi ya chungwa.
Kwa haraka, Gift akaingiwa na mawazo kwamba kumbe maisha ya raha aliyonayo Sabrina, yangekuwa yake kama asingemdharau Khalid. Alimuona ni kijana aliyeishia kidato cha nne lakini ameweza kufanya mambo makubwa kumuwezesha kumiliki pesa na mali nyingi.
Mfano wangu una maana kuwa Gift ni mnyonyaji, alimuona Khalid ni daraja la kutimiza malengo yake kimaisha bila kuzingatia kwamba Khalid naye ni binadam. Kumbe badala ya kumfanyia visa, kumnynyasa, kumsimanga na kumdhalilisha kielimu, angeweza kushirikiana naye kujenga maisha bora.
Ingependeza kama Gift angeona umuhimu wa kutumia elimu yake kushirikiana na Khalid kujenga maisha lakini kwa sababu aliingiwa na ubinafsi, dharau kwa kumuona ni mwaume mbumbumbu, ndiyo maana baadaye akajuta. Ni sawa na mtu anayekumbuka almasi aliyoitupa, wakati akiwa bize anakusanya mawe.
Hakuna sababu ya kujuta baadaye, wala haitakiwa kuachana kisa mmoja amemuona mwenzake mnyonyaji, isipokuwa kila mmoja anapaswa kujiuliza na kupata jibu: “Ninapewa, je mimi natoa nini kwa mwenzangu?”
www.globalpublishers.info
1 comment:
mmhh!
Post a Comment