Akielezea ubadhirifu wa Tirdo, Kaimu Mwenyekiti wa POAC, Muhammad Chomboh, alisema mwaka 1996, Tirdo ilimlipa aliyekuwa mkurugenzi wa shirika hilo Sh. milioni 22 kwa ajili ya kulipia kodi ya nyumba jambo, ambalo lilikuwa ni kinyume cha mkataba.
Alisema Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) alibaini kuwapo kwa malipo hayo wakati mkurugenzi huyo alikuwa ameuziwa nyumba hiyo na Wizara ya Fedha.
Akijibu tuhuma hizo, Kaimu Mkurugenzi wa Tirdo, Ludovic Manege, alisema ni kweli kulikuwa na makosa ya ulipwaji wa fedha hizo mwaka 1996 hadi Machi, mwaka jana alipostaafu, na kusema maamuzi hayo yalitolewa na mkurugenzi mwenyewe.“Nakiri makosa yalifanyika na mpaka sasa fedha hizo hazijarudishwa, lakini mkurugenzi mwenyewe ndiye akiyeidhinisha malipo hayo kwa kuwa alisema aliteuliwa na rais kushika wadhifa huo,” alisema Manege.
Alisema mchakato wa kuzirudisha fedha hizo unafanyika, ikiwamo kuandaa mkataba mpya wa kumrudisha madarakani mkurugenzi huyo na kumwamuru kulipa fedha hizo.
Chomboh alisema kamati yake pia imebaini ununuzi hewa wa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh. milioni 155, vilivyokuwa vinatakiwa kutumika katika ujenzi wa boma lililopo Baganoyo.
Alisema mwaka 2010 Wizara ya Ujenzi ilitoa Sh. milioni 216 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa boma hilo, lakini Tirdo ilitumia Sh. milioni 155 katika ununuzi wa vifaa hivyo na Sh. milioni 61 zilizobaki hazikujulikana zilikokwenda.
Tirdo pia inatuhumiwa kuhifadhi fedha, ambazo siyo za shirika katika akaunti yake zenye thamani ya milioni 60, ambazo ziliingia kwa makosa kutoka vyanzo mbalimbali na taasisi hapa nchini pasipo kuzitolea taarifa sehemu.
Kutokana na makosa hayo, POAC ilikataa kupitisha hesabu za Tirdo na badala yake wakatakiwa kuandaa upya hesabu hizo na kupitiwa upya na CAG kabla ya kurudi tena kwenye kamati hiyo na kutoa onyo kali kwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Tirdo, kwa makosa aliyoyafanya.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment