ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 24, 2013

Pombe toka Malawi zawagalagaza Vijana. Mbeya

* Paketi moja sawa na bia 8, huuzwa Shilingi 100. 
                  *Zazagaa Mbeya nzima, zadaiwa kupunguza mbegu za kiume

MIAKA takribani 11 tangu pombe kali aina ya Power No.1 super kadansana kutoka nchini Malawi kuua watu mkoani Mbeya, pombezingine zenye kilevi cha kati ya asilimia 40 na 42 zinaingizwa nchini Tanzania na kuathiri afya za watumiaji.

Kati ya pombe hizo ni aina ya Mowa Mafumu (pombe ya machifu) yenye kilevi asilimia 42 na Rider (chaguo la washindi) yenye kilevi asilimia 40.
Pombe hizo ambazo zipo kwenye makaratasi ya plastiki, zimezagaa kila kona ya wilaya ya Kyela, Rungwe, Mbeya mjini, Mbeya Vijijini, Mbarali, Mbozi na Momba huku zikiuzwa bei ya kati ya Sh.100-300 bei gharama ambazo vijana wengi wanaimudu na wanapokunywa wengi huzidiwa na kuanza kutokwa na jasho.
Hali hiyo imejidhihilisha baada ya Mwandishi wa habari hizi kutembelea wilaya ya Kyela iliyopo mkoani Mbeya na kukuta vijana wengi wakinywa pombe hizo ambazo wamekiri kuwa zinaathari kwa Afya zao.
Wakiongea kwa ombi la kutoandikwa majina yao, vijana wa eneo la Kasumulu, Kyela Mjini na Ipinda walisema kuwa wengi wanaotumia pombe hizo hugeuka vituko na wale wanaotumia vyombo vya moto hasa pikipiki huishia kugonga watu na baadhi yao kupoteza maisha.

’’Pombe hizi ni nzuri kwa bei lakini zina madhara makubwa kwasababu wengi tumewaona wakitumia pombe hizi huanza kutokwa jasho jingi katika miili yao jambo ambalo linaonesha kuwa pombe hizi zinakausha maji mwilini lakini vijana wanashindwa kuiacha kutokana na bei ni ndogo na hazikatazwi na Serikali’’ alisema mmoja wa vijana waliohojiwa.

Sanjari na hilo walibainisha moja ya athari iliyowahi kutokea kuwa ni kifo cha kijana mwenzao John Mwakapisye kilichotokea Julai 20,2010 baada ya kijana huyo kunywa pombe hizo kisha kuendesha pikipiki na baadaye kupinduka na kujisababishia kifo.

Waliongeza kuwa uwepo wa pombe hizo ambazo zinatengenezwa na kiwanda cha Bwenda Group Limited kilichopo mjini Lilongwe nchini Malawi kumetokana na kuadimika kwa pombe iliyojulikana kwa jina la Kadansana kutoka huko huko nchini Malawi.
Wakielezea kwa kina uwepo wa uholela wa pombe hizo ambazo wamekiri kuwa huingizwa nchini kwa njia za magendo, walisema kuwa pombe aina ya Kandasana nayo pia ilikuwa na madhara kwa watumiaji ambapo wengi wao hasa wanaume walikuwa wakiishiwa nguvu za kiume baada ya kunywa pombe hiyo.

’’Unashangaa hizi Mowa wa Mafumu na Rider! Mwanzo kulikuwa na pombe ilikuwa inaitwa Kadansana ambayo ilikuwa na athari kubwa zaidi kwasababu wanywaji hasa wanaume walikuwa wakiishiwa nguvu za kiume’’ alieleza mmoja wa vijana mjini Kyela.

Uwepo wa pombe hizo hapa nchini ni mwendelezo wa udhibiti mdogo wa dawa na vyakula hapa nchini hususani mkoa wa Mbeya ambapo hivi karibuni tuliweka wazi matumizi mabaya ya vidonge vya Crolofenical kutumika katika pombe za kienyeji huku Mamlaka ya udhibiti wa dawa na chakalu TFDA wakisema kuwa hawajui lolote.
Kwa upande wake mkaguzi wa TFDA nyanda za juu kusini Rodney O. Atananga, alisema utaratibu wa kukamata bidhaa zilizopigwa marufuku nchini na ambazo hazifai kwa matumizi ya binadamu huhusisha pia Jeshi la polisi na idara ya afya.
Alisema wamekuwa wakifanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kubaini ubora wa bidhaa zilizoko sokoni ili kubaini usalama wake na kama zinafaa kwa matumizi ya binadamu.


Atananga alisema watu wanaokamatwa na bidhaa hizo wanafikisha mahakamani kwa sababu ni kinyume na sheria ya chakula na dawa ya mwaka 2003 ambayo inakataza kuuza na kusambaza bidhaa ambazo hazijasajiliwa na kupigwa marufuku.
Alisema baadhi ya bidhaa zilizopigwa marufuku ni vipodozi vyenye viambato vyenye sumu pamoja na vinavyoingia nchini bila kibali au kusajiliwa.

Aliongeza kuwa bidhaa zenye viambapo vyenye sumu zinakatazwa kwa sababu zinamadhara kwa mwili wa binadamu ambapo alisema madara yake hutokea baada ya muda mfupi na mengine huchukua muda mrefu kujitokeza.

Alisema baadhi ya madhara hayo ni kansa ya ngozi na damu ambayo hujitokeza baada ya muda mrefu lakini madhara ya muda mfupi ni uharibifu wa ngozi na wajawazito kuharibu uzio wa ubongo wa mtoto akiwa tumboni pamoja na kuumwa kichwa.

Kwa sasa pombe kali zilizozagaa mkoani Mbeya ni pamoja na Zed pineapple spirit, double punch,Assorted sarit, Power na Rider can. 

HABARI KWA HISANI YA PASTOR GORDON KALULUNGA

No comments: